Wednesday, March 13, 2013

CHADEMA yazuia wabunge wake

Mbowe: Tuko tayari wafukuzwe ila kamati ya Bunge haitawahoji

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kiko tayari wabunge wake wafukuzwe ubunge lakini hawatahojiwa na Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge kama ilivyotangazwa.
Msimamo wa CHADEMA unakuja zikiwa ni siku mbili tangu ofisi ya Bunge itumie Jeshi la Polisi kuwataarifu baadhi ya wabunge wa chama hicho kuwa wanahitajika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano na kamati hiyo.
Akitangaza msimamo wa CHADEMA jana mjini Musoma katika mkutano wa hadhara, Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe, alisema kuwa suala hapa si wabunge wa CHADEMA, bali wawakilishi wa wananchi.
Katika tamko hilo maalumu kama ‘Tamko la Musoma’, Mbowe alisisistiza kuwa kamwe wabunge wao hawatakwenda kuhojiwa kwenye hiyo kamati ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo, Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi (CCM).
Alisema kuwa kama ni kuwafukuza ubunge, wako tayari na kwamba Spika wa Bunge, Anne Makinda, ajaribu kufanya hivyo.

Wabunge wengi wa chama hicho pamoja na wengine wa NCCR-Mageuzi walidaiwa na Spika wa Bunge kuwa walifanya vurugu wakati wa kikao pale walipogomea uamuzi wa Naibu Spika, Job Ndugai, kuhusu hatua yake ya kuhitimisha kibabe hoja binfsi ya mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia.
Pia wabunge hao wanadaiwa kukwamisha kwa muda shughuli za Bunge katika kikao kilichofuata baada ya kusimama na kupinga uamuzi wa Ndugai wa kuiondoa hoja binafsi ya mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Mbowe aliwaambia maelfu ya wafuasi wa chama hicho kuwa kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Bunge namba 113 (7), inayozungumzia ukomo wa uhai wa kamati za Bunge, uhai wake unaishia mkutano wa kumi wa Bunge ambapo inakuwa ni nusu ya kwanza ya uhai wa Bunge lenyewe.
“Kwa hiyo kamati hiyo inayowaita wabunge wa CHADEMA, iliisha uhai wake siku Bunge la Kumi lilipoahirishwa, yaani Februari 8, 2013,” alisema Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na mbunge wa Hai.
Aliongeza kuwa kanuni ya 113 (10), inazungumzia nafasi ya mwenyekiti, kwamba uenyekiti wa kamati ya Bunge unakoma mkutano wa 10 ambapo inakuwa ni nusu ya uhai wa Bunge, kwa hiyo uhai wa Ngwilizi kama mwenyekiti uliisha Februari, siku ile Bunge lilipoahirishwa.
“Hivyo kwa mujibu wa kanuni za Bunge kamati hiyo haipo na mwenyekiti wake alishamaliza muda wake,” alisisitiza Mbowe.
Alisema kuwa wamewaita wabunge wa CHADEMA kwa sababu ya vurugu zilizotokea bungeni Februari 4, 2013, wakati wanajua kuwa kamati hiyo tayari ilishalifanyia kazi jambo hilo, ikatengeneza tuhuma, ikaendesha mashtaka, ikatoa hukumu, ikiwataja hata wahusika.
Wahusika waliotajwa ni Tundu Lissu, John Mnyika, Paulina Gekul (Viti Maalum) na Joshua Nassari.
Mbowe aliongeza kuwa watambue kuwa kamati hiyo inapokaa huwa ni sawa na mahakama, kwa kawaida kisheria na kikanuni, mahakama/kamati hiyo inapokuwa imeshaamua jambo haiwezi tena kamati hiyo hiyo kulikalia na kulifanyia kazi jambo hilo hilo.
“Mbele ya Watanzania wote, Tanzania nzima na dunia nzima ikisikia, kamati ile iliwahukumu wabunge wa CHADEMA bila hata kuwasikiliza itakuwa kichekesho; dunia nzima inajua hivyo, sasa wanataka kusikiliza nini tena, wakosaji wanajulikana, walihukumiwa bila hata kufuata taratibu,” alisema.
Kuhusu maandamano ya kumshinikiza Waziri wa Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa, na Naibu wake, Philip Mulugo, kuachia ngazi kutokana na matokeo mabovu ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni, Mbowe alisema yatafanyika Machi 25 mwaka huu katika majiji manne.
Aliyataja majiji hayo kuwa ni Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Arusha na hivyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi mitaani kushiriki maandamano hayo.
Mbowe aliwataka wenye baiskeli, bajaj, pikipiki, magari kujitokeza kwa wingi mitaani huku akilionya Jeshi la Polisi kutothubutu kuingilia kuvuruga maandamano hayo.
CHADEMA kupitia kwa Mbowe ilitoa siku 14 kwa waziri na naibu wake kuachia ngazi tangu Februari 18 mwaka huu, kama sehemu ya uwajibikaji kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni.
Alisema kuwa viongozi hao ndio walichangia matokeo hayo mabaya kutokana na kutowajibika ipasavyo hivyo lazima wahakikishe wanaondoka hata kwa kulazimishwa.
Mbowe alisema Kawambwa na Mulugo pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, wameshindwa kuiongoza sekta hiyo muhimu, ndiyo maana kwa sasa wanafunzi wanaishia kuandika matusi na kupata sifuri katika mitihani ya kumaliza kidato cha nne.
Alisema waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa ameliingiza pabaya na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini kumaliza elimu zao za msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika.
Katika matokeo hayo, Kawambwa alisema watahiniwa wote kwa ujumla waliosajiliwa walikuwa 480,036 kati yao wasichana 217,583 sawa na asilimia 45.33 na wavulana 262,453 sawa na asilimia 54.67 lakini waliofanya mtihani huo ni 456,137 sawa na asilimia 95.44, wengine 21,820 (asilimia 4.55) hawakufanya mtihani.
Katika matokeo hayo wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni 1,641, la pili 6,453, la tatu 15,426, la nne 103,327 na daraja sifuri wako 240,903.

No comments:

Post a Comment