Wednesday, March 6, 2013

CHADEMA ilete muswada wa mabadiliko ya sheria ya Tume ya Uchaguzi


MWAKA wa tatu sasa tangu Uchaguzi Mkuu wa 2010 ufanyike na sheria ya uchaguzi ya Tanzania bado ipo kama ilivyokuwa Oktoba 30, 2010 na sheria ya Tume ya Uchaguzi bado iko vilevile.
Pamoja na matatizo yote ambayo tuliyaona wakati ule na ambayo mengine tuliyadokeza miezi kabla ya uchaguzi huo, bado sheria zetu za uchaguzi ziko vilevile.
Cha kushangaza zaidi ni kuwa mhanga mkuu wa sheria hizi mbovu na mfumo mbovu wa uchaguzi – CHADEMA, bado inaendelea kufanya kazi na kushiriki chaguzi ndogo kwa sheria zilezile zikisimamiwa na tume ileile.
Watu ambao walisimama kuilalamikia tume ya uchaguzi jinsi ilivyochelewesha matokeo na hata kuendesha uchaguzi vibaya bado wapo wakiendelea kuishi kana kwamba sheria za uchaguzi zimebadilika.
Lakini cha kushangaza zaidi ni kuwa watu hawa hawa ambao walilalamikia mfumo mbovu wa sheria kwenye chaguzi ndogo mbalimbali ndio hawa hawa wamekaa kimya leo wakiamini kuwa CCM na serikali yake itawafanyia hisani ya kuwapatia uchaguzi mzuri. Matokeo yake ni kuwa ili upinzani ushinde nguvu kubwa sana inahitajika ili kulinda “matokeo”.
Sasa hivi CDM inaonekana wamekubali demokrasia ya kulinda kura na wamefika mahali wanatoa mafunzo ya jinsi ya kulinda kura. Wao wenyewe wanaamini kwa kufanya hivyo wanatekeleza nadharia yao ya “nguvu ya umma”. Hili linashangaza. Nguvu ya umma ili takiwa itumike katika kushinikiza mabadiliko ya sheria ya uchaguzi, sheria ya msajili wa vyama vya siasa, sheria ya Polisi na ile ya Usalama waTaifa. Cha kuudhi ni kuwa CDM bado inalalamikia vyombo hivyo hivyo mwaka wa saba sasa!
Na hivi karibuni chaguzi ndogo kadhaa zitaitishwa nchini na tusipo angalia matatizo yale yale tutayaona tena na siasa zile zile za kutumia nguvu kubwa zaidi zitatumika na tusipoangalia kwa mara nyingine tena damu itamwagika kwa sababu tumekubali kuendelea kufanya siasa chini ya mfumo uleule mbovu, ukisimamia na sheria zile zile zilizotuingiza katika matatizo mara ya kwanza.
Ni kwa sababu hiyo basi kama kweli CDM inaamini ina nguvu ya umma nyuma yake, na kama kweli ina amini inapendwa na kukubalika basi umefika wakati ianze kupigania vitu vyenye matokeo y amoja kwa moja kuliko kuendeleza siasa za maandamano yasiyo koma ambayo matokeo yake kwa kweli ni vigumu kupima zaidi ya kuonesha picha za watu wengi, wakivaa magwanda wakiamini kuwa wanapendwa na kukubalika kweli kweli. Wakati umefika kwa CDM kuanza kufikiria kama mkakati wake wa kuandamana na kuhutubia mashabiki wake umeweza kubadili lolote katika mifumo ya siasa iliyopo.
Je, mikutano yote na maandamano yote na kauli kali za majukwaani ambazo viongozi wake wamekuwa wakizitoa zimemabadilisha sheria gani? Hivi kama pamoja malumbano yote na kelele bado Msajili wa vyama ni yule yule kweli tunaweza kusema mikutano hii imekuwa na matokeo chanya kweli?
Naam! Wapo watakaosema mikutano hii imepeleka chama vijijini zaidi na kuwa CDM inakubalika zaidi sasa hivi. Hivi kweli kampeni ya Dk. Slaa wakati wa uchaguzi haikuwa imekipeleka chama chini zaidi na kuifanya CDM ikubalike zaidi?
Binafsi nitapima matokeo ya mikutano na maandamano haya kuwa ni ya mafankio endapo:
  1. Mfumo wauandikishaji kura utabadilisha na kuhakikisha kuwa wakati wowote Mtanzania yeyote mwenye sifa ya kupiga kura anaweza kujiandikisha kupiga kura na siyo kusubiri hadi mtukufu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzia aamue lini ataboresha daftari la wapiga kura. Ni lazima uwepo mfumo mzuri, rahisi, na nafuu wa kuandikisha wapiga kura muda wote wa mwaka na hivyo kuwa na daftari lenye taarifa sahihi na za muda muafaka kuliko ilivyo sasa.
