Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinawatahadharisha wananchi kwa kile ilichokiita ‘mianya ya uchakachuaji’ katika muongozo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Chadema imesema mwongozo huo unaohusu muundo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya wilaya (mamlaka za serikali za mitaa) na uendeshaji wake, haujazingatia maoni ya msingi yaliyotolewa na wadau mbalimbali kikiwemo chama hicho.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema jana kuwa mianya hiyo imeachwa kwenye ngazi ya kamati ya maendeleo ya kata, ambayo wajumbe wake ni madiwani na wenyeviti wa mitaa na vijiji.
Alisema kwa mujibu wa matokeo ya chaguzi za mwaka 2009 na 2010, kuna hodhi kwenye vikao hivyo yaCCM.
Mnyika alisema muongozo huo umeminya mamlaka ya wananchi, kupitia mikutano ya vijiji na mitaa kwa upande wa Tanzania Bara kuwa ni kupendekeza majina na si kuchagua wajumbe.
“Muongozo umetangaza utaratibu tofauti kwa upande wa Zanzibar, ambayo wawakilishi wakichaguliwa na wananchi kwenye mkutano wa Shahia, majina yao yanawasilishwa moja kwa moja bila kuwa na mianya ya uchakachuaji kama ilivyo kwa Bara,” alisema.
Mnyika, Chadema inahimiza kuwa baada ya wananchi kuchagua wawakilishi wao kupitia mikutano mikuu maalum kwenye vijiji na mitaa, waingie moja kwa moja kwenye mabaraza ya Katiba bila kuchujwa na vikao vinavyotawaliwa na CCM.
Kwa mujibu wa Mnyika, upungufu katika mchakato wa ukusanyaji maoni ya wananchi binafsi, ulisababisha idadi ndogo ya watu waliotoa maoni ambayo mpaka awamu nne zinakamilika, walikuwa watu 318,223, sawa na asilimia 0.7 ya wananchi wote.
No comments:
Post a Comment