Friday, March 10, 2017

Katibu Mkuu Dkt. Mashinji alitaka bunge ‘kusimama’ bajeti ijayo kunusuru nchi



Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Vincent Mashinji ameonya kuwa iwapo katika mkutano ujao wa bajeti, Bunge halitasimama imara kuiwajibisha Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, kupitia kamati na hatimaye bunge zima, nchi inaelekea kuwa katika wakati mgumu zaidi.

Dkt. Mashiji amesema kuwa tayari hali hiyo ngumu imeanza kujidhihirisha kupitia katika bajeti ya sasa, ambapo wakati inakaribia kumalizika, kiuhalisia, kutokana na uchambuzi ambao umefanyika, ukihusisha CHADEMA kutuma watu kufuatilia, hadi sasa utekelezaji wake haujafikia asilimia 40.

Amesema kuwa utekelezaji wa bajeti unasuasua, hivyo kuthibitisha kauli iliyotolewa na Kambi ya Upinzani Bungeni mwaka jana kuwa Serikali ilipeleka bajeti hewa bungeni, akitolea mfano wa ahadi ya mil. 50 kwa kila kijiji, huku pia akihoji zaidi kuhusu mpango wa kutenga asilimia 40 ya mapato ya ndani kugharamia miradi ya maendeleo ambao nao haujatekelezwa hadi sasa bajeti ikiwa imefika robo ya nne tangu ilipopitishwa.

Akitoa kauli ya Chama mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, kuhusu bajeti ya 2016/2017 na mwelekeo wa bajeti ijayo, Dkt. Mashinji amesema muda wa kuanza kwa vikao vya kamati za bunge kwa ajili ya Mkutano wa Bunge la Bajeti ujao, ambao ulipangwa uwe wiki tatu umepunguzwa hadi kuwa wiki mbili, akisema kuwa hiyo ni mbinu ya Serikali kukwepa uwajibikaji mbele ya chombo hicho kwa sababu haina majibu kuhusu kutotekelezeka kwa bajeti ya sasa, ambako kunatoa taswira ya mwelekeo wa bajeti ijayo..

“Hii maana yake Serikali haitaki kusimamiwa kikamilifu. Inayumbisha mhimili huu kwa makusudi. Nawasihi wabunge wote wasikubali hali hii. Wahakikishe bunge linasimama kama mhimili na kutimiza majukumu yake kuisimamia na kuiwajibisha serikali kwa mujibu wa Katiba ya Nchi.

Dkt. Mashinji amesema kuwa mhimili wa Serikali kupitia kwa Rais umekuwa hauthamini bajeti iliyopitishwa na bunge, hilo limethibitika katika maeneo kadhaa, akitolea mfano wa mpango wa serikali kuhamia Dodoma ambao unatekelezwa bila kupangiwa bajeti wala sheria yake haijakamilika.

“Hata ujenzi wa kiwanja cha ndege Chato zilikuwa zimetengwa bilioni 2 pekee kwa ajili ya upembuzi yakinifu tu, lakini cha kushangaza ujenzi unaendelea kuelekea kukamilikas…majuzi pia tumeona akichezewa hadi ngoma watu wanashangilia baada ya kuelekeza bilioni 10 kwenye ujenzi wa mabweni, nje ya kasma za kibajeti. Si sahihi. Ni kudharau mhimili wa bunge ambao ndiyo wajibu wake.”

Akizungumza kwa kina kuhusu mwelekeo wa bajeti ijayo, Dkt. Mashinji amesema kuwa CHADEMA imefanya uchambuzi katika wizara moja tu ya Mambo ya Ndani ya Nchi, na kubaini kuwa bajeti ya 2017-2018, haitoi matumaini kwa Watanzania ambao tayari wako kwenye hali ngumu ya maisha kutokana na bajeti ambayo haikuwagusa katika uhalisia wa maisha yao, akisisitiza wabunge wana wajibu mkubwa kusimama imara kuiwajibisha Serikali ili kunusuru taifa na watu wake.

“Jeshi la Zimamoto na Uokojai wametengewa fedha za maendeleo shilingi bilioni 1.5 ambazo zinatosha kununua magari 2 tu ya zimamoto, fedha za uendeshaji wametengewa bilioni 3 pekee. Tujiandae majanga ya moto yakitokea hawana uwezo wa kununulia dawa za kuzimia moto.

“Huko magereza pia hali ni hiyo hiyo, sare za askari waliomba bilioni 4 wametengewa milioni 25 tu, vifaa vya wafungwa waliomba bilioni 1.692 wametengewa milioni 50 tu, sare za wafungwa waliomba bilioni 1.980 wametengewa milioni 20. Chakula cha wafungwa ziliombwa bilioni 48.223 zimetengwa bilioni 18.

“Si hivyo tu, madeni ya watumishi wanadai bilioni 50, pamoja na deni hilo kuhakikiwa zimetengwa shilingi 0, posho zao kwenye maduka yaliyofutwa kwenye bajeti iliyopita kuwa wataongezwa askari iliombwa bilioni 19 lakini zimetengwa shilingi 0; gharama za kuhamia Dodoma waliomba bilioni 1.2 zimetengwa shilingi 0. Hali hi hivyo hivyo kwa polisi na uhamiaji.”

Katibu Mkuu Mashinji amesema kuwa iwapo hali hiyo itaachiwa na hususan mhimili wa Bunge ukikubali kuwa chombo cha kutumiwa na serikali, kuna hatari kuwa serikali itashindwa kuendesha nchi inavyotakiwa na Watanzania watazidi kuwa katika wakati mgumu zaidi kuliko ilivyo sasa.

Dkt. Mashinji amewataka wabunge kujiandaa kikamilifu kuyapitia kwa kina mapendekezo ya bajeti ya serikali ambayo amesema kuwa yamejaa mapungufu na wasipokuwa makini, kwa mara nyingine tena, watapitisha bajeti isiyotekelezeka.

Amesisitiza kuwa mbali ya kudhibiti wa deni ya taifa lisiendelee kukuwa kwa kasi kama inavyoonekana sasa, pia amewataka wasimamie kikamilifu kuhakikisha kuwa utawala wa kidemokrasia unaheshimiwa na mtu yeyote asiruhusiwe kuvunja katiba na kupuuza sheria za nchi, kwa sababu mbali ya kuumiza wananchi wanyonge, athari zake zimekwenda mbali hata kuathiri mzunguko wa bajeti ambapo wapo wafadhili na washirika wa maendeleo wanajitoa kusaidia bajeti ya taifa kwa sababu ya kuvunjwa kwa misingi ya utawala bora.

No comments:

Post a Comment