JAMBO usipolijua ni sawa na usiku wa giza, na ni wazi kuwa hata ngoma ambayo huwezi kuicheza pia huwezi kujua utamu wake. Inawezekana mgongano huo wa semi ukawa sehemu ya kile ambacho leo nataka kukisema.
Nilikuwepo wakati wakazi wa mikoa ya nyanda za juu kusini; Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma kwa nafasi zao walivyoshiriki mkutano mkubwa na wa aina yake ulioandaliwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wiki hii jijini Mbeya.
Waliofika kwenye mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya Luanda-Nzovwe watakubaliana na mimi kuwa ulijenga sura ya utaifa zaidi kuliko ya kichama na hasa kutokana na hoja za msingi zilizozungumzwa hapo ikiwamo anguko la elimu hapa nchini.
Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe kwa msisitizo mkubwa alizungumzia hali mbaya ya mfumo wa elimu katika nchi hii na ufaulu mbovu wa wanafunzi.
Mwisho wa hotuba ya Mbowe, wananchi waliimba nyimbo za kulaani mfumo mbovu wa elimu na wakikubaliana kwa pamoja kuwa ipo haja ya msingi kabisa, mawaziri wenye dhamana na wizara ya elimu wajiuzulu. Jambo kubwa lililojitokeza kwenye mkutano huo ni hilo.
Pia wananchi walipata fursa ya kuambiwa kuwa mfumo wa uundwaji wa mabaraza ya katiba ya wilaya ngazi ya mamlaka za serikali za mitaa ni haki ya kila mwananchi kuweza kushiriki na kwamba dhana kubwa hapo ilikuwa lazima wananchi washirikishwe na wameshirikishwaje kutoa maoni.
Mambo yaliendelea katika mkutano huo, na haukupita muda mrefu wakaguswa na hoja ya upatikanaji wa vitambulisho vya uraia na mgongano unaoweza kujitokeza wengine wakipata na wengine kukosa.
Wengi walionesha shaka namna vitambulisho vya uraia vinavyoweza kutolewa kwa urasimu.
Kwa ujumla wake mkutano huo uligusa mambo mengi ya msingi ambayo kwa siku zijazo serikali inapaswa kuharakisha kuyafanyia kazi kabla jua halijazama.
Wananchi wanataka kufahamu haki yao ya msingi ya kupiga kura mwaka 2015 itakuwa na mwongozo gani. Je, watatumia kadi za kupigia kura walizopatiwa katika chaguzi mbili kuu za nyuma zilizopita au watatumia vitambulisho vyao vya uraia?
Mengi yalijitokeza, lakini jambo la msingi ninalotaka kuligusia hapa ni namna wanachama, wapenzi wa chama hicho kikuu cha upinzani na wananchi wengine kwa ujumla walivyoshiriki mkutano huo kwa amani na utulivu mkubwa.
Katika viwanja hivyo vya Luanda- Nzovwe amani ilitawala kwa asilimia 100, wananchi walikuwa na uhuru wa kushangilia na kurukaruka bila kubughudhiwa na chombo chochote cha usalama, walijivunia mazingira mazuri na maandalizi ya mkutano huo kwa muda mfupi.
Ndiyo maana nasema kuwa amani itawale CHADEMA hadi mwaka 2015 wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ili kuweza kuondoa mtazamo mchafu na propaganda zinazopigwa kila siku kuwa wananchi wa mikoa ya nyanda za juu kusini sio wastaarabu.
Kwamba wananchi wa mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma wanatawaliwa na vurugu, jambo ambalo halina ukweli wowote.
Kilichotokea mwishoni mwa wiki hii kwenye mkutano wa CHADEMA kinadhihirisha wazi kuwa wananchi sasa wana mwamko mkubwa wa kujitokeza na kusikiliza mikutano ya hadhara.
