Sunday, November 18, 2018

NIA OVU KATIKA MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA VYAMA VYA SIASA, 2018


CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

 NIA OVU KATIKA MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA VYAMA VYA SIASA, 2018


 UCHAMBUZI MFUPI KWA AJILI YA VYOMBO VYA HABARI

_______________

 Mtizamo wa vifungu vichache:

Muswada unaanzisha  Kifungu cha 3 juu ya kazi za Msajili ili zijumuishe pamoja na mambo mengine kufuatilia mfumo wa chaguzi ndani ya vyama na pia utaratibu wa uteuzi. Jambo hili kwa hakika ni kuingilia mfumo wa kidemokrasia ndani kabisa ya vyama vya siasa, kitu ambacho kinafanywa kwa mujibu wa katiba za vyama vyenyewe. Nia mbovu katika hili ni kule kutaka kuamua juu ya khatma ya uongozi ndani ya vyama vya siasa – lengo kuu likiwa ni vyama vya upinzani.

Muswada unaweka kanuni kali juu uendeshaji  wa  elimu ya uraia ndani ya nchi na kwa mujibu wa Kifungu 5A(1)  “ Mtu au taasisi iliyosajiliwa ndani au nje ya Jamhuri ya Muungano itakayo kusudia kuendesha elimu ya uraia au aina yoyote ile ya mafunzo ya uwezeshaji au nia kama hiyo kwa chama cha siasa, italazimu kabla ya kufanya mafunzo kama hayo, kumuarifu Msajili kwa maandishi juu ya madhumuni na aina ya programu ya mafunzo hayo, watu wataohusika katika mafunzo hayo, visaidizi vya kufanyia mafunzo na matarajio ya mafunzo hayo.”  ( Sio tafsiri rasmi)

Zaidi ya hapo Muswada unaeleza katika Kifungu kidogo (2)  kuwa  “ Baada ya kupokea taarifa chini ya Kifungu kidogo (1),  Msajili anaweza kuyakataa mafunzo hayo au program ya uwezeshaji huo na kutoa sababu ya kukataa kwake. Kwenda kinyume na kifungu hiki kunaweza kupelekea kutozwa faini ya juu kabisa ya isiyozidi shs 30 millioni, kifungo kisichopungua miezi 6.” (Sio tafsiri rasmi)


Nia ovu katika Kifungu hiki ni kuzuia ushirikiano na kusaidiana baina ya vyama rafiki, hasa vile kutoka nje ya nchi.


Kifungu cha 5B (1) Muswada unasema Msajili anaweza kudai taarifa yoyote kutoka Chama cha Siasa, kiongozi au mwanachama yeyote juu ya chama cha siasa.


Nia ovu iliopo hapa ni kule kupewa mamlaka ya kuuliza “chochote”  kwa sababu taarifa au mambo mengine ni ya faragha na hayana mnasaba wote na mas-ala ya siasa na si ya kikatiba.


Nacho Kifungu cha 6 kinasema  “Hakuna kesi/shauri litakalokuwa dhidi ya Msajili, Msajili Msaidizi, Mkurugenzi  au maafisa wowote chini ya Msajili kwa kitu chochote kitakachofanywa au kutokufanywa kwa nia njema katika utekelezaji wa kazi chini ya sheria hii.”


Nia ovu katika Kifungu hiki ni kuwekwa kwa kinga kwa ofisi nzima ya Msajili jambo ambalo linakwenda kinyume na misingi ya uwajibikaji na  ni jambo linaloweza kupelekea kutumika vibaya kwa madaraka kwa mgongo wa kinga hiyo.


Nako tena kuna Kifungu cha  6A (6)  ambacho kinasema “ Chama cha siasa hakitafanya kazi ya kuwa kikundi cha shindikizo au cha uana harakati” (Sio tafsiri rasmi).


Tujuavyo sisi ni kuwa kwa maumbile yake vyama vya siasa ni vikundi vya shindikizo na vya uana harakati. Vina wajibu wa kuibua na kueneza uelewa wa masuala mbali mbali ya umuhimu katika jamii na vinapaswa kuwa ndio mdomo wa wanyonge.


Kuvikatalia vyama vya siasa wajibu huu wa kusemea wasiokuwa na sauti ni sawa sawa kabisa kuwa kama vimepigwa marufuku.


Kifungu cha 8D kinaeleza kuwa Waziri ataamua juu ya khatma ya katiba za vyama vya siasa kupitia kanuni. Ziada ya hilo katika kifungu hiki Msajili anapewa mamlaka ya kuamuru chama chochote cha siasa kurekebisha kifungu/vifungu vya katiba za vyama hivyo ndani ya miezi 6, ikiwa atakuwa ameona kifungu/vifungu hivyo haviendani na masharti ya Sheria.

Uchambuzi: Katiba ya Chama cha Siasa ni andiko ambalo linaakisi utaratibu wa kujiendesha ambao wanachama wamekubali kuwafunga pamoja na juu ya namna wanavyotaka katiba hiyo iwe kiongozi kwao.


Kumpa mtu mwengine fursa ya kutia mkono kwenye Katiba za Vyama cha Siasa ni kuingilia uhuru na utashi wa wanachama wa vyama hivyo ambao wamechagua juu ya mfumo wa chama chao na undeshaji wa kazi zake uwe.

Kwa ujumla Muswada huu unamgeuza Msajili wa Vyama vya Siasa au ofisi hiyo sasa kuwa ni Mamlaka ya Usimamizi

Muswada huu una jinaisha siasa nchini Tanzania. Umejaa adhabu za faini na pia vifungo kwa makosa maduchu maduchu. 

Muswada unaingilia uhuru wa mtu mmoja mmoja wa maaumuzi, kukusanyika na uhuru wa kujieleza ambao huwa ni zaidi ya kutoa kauli au kuandika.

Muswada unampa mamlaka Waziri ambae vyama vya siasa viko chini yake kuamua juu ya muungano au ushirikiano wa Vyama vya siasa.Msajili anaendelea kuwa  ni mteule wa Rais na kwa hivyo kumpa mamlaka ya nyongeza yakiwa ni makubwa zaidi, ni sawa na kumpa Rais mamlaka juu ya Vyama vya Siasa - na chama chake Rais kikiwa ni mshindani wa vyama vyengine.


Kutokana na nia ovu kadhaa zilizo sokotwa ndani ya Muswada huu basi tunatoa wito kwa Wabunge, Vyama vya Siasa, Wananchi, Taasisi za Kidini, Azaki, Wasomi na Jumuia ya Kimataifa kuunganisha ushirikiano wao, kupaza sauti na kukusanya  nguvu zao pamoja ili kuupinga Muswada huu muovu kwa ustawi wa demokrasia ya Tanzania. 


John Mrema 

Mkurugenzi wa Uenezi, Mawasiliano and Mambo ya Nje 

Dar Es Salaam.

16 November, 2018


No comments:

Post a Comment