  2. Mfumo wa kufanya kampeni katika uchaguzi mkuu ubadilishe ili uruhusu watu kujiandikisha pia kupiga kura hadi siku chache kabla ya uchaguzi. Maana kama vyama vinafanya kampeni na kuvutia watu na watu hawawezi tena kujiandikisha kupiga kura kwa muda wa karibu miezi mitatu kabla ya uchaguzi kuna maana gani ya kufanya kampeni basi? Kampeni hazipaswi kuwa kwa ajili ya kuwaamasisha waliojiandikisha wakapiga kura bali zinapaswa kuwa sababu ya watu ambao hawajajiandikisha kujiandikisha.
  3. Mfumo wa kukusanya na kutangaza matokeo ya kura zote kuwa wakisasa zaidi ambao utahakikisha matokeo kutoka vituoni yanaripotiwa kwa usahihi zaidi katika vituo vya kanda.
  4. Hili ni muhimu badala ya mfumo wa sasa ambao watu wote wanaangalia Makao Makuu ya Taifa ya Tume. Kila kanda inakuwa huru kutangaza matokeo yake ya uchaguzi na tume ya taifa jukumu lake ni kukusanya tu matokeo ya kanda na kuyajumlisha na kuyatangaza kisheria. Hii ina maana mtu mwingine yeyote (vyama na vyombo vya habari) akiweza kukusanya matokeo kutoka kwenye kanda zote basi matokeo yake ni LAZIMA yawe sawa na yale yatakayo tangazwa na Tume ya Taifa.
  5. Mfumo wa sheria ya vyombo vya usalama ibadilishwe ili kuhakikisha kuwa vyombo vya usalama haviingilii kabisa mchakato wa uchaguzi isipokuwa katika kuhakikisha usalama wa uchaguzi.
  6. Haviruhusiwi kutoa kauli yoyote ambayo inaweza kuonekana kupendelea serikali au chama fulani cha siasa. Hatutaki mambo ya Shimbo ya 2010 yarudie tena. Na JWTZ likatazwe kujiingiza katika siasa kabisa kwa kutakiwa kisheria wapiganaji wake kubakia kambini.
  7. Endapo hali inatokea kuwa Jeshi la Polisi limeshindwa kudhibiti hali ya usalama basi uongozi wa Jeshi la Polisi utoe tamko hadharani na kuialika JWTZ na kwa kufanya hivyo viongozi wa Polisi watatakiwa kukaa pembeni ili jeshi lirudishe amani na utulivu. Hatuwezi kuwa na vyombo viwili ambavyo vyote vinajaribu kusimamia hali ya usalama bila kujua nani yuko juu ya nani.
  8. Sheria ya uchaguzi ibadiliswe ili kwamba kiongozi yeyote wa kisiasa au wa kidini ambaye ataonekana ametoa kauli au kufanya vitendo vya kutishia amani basi kama ni mgombea ataondolewa. Haijalishi ni nani na anagombea nafasi gani. Lugha za kibaguzi na kidini tulizo shuhudia huko nyuma zijekurudiwa tena.
Hayo ni mambo baadhi tu. La msingi ni kuwa CDM ianze kupigania vitu vyenye matokeo kweli kweli katika kubadilisha mfumo. Ikumbukwe kuwa hatutaki kubadilisha watawala ili kubadilisha sura tu; lengo la kutakakubadilisha watawala ni kubadilisha utawala. Na sasa hivi, CDM haionekani inapigania kubadilisha utawala.
Sasa badala ya kuleta “hoja binafsi” CDM ioneshe kuwa ni chama cha upinzani kwa kuandaa miswada binafsi ya sheria au mabadiliko ya sheria ili tujue wao wanataka mifumo yetu ya utawala iweje.
Imechosha kuwasikia na wao wanataka serikali ilete ‘sheria’ au serikali ifanye ili au lile. Ni wakati tuone CDM ikiandika sheria ambazo ingependa ziwepo nchini. Hata kama hazitopita bungeni lakini angalau tutajua mawazo yao ni nini katika kubadilisha mifumo ya utawala nchini.
Hivi sasa hatujui wanataka kufanya nini wakija kushika madaraka. Hatujui sheria zitakuwaje chini yao. Wasije kutuambia kuwa tuwachague kwanza halafu wakishafika madarakani ndipo watafikiria ni sheria gani na vipi watazibadili.

No comments:

Post a Comment