Wednesday, September 13, 2017

Pole Lissu, Mungu atakuponya, Pole Lissu.

Leo nimemsikiliza Katibu mkuu wa Chadema Dr Vicent Mashinji akielezea hali ya Tundu Lissu,nimestuka sana kwamba mguu na mkono wa kushoto pamoja na nyonga zimevunjwa,mara ya kwanza nilipopata taarifa za Lissu Kupigwa Risasi,nilichagua kukaa kimya nisiseme wala kuandika kitu,niwasikilize zaidi wengine.

Baadae nilianza kuona picha na taarifa mbalimbali za jinsi Lissu alivyojeruhiwa,niliumia sana kuona binadamu mwenzangu alivyoumizwa,sikuwa na taarifa sahihi jinsi Lisu alivyoumizwa.

Kesho yake nikamuona Spika akitoa taarifa bungeni na kuueleza umma kuwa Lisu alimiminiwa Risasi 32,nilistuka sana,kwa nini Risasi 32 zimiminwe kwa mwanadamu?mtu ambaye si jambazi?inakuwaje Risasi zaidi ya 30 zimiminwe kwa Mwanasiasa na mwanasheria?.

Nilibaki natetemeka,nikikuomba Mungu anipe moyo wa kujifunza kwa wengine na nijue hasa kwa nini mwanasiasa na mwanasheria amiminiwe Risasi zaidi ya 30?kakosa nini?

Kwa nini najiuliza maswali mengi mpaka sasa na kubaki njia panda?

Binafsi nilimfahamu Lissu kabla hajaingia bungeni mara ya kwanza kukutana nae ilikuwa mwaka 2006,wakati huo Lissu alikuwa mpambanaji mkubwa na makampuni makubwa ya uwekezaji kwenye sekta ya madini nchini Tanzania!.

Nilikutana nae wakati huo nikiwa nimejikita zaidi kwenye uandishi wa habari za madini,tulijikuta wote tupo kwenye eneo moja,yeye akifanya kama mwanasheria na mimi nikifanya kama mwandishi wa habari.

Lissu aliniambia amekuwa na mapambano makubwa na kampuni la Barrick,alikuwa akipaza sauti kweli kweli kuhusu wizi unaofanywa na wawekezaji hawa,Lissu alikuwa ni miongoni mwa wanaharakati kutoka chama cha wanasheria wa mazingira waliopaza sauti kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu tuhuma dhidi ya mgodi wa Bulyanhulu kuwa uliwafukia baadhi ya wachimbaji wadogo,kama sijakosea ilikuwa mwaka 1999.

Lissu aliniambia mapambano yake na Barrick yalimsababishia aishi maisha magumu yaliyojaa hofu,Serikali ilimpinga na kusema Lissu alikuwa anasema uongo na kuwagombanisha wawekezaji na wananchi.

Lisu akaniambi alilazimika kufanya mkutano na waandishi wa habari kuelezea tuhuma dhidi ya Barrick,mkutano ule aliufanya muda mfupi kabla hajaondoka kwenda masomoni Nchini Marekani,mkutano ule ulimsababishia ugomvi mkubwa na Serikali ya Awamu ya tatu,aliitwa majina mengi,kubwa lilikuwa mchochezi.

Lissu alipotoka kwenye masomo yake ya shahada ya pili,aliendelea na harakati zake za kupambana na wawekezaji kwenye sekta ya madini.

Lissu aliporudi alikuta kundi kubwa la wananchi wanaoshi pembezoni mwa migodi wakiwa kwenye vifungo baada ya kukutwa na makosa ya uvamizi kwenye migodi,Lissu aliamua kuanza mchakato wa kuwatetea na hata kukata rufaa kwa watu waliokuwa wamewekwa ndani kwa makosa ya kuvamia migodi,makumi kwa mamia ya watu walitetewa bure na kutoka jela kwa utetezi wa Lissu bila malipo,Lisu alipataza sauti kuwa uwekezaji umegeuka kuwa unyama nchini Tanzania.

Harakati zake zilimsababishia ugomvi na serikali pamoja na wawekezaji,mwaka 2011,Baadhi ya wakazi wa Nyamongo waliingia kwenye mgodi kusaka mabaki,wakapogwa Risasi na Polisi na watu wawili nakumbuka walifariki dunia.

Lissu akiwa kwanza ndiyo ameingia bungeni,alikwenda Nyamongo,aliitisha mikutano,familia na wanajamii ya nyamongo,ziligoma kuzika maiti zilizopigwa Risasi.

Lissu akiwa Nyamongo alikamatwa na kuwekwa ndani kwa makosa ya kuwachochea wananchi wawachukie wawekezaji,Lissu aliwekwa ndani akafikishwa mahakamani na baadae kuamriwa asikanyage Nyamongo kwani amekuwa anachochea chuki wananchi wa Tarime wawachukie Barrick,sidhani kama katazo hilo lilifutwa.

Mwaka 2006,jumuiya ya viongozi wa dini nchini hapa ni viongozi wa dini zote na madhehebu yote,nakumbuka mara mbili nilifuatana nao,kwa kushirikiana na Lissu ilizunguka migodi yote nchini kuwatetea wananchi waliokuwa wananyanyaswa na wawekezaji.

