Tuesday, December 19, 2017

Taarifa kwa Umma - kuhusu uchaguzi wa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki.

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

Taarifa kwa Umma - kuhusu uchaguzi wa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki.

Leo tarehe 18 Novemba,2017 pamoja na mambo mengine ilitarajiwa kufanyika kwa uchaguzi wa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA)huko Arusha.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 8 ya Kanuni za Bunge hilo kuhusu uchaguzi wa Spika inasema kuwa Spika wa Bunge hilo atapatikana kwa njia ya mzunguko kutoka nchi moja baada ya nyingine, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo ni kuwa Tanzania, Kenya na Uganda walishakuwa na Spika wa Bunge katika Bunge hilo.

Awamu hii Spika alipaswa kutoka Rwanda, Lakini Tanzania kwa kuwa CCM imezoea kutokuheshimu Sheria na Kanuni zilizopo imemteua Mbunge wake Adam Kimbisa kugombea nafasi ya Spika kinyume kabisa na Kanuni za Bunge hilo na huu ukiwa ni mwendelezo wa utamaduni wao wa kutokuheshimu Sheria na Kanuni, kitendo ambacho kinatishia ustawi na uwepo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

CHADEMA tunalaani kitendo hiki, CCM wajue kuwa watabeba lawama zote kama kutakuwa na mgogoro ndani ya Bunge la Afrika Mashariki ambayo unaweza kupelekea mgogoro wa kidiplomasia katika Jumuiya nzima kutokana na tabia yao ya kutoheshimu taratibu zilizowekwa.

CHADEMA tunataka Kanuni za EAC ziheshimiwe, Kwani tunakumbuka Matendo ya Idd Amin mwaka 1977 yalivyovunja Jumuiya hii, hatutaki yajirudie kamwe.

Imetolewa Leo tarehe 18 Novemba, 2017.

John Mrema

Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje.

No comments:

Post a Comment