Friday, January 19, 2018

Mbunge wa Mbeya Joseph Mbilinyi 'Sugu', amenyimwa dhamana tena na amerudishwa rumande hadi 22 Jan 2018

Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Joseph Mbilinyi “Sugu’’ pamoja na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Emmanuel Masonga, wamerudishwa rumande hadi Jumatatu ijayo ambapo kesi yao ya kutoa matamshi ya uchochezi itaanza kusikilizwa mfululizo.

Wawili hao, walifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza Jumanne tarehe 16 Januari, 2018 katika Mahakama ya Mkoa wa Mbeya na mahakama iliwanyima dhamana na kuamuru wapelekwe rumande mpaka tarehe 19 Januari 2018(leo) ambapo pia wamenyimwa dhamana hadi Jumatatu.

Kesi hiyo ambayo watuhumiwa wanasimamiwa na Wakili msomi Boniface Mwabukusi ilifunguliwa kutokana na maneno waliyotoa katika hotuba zao walizotoa katika Mkutano wa Hadhara wa Mbunge huyo wa Mbeya Mjini uliofanyika tarehe 30 Disemba, 2017 katika kiwanja cha Shule ya msingi Mwenge iliyopo katika Kata ya Ruanda jijini Mbeya.

Mashtaka yao ni matumizi ya lugha ya fedheha dhidi ya Rais Magufuli ambaye amechaguliwa na Watanzania wakiwamo watu wa Mbeya

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Mbeya amesema sababu kumnyima dhamana mshtakiwa Sugu na mwenzake Emmanuel Masonga ni hofu ya mshtakiwa kutohudhuira mahakamani mara kwa mara.

Wakili wa Serikali aliiambia mahakama iwaweke ndani watuhumiwa kwa ajili ya usalama wao na walikuwa wakifuatiliwa na kuna viashiria vya usalama wao kuwa mdogo.

No comments:

Post a Comment