Wednesday, March 6, 2013

CHADEMA: Tutasimamisha mgombea urais Zanzibar

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza kusudio la kusimamisha mgombea urais visiwani Zanzibar katika uchaguzi wa mwaka 2015. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa chama hicho kusimamisha mgombea urais visiwani humo, tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa urejeshwe nchini Julai, 1992.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Zanzibar, Said Issa Mohamed, alisema kusudio la chama chake ni kusimamisha wagombea katika nafasi zote.

Alisema uamuzi wa CHADEMA kusimamisha mgombea urais Zanzibar, unatokana na Serikali ya umoja wa kitaifa kushindwa kutatua kero za wananchi.

Alisema baada ya CHADEMA kuona wananchi wanaanza kulalamikia Serikali hiyo kushindwa kutimiza ahadi na kusema walikaa na kuona umuhimu wa kusimamisha wagombea katika nafasi zote. 

“Tulitarajia mambo makubwa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, juu ya utatuzi wa matatizo ya ajira, manyanyaso, elimu bora, uhaba wa shule na walimu na masuala mengine yaliyoashiria uvunjifu wa amani kama tofauti za kidini.

“Lakini Serikali hii imeshindwa kabisa kutatua matatizo ya wananchi kama ilivyotarajiwa. Awali ilionekana kuwa CCM na CUF ndiyo vyama vyenye nguvu Zanzibar, huku CHADEMA ikirushiwa tuhuma kuwa ni chama cha udini.

“Hivi sasa hali ni tofauti kule Zanzibar, wananchi wenyewe wametuita na kutueleza matarajio yao na wakatuomba tufanye operesheni kama ilivyo Bara,” alisema Mohamed.

Alisema mtazamo na imani ya wananchi wa Zanzibar katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, imetoweka na badala yake wamekiona CHADEMA kama ukombozi pekee uliobaki kwao. 

Alisema binafsi katika mikakati hiyo amejiwekea mazingira ya kuhakikisha anashinda Jimbo la Wawi linaloongozwa na Hamad Rashid (CUF).

Alisema upokeaji wa kadi za CCM na CUF umeanza Pemba na kuongeza kuwa operesheni rasmi ya kanda inatarajia kuanza hivi karibuni.


Mtanzania

No comments:

Post a Comment