Kwa utulivu uliokuwepo na hali ya usalama ilivyokuwa imeandaliwa kisayansi, naamini kwa mwendo huo ipo haja vyombo vingine vya dola, hususani Jeshi la Polisi wakaenda Mbeya kujifunza na wanapaswa kujiuliza wenzao wanawezaje kusimamia mikutano mikubwa na ikamalizika kwa amani na utulivu mkubwa.
Jambo la msingi na la kujifunza ni kwamba ni dhambi polisi kuwapiga mabomu, au kuwatisha wananchi kwa vipaza sauti wakati ndio waliotoa kibali ili kuruhusu mkutano ufanyike.
Polisi wa Mbeya wanajua kazi na majukumu yao kuwa ni kulinda usalama wa raia na mali zao, jambo ambalo walilifanya kwa asilimia 100.
Naamini wakati hali ikiwa shwari mkoani Mbeya hasa katika mikutano inayoandaliwa na vyama vya upinzani, ipo haja vyama vyote vya siasa vikaacha tabia ya kuwachochea wafuasi wao kuwa chama fulani kikifanya mkutano wake lazima vurugu zitokee, jambo ambalo ushahidi wake haupo.
Ni vyema kila chama kikajitathimini kwa wananchi kuwa je, kinakubalika? Je, wananchi wanavutiwa nacho? Je, kina hoja za msingi za kuwaambia wananchi na utayari wa kuweza kutatua matatizo yao au njia pekee iliyobaki ni kupiga propaganda za uongo kuwa chama hiki wanachama wake wana vurugu?
Kwa hali iliyotokea jijini Mbeya, nina kila sababu ya kuwapongeza wananchi wa mikoa hiyo yote waliounda kanda ya kichama kwa kufanya mkutano mkubwa uliozungukwa na amani kila kona, pia Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa ya kulinda na kuongoza maandamano ya amani bila bughudha.
Siku zote ujenzi wa demokrasia imara katika nchi yoyote utawaacha polisi wakiwa hawana kazi kama watatekeleza vyema wajibu wao, lakini polisi wanapofanya kazi ya kutumika na hasa wanapotumiwa kwa maslahi ya watu wasiowajua, wanajikuta wakipambana na wananchi bila sababu za msingi.
Heshima ambayo Jeshi la Polisi itaendelea kupata kutoka kwa wananchi ni kuzidisha dhana ya ulinzi shirikishi, kuwasogeza wananchi wema jirani na vyombo vya dola katika masuala mbalimbali bila kusahau kuwa siku zote siasa huvuta wananchi wengi kwa pamoja kuliko jambo jingine.
Tabia iliyooneshwa katika mkutano huo wa Mbeya, uliokuwa na mkusanyiko mkubwa wa wananchi kupita kiasi na ukamalizika katika hali ya usalama wa kutosha, si jambo la kupuuzwa siku zijazo.
Najua nini umuhimu wa kulinda amani katika medani za kisiasa. Mara nyingi adui huweza kujipenyeza mahali ambako amani haipo na jambo lolote linaposhindwa kufikia malengo yake, watu hukimbilia kusema kuwa hapa hapakuwa na amani ndiyo maana mambo yameharibika.
CHADEMA wanapaswa kuitunza tunu ya amani kama walivyoweza kujionesha wazi kwenye mkutano wao wa Mbeya, ambapo hakika kila chama cha siasa kilichofika hapo kujionea, kina jambo la kujifunza kutoka kwa wenzao waliooandaa mkutano huo.
Basi tupinge mawazo potofu na mtazamo wenye chuki unaoandaliwa na watu wabaya wanaotumia majukwaa ya siasa kuwaambia wananchi kuwa vyama vya upinzani ni vyama vya vurugu.
Tuamini kuwa wale waliofika kwenye mkutano huo si wajinga, wamejionea na wameweza kujidhihirishia kuwa Watanzania wamefika mahali ambako hawadanganyiki tena. CHADEMA amani iwe nanyi hadi 2015, mtavuna mnachopanda.
Christopher Nyenyembe
No comments:
Post a Comment