Wednesday, September 13, 2017

MH. TUNDU ANTIPASS MUGWAI LISSU NI MZALENDO AU MCHOCHEZI?

Kwa muda mrefu mjadala mkubwa usio rasmi umetamalaki nchini iwapo Mh. Lissu ni mzalendo au mchochezi. Nikaona nijaribu kufuatilia maisha yake ili kuona kama naweza kutengua kitendawili hiki.
Lissu alizaliwa tarehe 20 Januari 1968 na alisoma shule ya msingi Mahambe, Singida. Katika miaka yake yote saba shuleni hapo, Lissu hakukubali hata mara moja kuamka alfajiri saa 11 kuwahi namba na daima aligomea kulima mashamba ya walimu, kuwachotea maji na kazi za namna hiyo kwani kwake aliona haziko sahihi. Hii ilipelekea awe anatandikwa bakora mara kwa mara. Shuleni hapo, bakora na mwili wa Lissu vilikuwa ni kama uji na mgonjwa. Hata hivyo, kilichomsaidia ni akili yake. He was a very, very brilliant pupil.

Lissu alifaulu mtihani wa darasa la saba na kwenda shule ya sekondari ya Ilboru, Arusha. Shuleni hapo, yeye ndie aliyekuwa mwanafunzi mdogo kuliko wote. Licha ya udogo wake, alikuwa mwiba mkali kwa prefects na walimu. Akiwa kidatu cha tatu wenzake walimtaka awe prefect lakini alikataa kwani alizoea kuwaita "manyoka" kwa tabia yao ya kupenda kupeleka taarifa za wanafunzi kwa walimu.

Lissu alifaulu vizuri na kuingia kidato cha tano shule ya sekondari ya Galanosi, Tanga. Akiwa Galanosi, akapewa Uenyekiti wa Kamati ya Taaluma. Hata hivyo, akakorofishana vibaya mno na mwalimu wa taaluma na kuvuliwa cheo hicho.

Akiwa kidato cha sita mwaka 1988, kulikuwa na disko la graduation. Kidato cha sita wakaruhusiwa kwenda kucheza na Korogwe girls lakini kidato cha nne wakakataliwa na wakaambiwa wataletewa taarabu shuleni hapo. Lissu aliona huo ni uonevu na daima shuleni hapo alichukia mno mwanafunzi mwenzake kuonewa hata kama ni wa madarasa ya chini. Hivyo, akaandika Waraka "TAARAB FOR WHOSE INTEREST". Lissu hakuandika jina lake kwenye Waraka huo. Akaubandika kwenye ubao wa matangazo usiku. Walimu walipouona walichukia sana na wakachunguza na kuhisi mwanafunzi pekee aliyepinda shuleni hapo mwenye ubavu wa kuandika vitu kama vile ni Lissu tu hivyo wakamkamata. Walimu wakamwita Lissu mchochezi na hivyo akapewa suspension. Hata hivyo, baadae akarudishwa shuleni na kisha akafanya mtihani wa kidato cha sita.

Mwaka 1989 akaenda Mafinga JKT kisha Itende JKT kwa mwaka mmoja. Wakati huo, vuguvugu la vyama vingi lilikua limepamba moto nchini huku CCM ikiwa haitaki kabisa kuskia mambo ya vyama vingi. Katiba ya CCM ilikuwa inautambua Mkoa wa Majeshi hivyo ilituma viongozi wake kutembelea kambi zote na kuulezea msimamo wa CCM kutotaka kuskia takataka inayoitwa vyama vingi.

RPC Omary Mahita (Rukwa) na Kanali wa Andrew Shija wakitokea Mkoa huo wa Majeshi wakapangiwa kwenda Itende JKT kuwaelezea servicemen msimamo wa chama. Walipofika wakaitisha mkutano mkubwa na ukumbi ukawa umefurika. Katika mkutano huo, Mahita na Shija wakaeleza kwamba "Sisi haya mambo ya vyama vingi hayatuhusu. Haya ni mambo ya wazungu huko Ulaya mashariki hivyo tusiyashabikie".

Kitu ambacho viongozi hao hawakukijua ni kwamba miongoni mwa servicemen hao alikuwepo kijana mmoja very brilliant mwenye uelewa mkubwa wa mambo mengi yanayoendelea duniani asiye na simile kuongea kilichomo akilini mwake.

Lissu alikuwa ameskiliza hotuba ya Baba wa Taifa alipoongea na Baraza Kuu la Umoja wa vijana wa CCM Mwanza wiki chache kabla ya mkutano huo wa akina RPC Mahita. Mwalimu alikuwa amesema -"Wanaodhani mageuzi hayatuhusu bali yanazihusu nchi za Ulaya mashariki pekee ni wajinga kwani Tanzania sio kisiwa".

Muda wa maswali ulipofika huku wengi wakiamini hakuna atakaekuwa na ubavu wa kuuliza swali, Lissu bila kuogopa na kwa ujasili wa hali ya juu ambao haukuwahi kuonekana hapo Itende JKT, akanyoosha mkono. Servicemen wenzake waliokuwa wakijua misimamo yake isiyoyumba walijitahidi kumshusha mkono bila mafanikio. Huku akitumia lugha kali bila kumun'gunya maneno kama kawaida yake, Lissu aliwauliza viongozi hao -"Je, mjinga ni Baba wa Taifa aliyesema mageuzi ya vyama vingi yanatuhusu au ni nyie mnaosema hayatuhusu?"

RPC Mahita, kwa wajihi, ni mweupe sana lakini swali hilo lilimbadilisha na kuwa mwekunduuuu. Ghafla bin vuu maafande wakamkimbilia Lissu kutaka kumkwida kwa "kosa" la kutukana meza kuu. Bahati nzuri, Kanali Shija akawa na busara na akawazuia na kuwaambia "Huyo kijana Lissu yupo sahihi kwani hicho ndicho alichosema Baba wa Taifa." Huo ndio ukawa mwisho wa mkutano.

Baada ya songombingo na tafrani hiyo ya kipekee siku hiyo , maafande wote wa Itende JKT wakaanza kumuogopa sana Lissu wakiamini yeye ni mtu wa Usalama wa Taifa na akawa hapangiwi tena kazi bali akawa anakula shushi hadi kumaliza muda wake!

Kutokana na kufaulu vizuri kidato cha sita, Lissu alijiunga na kitivo cha sheria mwaka 1991 UDSM. Huko aliendelea na harakati zake za kupigania haki za wanafunzi na akajiunga na NCCR MAGEUZI. Miaka hiyo, chama hicho kilichokuwa chini ya mmoja ya viongozi waliowahi pendwa mno nchini, Mh. Augustin Mrema, ndicho kilikuwa chama kikuu cha upinzani nchini.

Baadae mwaka 1995, Lissu akaenda kusomea shahada ya uzamili chuo cha Warwick UK. Alipofika huko akaomba ruhusa aje kugombea ubunge Singida mashariki. Hata hivyo, kutokana na maandalizi duni, kura hazikutosha hivyo akarejea masomoni.

Lissu alipomaliza masomo yake 1997 alirejea na kufanya kazi ya sheria Arusha. Baadae akaoa na kuhamia Dar Es Salaam. Akawa mmoja wa wanasheria wa chama cha wanasheria wa mazingira (LEAT) pamoja na Dr. Rugemeleza Nshalla na Alex Shauri. Lissu akaanza kujipambanua kama mtanzania anaepigania haki za wanyonge na maliasili za nchi yake bila woga wowote.