Nakumbuka kwenye tema hiyo alikuwemo Shehe Fereji,Askofu Munga,Askofu Mkuu Ruzoka na viongozi wengi,hawa walipaza sauti kuiambia serikai kuhusu wizi na unyama unaofanyika kwenye sekta ya madini nchini.

Mpaka leo nalikumbuka chozi la Aksofu Munga na Shehe Fereji walipofika kwenye mgodi wa RUSU huko Nzega mkoani Tabora baada ya kukuta wananchi wakiteseka na kuishi maisha ya simanzi na umasikini wa kutopea,kwa kila aliyepaza sauti aliitwa mchochezi ana wivu wa maendeleo.

Viongozi wa dini hawa walitafuta wataalam kutoka ndani na nje ili wafanye utafiti wa kisayansi kuhusu mchango wa sekta ya madini nchini.

Walikuwa ni Curtus na Tundu Lissu ndiyo waliozunguka migodi yote nchini na kutoka na ripoti ya kina kuhusu hali ya uwekezaji kwenye sekta ya madini.

Lissu na Curtus walikusanya ushahidi kutoka mgodini,serikalini na kwa wananchi wa kawaida,wakatoka na ripoti iliyoitwa 
"THE GOLDEN OPPORTUNITY",ripoti hii waweza ipata mtandaoni,iliandikwa na Lisu huyu ambaye muda huu anateseka kitandani huko Nairobi.

Mwaka 2009,wakati huo nikifanya uchunguzi kuhusu ukweli wa sumu za mti Tigite huko Nyamongo,na hii ni baada ya baadhi ya wakazi wa Nyamongo kubabuka na wengine walipoteza maisha kutokana na kilie kilichodaiwa kuwa ni Sumu,nilipokuwa Nyamongo,kila familia niliyoitembelea,walikuwa wananiambia niwasaidie kumwambie Lissu aende kwani wanakufa na Sumu.

Watu wale walimuona Lisu ndiyo kimbilio lao,mwaka Huo huo,ili kuionesha ushahidi serikali kuwa mgodinwa Barrick umetiririsha sumu kwenye vyanzo vya maji huko Nyamongo,Lisu huyu anayeteseka huko Nairobi muda huu na chama cha wanasheria za mazingira walilazimika kuwasafirisha kwa ndege waathirika wa sumu za mto Tigite.

Lissu alimsafirisha mzee Mwikwabe ambaye mwili wake ulikuwa umebabuka na sumu za mto Tigite,ilikuwa ni usiku kupitia Channel Tena,Lissu akiwa na Mzee Mwikwabe,walijitikeza kwenye mjadala na Lissu akawa anaongea kwa ukali akiiambia Serikali,"Mnataka niwape ushahidi upi ili muamini kuwa huko Nyamongo kuna watu wanakufa kwa sumu zinazotiririshwa na mgodi"

Lisu hakusikilizwa,Mgodi ulikana,Serikali
ilikana,bunge liliunda kamati ,kama sikosei spika wa sasa wakati huo akiwa mwenyekiti wa kamati walikwenda Nyamongo ba baadae wakasema hakuna ushahidi kuwa zile ni sumu.

Nakumbuka siku kamati ilipokuwa Nyamongo,mimi na team yangu tulikuwa Nyamnongo,katika kijiji cha Kewanja,wananchi waliwaambia wabunge wa kamati ya mazingira kuwa kama wanadhani maji hayana sumu wanaguse ama kunywa,hakuna mbunge aliyegusa.

Ni Lissu na baadhi ya waandishi wa habari akiwemo Christopher Gamaina wakati huo akiwa na Gazeti la Mtanzania ndiyo waliosema kuna watu wameungua kwa sumu.

Lissu alisimama na kusema bila hofu kuwa wawekezaji hawa wanaliibia taifa,wanaua watu kwa bunduki na sumu zinazitirirka kwenye vyanzo vya maji,lakini akaitwa mwanaharakati anayetaka wagombanisha wawekezaji na wananchi.

Nakumbuka wakati tunachunguza ukweli wa sumu kwenye mto Tigite,moja ya nyaraka tulizotumia ni Ripoti za Lissu,nakumbuka kwenye makala za uchunguzi huko Geita,tulitumia mapendekezo ya ripoti Lisu na Curtus kuitaka serikali ifanye
mabadiliko ya kisera na kisheria ili watanzania wanufaike na madini,Ripoti ya Lisu ndiyo ilikuwa mwongozo wa nini tufanye?

Najiuliza,mbona Lissu amekuwa mpambanaji wa mali za umma,tangu ubarubaru wake leo anatesema kiasi hiki na hata kudhihakiwa na baadhi ya watu wakati huu akitesema huko Nairobi?

Muda,Ujasiri,kujitoa kwake kupambana na wawekezaji wa Lissu hautoshu wote tunuombee badala ya wengine kumdhihaki?,ni kweli kazi na upambanaji wa Lissu haujulikani?

Pole Lissu,Mungu anajua kazi za akili na mikono yako,naamini utapona Lissu,nayaona maumivu uliyonayo muda huu hapo hospitali,Naamini Utapona,naaamini Mungu anayaona maumivu na machozi.

No comments:

Post a Comment