Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kuwa safari ya CCM kuingia Ikulu 2015 imefika mwisho.
Hayo yalielezwa na wabunge wa Kanda ya Ziwa Mashariki yenye mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara katika mkutano uliofanyika mjini Maswa ambako ndiko yaliyoko makao makuu ya kanda hiyo.
Wabunge hao waliokuwa wameongozana na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Taifa la chama hicho, Shilugushela Nyangaki, walieleza kuwa pamoja na chama hicho kuwa madarakani kwa miaka 51 bado wananchi wa Tanzania ni masikini wa kutupwa kutokana na sera za CCM.
Katika mkutano huo wabunge hao, Rahel Mashishanga (Viti Maalum), jimbo la Shinyanga, Silvester Kasulumbayi, mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki, Meshack Opolukwa mbunge wa jimbo la Meatu na mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi John Shibuda, walisema serikali ya CCM imewatelekeza wananchi wake katika sekta za elimu, afya, maji miundombinu na hata chakula.
Wakizungumzia elimu hususani matokeo ya kidato cha nne, Mashishanga na Opolukwa walisema kuwa mitaala ya elimu kuanzia shule za msingi hadi sekondari ni mibovu na hata kufanya vibaya kwa wanafunzi wengi wa kidato cha nne mwaka 2012 ni kutokana na mgomo baridi wa walimu kuanzia shule za awali hadi vyuoni.
Walisema kuwa kuwapo kwa hali hiyo sasa Tanzania itarajie kuwa na taifa mbumbumbu kutokana na mfumo mbaya wa elimu na kushauri kuwa serikali iwajali walimu kwani wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu.
Kuhusu afya, wabunge hao walisema kuwa wananchi wamekuwa wakihaha kupata madawa na kuwapo kwa migomo baridi kwa madaktari na wauguzi hasa maeneo ya vijijini.
Opolukwa alisema kuwa serikali ya CCM imekuwa ikifanya mzaha na elimu kwani watoto wanaofaulu ni wasiojua kusoma na kuandika huku waziri mwenye dhamana akikataa kuwajibika kwa kujiuzulu .
Wakizungumzia kutelekezwa kwa wakulima wa zao la pamba, Opolukwa alisema wakulima wameshindwa kunufaika na kilimo cha zao hilo hasa ikizingatiwa kuwa wamekuwa wakinunua mbegu ya pamba kwa Sh. 1,200 kwa kilo na kuuza kilo moja kwa Sh. 660 jambo ambalo halimsaidia mkulima kumwondolea umasikini.
Naye Shibuda alisema kuwa serikali ya CCM imekuwa ikikopa fedha nyingi badala ya kuzitumia kuwasaidia wakulima imekuwa inatumia mabilioni kwa anasa na safari lukuki za viongozi nje wakiambatana na msafara mkubwa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment