Wednesday, September 6, 2017

KAULI YA MHESHIMIWA FREEMAN KUHUSU RIPOTI YA KAMATI ZA MADINI

Bunge letu likiamua kufanya kazi kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu linayo nafasi kubwa sana ya kuisaidia Serikali, kwa kuunda Kamati hizi Mhe. Spika ameisaidia Serikali.

Naimani kabisa Mhe. Spika na timu yake wanatambua Bunge limejaa watu wenye uwezo mkubwa, experiences tofauti, ambao wakitumika kikamilifu wanaweza wakawa msaada mkubwa sana kwa Taifa, wanaweza kuwa msaada mkubwa sana kwa utekelezaji wa kazi za Serikali.

Kamati hizi zimetambua mambo mengi mazito, na kweli kihistoria kwa wale ambao tumekuwa ndani ya Bunge kwa miaka mingi, pale kamati teule za Bunge zinapotumwa majukumu mahsusi huleta ripoti zilizosheheni ukweli ambazo kwa bahati mbaya pengine hazitekelezwi sana kwa yale maazimio ambayo yanatokana na ripoti hizo.

Natambua busara ya Mhe. Spika iliyompeleka mpaka aone ripoti hizi kwa unyeti wake zisisomwe tu ndani ya Bunge, lakini hata watu wengine ambao ni watendaji wakuu, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama navyo viweze kushiriki kupokea ripoti hizi.

Kwa busara hizo hizo ili ripoti hizi ziweze kupata uzito wa Kibunge, tuzijadili ndani ya Bunge ili Wabunge sasa watoke na maazimio rasmi ambayo yatakuwa ni maelekezo ya Bunge kwa Serikali.

Na Waziri Mkuu namuomba kama Kiongozi Mkuu wa Serikali ndani ya Bunge apokee ripoti hizi kwa kutambua tu kwamba Bunge linajaribu kuisaidia Serikali katika kutekeleza majukumu yake ipasavyo na Bunge linafanya wajibu wake na sio suala la chuki.

Nia njema ya Serikali isipotekelezwa kwa misingi ya haki inaweza ikapoteza ndoto ya faida kwa Taifa na ikawa hasara.

Kwa sababu wengi wametajwa katika ripoti hizi haki ikatendeke kwa wote, vyombo vyote vya umma vitakavyofanya kazi ya kusimamia jambo hili au maazimio yatakayokuwa ya Bunge au maelekezo yoyote ya Kibunge au Serikali, tunaomba vikafanye kazi hii kwa haki kila mmoja apate haki inayomstahili, asionewe mtu lakini haki isiende kupindwa katika kuwakabili wahusika na changamoto zinazowahusu.

Pale ambapo kuna na ushirikiano wa kutosha kati ya Bunge na Serikali faida kwa Taifa inaonekana, Mhe. Spika alipounda Kamati teule alichanganya Wabunge kutoka vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, unaona jinsi wabunge hao wamefanya kazi kwa pamoja sio kwa misingi ya kiitikadi, wamefanya kazi kama viongozi, wamefanya kazi kama wawakilishi wa Wananchi , wamefanya kazi kama Watanzania na ripoti yao ni ya Watanzania.

Tunaomba ushirikiano huo usiishie kwenye Kamati teule tu, ushirikiano wa Wabunge wa pande zote mbili, Wabunge wa Chama kinachotawala na Kambi ya Upinzani ukajidhihiri ndani ya Bunge, nje ya Bunge katika wajibu wetu wa kulitumikia Taifa kwani sote ni Watanzania, nyumba tunayoijenga ni moja.

No comments:

Post a Comment