Tuesday, March 5, 2013

Mbowe ataka CCM ipumzishwe 2015


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amemwagiza gavana mpya wa chama hicho katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Frank Mwaisumbe, kuunda mara moja baraza la watu 25 watakaokipumzisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushika hatamu ya uongozi hadi kufikia mwaka 2015.

Mwaisumbe alipokea maelekezo hayo jana siku chache baada ya kuchaguliwa wiki iliyopita kwa ajili ya kuingoza kanda hiyo. Kabla ya kuikwaa nafasi hiyo, aliwahi pia kuwa Mhadhiri wa Kitivo cha Uchumi na Biashara cha Chuo Kikuu cha Tumaini-Iringa (IUCo).

Mbowe alitoa agizo hilo baada ya viongozi na makada wa chama hicho mikoa ya Rukwa na Katavi kuomba mikoa yao kuingizwa katika kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayoundwa na mikoa ya Mbeya, Iringa na Ruvuma tofauti na ilivyokuwa imepangwa awali.

“Mwenyekiti ameniagiza kuunda baraza hilo mara moja na yeye atalizindua siku chache zijazo baada ya taratibu kukamilika. Anataka CCM ibaki historia katika mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya, Rukwa na Katavi wasiamini kitakachotokea ikiwamo kufutika katika nyanda hiyo,” alisema Mwaisumbe.

“Tutahakikisha kuwa kila ngazi kuanzia shina, tawi, kata hadi jimbo tunajaza nafasi zote katika chaguzi na hao wanaosema ufunguzi wa kanda za kichama hakuna maana watafakari watapata jibu sahihi kwamba ni kwa namna gani nchi nyingi za Ulaya zimepiga hatua kwa mfumo huo,” alisema gavana huyo.

Hata hivyo, Mwaisumbe amewataka wabunge wa CCM katika majimbo yaliyopo nyanda za juu kusini kukaa mkao wa kula kwa kuwa wanachopaswa kukifanya hivi sasa ni kujiandaa kuachia ngazi kuipisha nguvu ya umma.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment