TUNDU Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameachiwa baada ya kukamatwa na kuhojiwa Jeshi la Polisi katika Kituo Kikuu cha Kanda Maalum ya Dar es Salaam, anaandika Faki Sosi.
Mapema leo asubuhi Lissu alikamatwa na kupelekwa kituoni hapo ambapo ilielezwa kuwa alichukuliwa kwa lengo la kuhojiwa kuhusiana na mkutano aliofanya na waandishi wa habari kuhusu wa kupotea kwa Bernard Saanane.
Ben Saanane alikuwa Msaidizi wa Freeman Mbowe Mwenyekiti wa Chadema Taifa – alipotea ghafla takribani mwezi mmoja sasa na hajulikani alipo huku Lissu akiitisha mkutano na wanahabari tarehe 14 Desemba, 2016 na kuitaka serikali ieleza kama inamshikilia kijana huo au la.
Fredrick Kihweru mmoja kati ya wanasheria wa Chadema akitoa maelezo baada ya mahojiano ya polisi na Lissu kumalizika amesema, “aliitwa kuhojiwa juu ya Press conference aliyofanya na kuzungumzia suala la Saanane lakini pia wamemuhoji anamaanisha nini kumwita Rais John Magufuli jina la “Mtukufu.”
Itakumbukwa kuwa Lissu amekuwa akimtaja Rais Magufuli kama “mtukufu” mara kadhaa tangu aliposhitakiwa kwa kutamka kuwa “Dikteta uchwara anapaswa kupingwa kwa nguvu zote” kesi ambayo bado inaendelea mahakamani.
Wakili Kihweru amesema Lissu amehojiwa pia kuhusu hatua yake ya kuitaka Serikali iseme kama haimshikilii Ben Saanane na pia ieleze juu ya mawasiliano yake ya mwisho ya Ben alifanya na nani, wapi na waliwasiliana nini.
Baada ya mahojiano hayo Lissu ameachiwa kwa dhamana na anaweza kuitwa wakati mwingine atakapohitajika.
No comments:
Post a Comment