SERIKALI ITOE MAELEZO
YA KINA KWA VIJANA NA WANACHI WA MTWARA KWA UJUMLA JUU YA RASILIMALI YA GESI ASILIA
Wananchi wa Mtwara wameandamana kupinga zoezi la serikali kusafirisha
gesi asili inayotoka mkoani humo hadi Dar es salaam. Wengi wa walioandamana walikuwa
ni vijana waliobeba mabango yenye ujumbe mbalimbali kwa watawala kuhusiana na
rasilimali hiyo.
Kwetu sisi BAVICHA, wananchi wa Mtwara hususan vijana wana
haki ya kupinga hilo kwa sasa ili kuepuka yale yanayotokea kwenye maeneo
mengine ya nchi yetu ambayo rasilimali zake zimekuwa zikitapanywa huku si
wananchi wa eneo husika wala taifa wakinufaika vyema na rasilimali hizo hasa
kwa Maendeleo endelevu. Maeneo yenye mathalani migodi ya dhahabu na almasi ni
kielelezo tosha cha jambo hili.
Wanachopinga Vijana na wananchi wa Mtwara kimsingi sio gesi
kusafirishwa kwenda Dar es salaam bali ni wao kuelezwa na kuoneshwa watanufaika
vipi na gesi asili jambo ambalo serikali
haijaweza kulifanya mpaka sasa.
Maandamano ya watu wa Mtwara hususani vijana kwa upande mwingine
ni kielelezo tosha cha jinsi sera za Chama cha Mapinduzi zilivyofubaa na hivyo
kutokidhi haja za watanzania ambao mpaka sasa ni maskini wa kutupwa.
Mfumo mbovu wa utawala wa Tanzania chini ya serikali ya CCM
ndio umetufikisha hapa na wananchi wa Mtwara na mikoa ya jirani wanapaswa
kuelewa hilo. Kwani kwa sasa mfumo huu umeweka mamlaka yote ya kuamua la
kufanya Dar es Salaam (Ikulu) juu ya rasilimali za taifa bila kujali mahitaji
halisi ya wakazi wa eneo husika na hata taifa kwa ujumla . Na kwenda kinyume kivitendo na kile
wanachokihubiri kuwa na “serikali sikivu” kumbe ni “serikali kiziwi na babe”.
BAVICHA inasisitiza kuwa tatizo la matumizi mabovu ya rasilimali si la Mtwara pekee bali
ni la nchi nzima ambako rasilimali nyingi ambazo matumizi yake mpaka sasa
hayajawanufaisha wakazi wa maeneo hayo wala taifa. Serikali ya CCM haina sera
makini na daima haitakuwa nazo zaidi ya ubabaishaji uliopo na ambao umekuwapo
kwa zaidi ya miaka 51 sasa.
BAVICHA inawataka Vijana na wananchi wa Mtwara na Tanzania kwa
ujumla kuelewa kuwa mbadala halisi wa sera haramu ya CCM na Serikali yake ambayo
CHADEMA imekuwa ikiwaeleza wananchi ni ile ya kubadili mfumo wa utawala wa sasa
wa kila kitu kuamuliwa Dar es salaam na kuweka mfumo mpya unaotokanana sera ya
MAJIMBO. Sera ambayo licha ya kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali za taifa
kwa manufaa ya taifa zima, pia unawapa mamlaka wananchi wa eneo husika lenye
rasilimali hizo kuamua njia bora za kuzitumia rasilimali hizo kwa maslahi yao
pia na kuhakikisha maslahi ya taifa zima.
Kwa sera hii ya CHADEMA ya mfumo mpya ya Utawala kwa njia ya
MAJIMBO, rasilimali kama ya Gesi asili ingekuwa msaada kwa wananchi wa eneo la
Mtwara (na Lindi) ambako mitambo ya gesi ingefungwa huko Mtwara (na Lindi) na
kuzalisha kama ni umeme ungezalishwa
huko huko na kuingizwa kwenye gridi ya taifa. Kama ni viwanda basi vingejengwa
Mtwara (na Lindi) na kuzalisha bidhaa husika na kisha kusafirishwa kwenye
maeneo mengine ya nchi yetu. Kwa mtindo huu ajira kwa Vijana wa Mtwara na
maeneo ya jirani zingepatikana kwa wingi na kuinua uchumi wa watu wa Mtwara na
Lindi. Jambo ambalo lingeondoa tatizo la uhamaji wa nguvu kazi toka vijijini
kuja mijini kama Dar es Salaam ambalo kwa sasa linakua siku hata siku.
BAVICHA tunasisitiza pamoja na wanachi wa Mtwara na hata
mikoa mingine ambayo ina rasilimali
nyingi ambazo mpaka sasa zimegeuka kuwa laana kwa taifa hili, kupinga kitendo
hiki cha matumizi mabovu ya rasilimali, wanapaswa kuunga mkono Sera ya CHADEMA
ya kuweka mfumo mpya wa Utawala wa MAJIMBO ambao utazuia ukwapuaji na
utoroshaji wa rasilimali hizi kutoka kwenye mikono ya wanachi wa Tanzania. Ni
Mfumo ambao licha ya kuweka rasilimali
hizi kama gesi ya Mtwara (na Lindi) mikononi mwa wananchi, pia itawapa nguvu ya
kufanya maamuzi yao juu ya rasilimali
hizo na kuwawajibishwa viongozi wao wanaoshirikiana na kikundi cha watu wachache
kuzitorosha na kuwaacha wao wananchi wakiwa wasindikizaji kama si washangaaji
wa matumizi ya rasilimali zao. Na hii ndiyo demokrasia ya kweli kwa maendeleo
endelevu kwa taifa kwa kuhakikisha ushirikishi hai na mpana wa wananchi wote.
Imetolewa leo tarehe 30/12/2012 Jijini Dar es salaam na:
Deogratias Munishi
Katibu Mkuu –BAVICHA
No comments:
Post a Comment