Ujasiri wake mkubwa wa kwanza kupigania maliasili za taifa lake ulikuwa mwishoni mwa miaka ya 90. Serikali ya awamu ya tatu ilikuwa imempa raia wa Ireland aitwae Reginald Nolan hekta 20, 000 kuchimba mabwawa ya kambakoche kwenye delta ya Rufiji katika maeneo ya watu yenye vijiji nane waliokuwa wakiishi na wakilima humo. Lissu aliwahurumia sana wananchi hao wanyonge. Hivyo, aliratibu kampeni iliyoendeshwa na LEAT kimataifa kuupinga mradi huo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kimataifa. Hii ilikuwa ni kazi ngumu mno na yenye vitisho vingi. Ilikuwa si ajabu asubuhi kukuta chini ya mlango wa ofisi ya LEAT Mavuno house barua ya vitisho. Lissu hakujali wala kuogopa.

Kutokana na juhudi kubwa ya Lissu, hatimaye "European Investment bank", iliyokuwa tayari kutoa mkopo kwa Nolan ambao ungedhaminiwa na serikali ya awamu ya tatu, ikakubaliana na hoja kuntu za Lissu na kugoma kutoa fedha hizo. Hivyo, mradi huo ukasambaratika. Huu ulikuwa ushindi mkubwa kwa Lissu na alipongezwa mno na wanavijiji hao wanyonge waliomuona kama Mungu.

Lissu akapata umaarufu na kualikwa kwenye kipindi cha "Hamza Kasongo hour" Octoba 1998 na mzalendo mmoja akawa amempa nyaraka za Baraza la Mawaziri ambazo zilisema mradi huo ni wa hovyo na ulipitishwa kinyemela!

Mwezi Septemba 2000 alikwenda USA kama mtafiti kwa miaka mitatu kwenye kampuni ya World Resource Institute huku akirudi mara kwa mara nchini kuendelea na kazi za LEAT.
Mwaka 2001 yeye na wenzake wa LEAT walifanya Press conference maelezo na kudai wana ushahidi wa video kuhusu mauaji ya Bulyankulu. Yeye akarudi US lakini wenzake wakakamatwa. Akaskia imeelezwa ametoroka na atafutwa na Interpol. Akarudi na akakamatwa. Akasachiwa nyumbani kwake na kupelekwa Central. Akafanya ujanja na kuingia na simu na usiku kucha akawa anawasiliana na magazeti ya US na Canada. Hiyo ikamsaidia kuondokana na msala huo.

Je Lissu aliingiaje CHADEMA?

Lissu alijiunga CHADEMA kimazabe mwaka 2004. Mwaka 2003, Lissu alikwenda Tarime kwenye masuala ya madini. Akakutana na Mh. Chacha Wangwe akiwa Diwani wa Tarime akiwa na kesi kumi za jinai. Mh. Wangwe akamwambia Lissu kuwa wanataka kumfunga. Lissu akamwambia aondoe hofu hawataweza.

Mh. Mbowe akampigia simu Mh. Lissu kumuomba amtetee Mh. Wangwe kwenye hizo kesi zilizokuwa zikifunguliwa kila uchao. Lissu akakubali na akafanya kazi yake kwa weledi wa hali ya juu. Mh. Lissu akasaidia pia kushinda kesi za wananchi wanyonge 366 katika kipindi cha miezi minne tu. Hawa ni wananchi waliokuwa wakiishi pembezoni mwa migodi kabla ya kuswekwa ndani kwa kosa la kuvamia migodi hiyo. Lissu aliwatetea bure wananchi hawa mafukara na baada ya ushindi wa kesi hizo akatamka-"Uwekezaji umegeuka kuwa unyama Tanzania". Lissu akaonekana ni mtu asiye na uzalendo na taifa lake kwa kuwasema vibaya wawekezaji ambao serikali ilikuwaikidai walikuwa wakiliingizia taifa mapato makubwa. Hata hivyo, kwa wananchi hao wanyonge, Lissu alionekana ni Mfalme.

Baadae Mh. Mbowe akampigia Lissu na kumuomba asaidie kutafuta wanasheria wengine waingie CHADEMA kama yeye. Lissu akamshangaza Mh. Mbowe kwani bila kupepesa macho wala kutikisa maskio, Lissu akasema yeye ni mwanachama wa NCCR MAGEUZI! Mh. Mbowe alistaajabu sana kwani aliamini Lissu ni mwanachama wa CHADEMA. Hivyo, Lissu akamwambia Mh. Mbowe "kama unataka nijiunge nanyi basi najiunga" ndivyo Lissu alivyojiunga CHADEMA.

