Sunday, October 1, 2017

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) TAARIFA KWA UMMA

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA UMMA

Leo tarehe 30 Septemba,2017 CCM wamehitimisha vikao vyao vya Chama walivyofanyia Ikulu ya Watanzania wote na tumezisikia kauli za Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM akitetea kitendo hicho na kusema ni halali na hawajakiuka sheria wala kanuni yoyote ile.
Aidha kupitia mkutano huo wake na waandishi wa habari leo, CCM imenukuliwa ikisema kuwa Mameya au Wenyeviti wa Halmashauri wao sio wenye halmashauri hizo bali wakurugenzi ndio wenye mamlaka na halmashauri hizo.

Kauli kama hizo zinaweza kutolewa na mtu mwenye upeo mdogo na asiyeelewa utaratibu wala Kanuni za Maadili zinazosimamia Vyama vya Siasa za Mwaka 2007 na Sheria zinazosimamia uendeshaji wa halmashauri za mwaka 1982.

Kuhusu kufanya vikao vya CCM Ikulu;

Kanuni Maadili ya Vyama vya Siasa za Mwaka 2007, sehemu ya tatu kifungu cha 5 (1)(i) kinasema kuwa chama chochote cha siasa kina wajibika "kuepuka kutumia mamlaka, rasilimali za serikali, vyombo vya dola au wadhifa wa kiserikali, kisiasa au ufadhili wa nje au wa ndani kwa namna yeyote ile ili kukandamiza chama kingine".

Hivyo basi kitendo cha CCM kutumia Ikulu kufanya vikao vyake ni kuvunja kifungu hiki cha kanuni za maadili ya vyama vya siasa na kinaenda kinyume kabisa na utaratibu wa kuendesha Ikulu katika nchi yenye mfumo wa vyama vingi.

Na kama CCM wataendeleza kupotosha kuwa wamefanyia vikao Ikulu kwa sababu ni makazi ya Rais, hii ni sawa na kusema kuwa ni haki kwa kila ambaye makazi yake yapo ndani ya eneo la kazi kama vile Mganga Mkuu wa Hospitali na wengine kufanya vikao vya ukoo au vya harusi ndani ya hospitali kwa kuwa ndipo makazi yake yalipo!

Aidha kama wamelipia ukumbi na gharama za vyakula kama walivyosema, tunataka sasa Ikulu iweke wazi utaratibu ambao CHADEMA inaweza kuufuata ili tuweze kupata ukumbi huo kwa ajili ya mojawapo ya vikao vyetu. Ingawa CHADEMA hatuamini kama Ikulu ya nchi yetu inaweza kuwa imefikishwa hatua ya kufanya biashara ya kukodisha kumbi za mikutano!

Halikadhalika tunaitaka CCM iweke hadharani vielelezo vya malipo ya ukumbi na yale ya chakula na vinywaji ili kuthibitisha kama kauli zao zina ukweli!

Kuhusu mameya na wenyeviti wa halmashauri;

Kusema kuwa Halmashauri ni mali ya wakurugenzi, ni mojawapo ya kauli ajabu kuwahi kutolewa katika karne hii kwani kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, ibara ya 145 na 146 iliyounda halmashauri hizi iko wazi kabisa kuwa hivi ni vyombo vya wananchi na vitaendeshwa na wananchi ama moja kwa moja au kwa uwakilishi. Sasa Mkurugenzi anamwakilisha nani? Au Pole pole hajui maana ya uwakilishi?

Mameya ni madiwani wa kuchaguliwa na wananchi na ndio wanakidhi sifa ya kuwa wawakilishi wa wananchi wanaopaswa kuendesha na kusimamia halmashauri kwa niaba ya wananchi.

Pili, sheria iliyounda Mamlaka za Serikali za Mtaa ya Mwaka 1982 inatambua kuwa halmashauri zipo chini ya Baraza la Madiwani na ndio wasimamizi wakuu na wenye maamuzi kwa niaba ya wananchi katika uendeshaji wa halmashauri zao.

Mkurugenzi ni mwajiriwa wa Baraza la Madiwani na Meya au Mwenyekiti wa Halmashauri ni mkubwa wake wa kazi (bosi) kwa mujibu wa sheria hii. Pole pole hajui uwepo wa sheria hii?

Aidha kwa tafsiri ya Polepole ni haki kusema kuwa Bunge lipo Chini ya Katibu wa Bunge na sio Spika! Au ni Sawa kusema kuwa Ikulu ipo chini ya Katibu Mkuu Kiongozi na sio Rais! Jambo ambalo sio kweli hata kidogo.

Tunawataka CCM watambue kuwa wao ni chama cha siasa kama vilivyo vingine. Hawako juu ya taratibu za uendeshaji wa nchi, ikiwemo Katiba na Sheria. Wanawajibika kutii Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa za Mwaka 2007 .

John Mrema
Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje- CHADEMA.

Imetolewa leo Jumamosi, tarehe 30 Septemba 2017.



No comments:

Post a Comment