Lissu aliendelea na jitihada zake kuwasaidia wananchi waliokuwa wakinyanyasika migodini huku akiacha wateja wenye fedha nyingi Dar Es Salaam. Kwa Lissu, hakuna kitu kinamuuma moyoni mwake kama akiona mnyonge ana haki lakini anaonewa. Lissu kamwe hawezi kukaa kimya kuona hali hiyo ikiendelea.

Jitihada hizi zikamfanya Lissu azidi kukorofishana na serikali mara kwa mara. Serikali ikamwita ni mchochezi anaechochea wananchi kuwachukia wawekezaji wa Barrick ambao serikali ilikuwa ikidai ni wawekezaji wazuri waliokuwa wakiliingizia taifa pato kubwa.

Lissu amekuwa mstari wa mbele kwenye harakati za kutetea sekta ya madini nchini. Kwa miongo zaidi ya miwili amekuwa akipambana na wawekezaji wazungu waliokuwa wakikingiwa kifua na serikali ya awamu ya tatu na ya nne na kuonekana yeye si mzalendo. Alikuwa ni mmoja wa waliopinga hadharani na kwenye maandiko yake, sheria ya madini ya mwaka 1998 na ya 2010 kwa hoja kwamba zinawatajirisha wawekezaji wazungu na kutuachia watanzania mashimo tu na umaskini mkubwa wakati Mungu aliibariki nchi hii kwa kuipa madini mengi. Hoja hizi zilikuwa zikikejeriwa na wabunge wa CCM ambao walikuwa wakiipitisha miswada hii kutokana na wingi wao bungeni. Aidha, Lissu alipinga vikali kupitishwa na bunge sheria zote za madini kwa hati ya dharura mwaka 2015 na 2017.

Licha ya jitihada hizi kubwa za kuwapigania wananchi wanyonge na maskini huku wengi akiwatetea mahakamani bure na kupambana vikali na wawekezaji wa makampuni ya madini ambayo yeye miaka yote amekuwa akiyaita ni ya wezi wanaotuibia madini yetu na kunyanyasa wananchi migodini, Lissu anaonekana kwenye macho ya baadhi ya watu kwamba si mzalendo bali ni "kibaraka anaetumiwa na wazungu asieitakia mema nchi yetu".

Je Mh. TUNDU ANTIPASS MUGWAI LISSU ni mzalendo au Mchochezi? The ball is in your court!

Naomba nimalizie makala yangu kwa nukuu hizi kuntu toka kwa viongozi wetu watatu wapendwa:

1."Mtu mwenye weledi huwezi tu ukakubali kila unachoambiwa. Unatakiwa kuwa kama Mbayuwayu. Akili zako unachanganya na za kuambiwa kisha unapata jibu".

MH. JAKAYA KIKWETE

2."Watanzania tumeibiwa sana haya madini yetu. Tumechezewa kiasi cha kutosha lazma tufike mahali tuseme imetosha. Sijui watanzania tumerogwa na nani? Basi tuwaombe mapadri, wachungaji na mashehe watuombee ili mapepo yatutoke. Kwa maamuzi haya mabovu ipo siku vizazi vyetu vitakuja kuyatafuta makaburi yetu na kuyapiga mawe".

MH. DR. J. MAGUFULI

12.6.2017

"Mzalendo wa kweli wa Taifa hili ni yule aliyeivishwa vizuri na TANU au ASP aliyetayari kujitoa muhanga kulipigania taifa lake kwa akili na nguvu zake zote bila woga kupambana na mabeberu na manyan'gau yasiolitakia mema taifa letu iwe kwenye mapambano ya kiuchumi au ya kulinda kulinda mipaka ya nchi yetu".

JK NYERERE, BABA WA TAIFA, 1.3. 1971


No comments:

Post a Comment