Tuesday, August 23, 2016

USAHIHI KUHUSU SAFARI YA MWENYEKITI WA CHADEMA TAIFA MHE.FREEMAN MBOWE


Usiku wa Leo Tarehe 22/08/2016 imesesambazwa Taarifa kuwa Mwenyekiti wa Chama Taifa Mhe.Freeman Mbowe amepanga kusafiri nje ya nchi tarehe 28.08.2016 yaani siku 3 kabla ya Maandamano na Mikutano ya Kisiasa iliyopangwa kufanyika kuanzia Tarehe 01.09.2016 kutetea na kulinda katiba na sheria za nchi

Taarifa hizo zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii ziliambatanishwa na Tiketi na Ujumbe Feki ili kuongezea uzito wa habari iliyosambazwa.

Ofisi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa Inakanusha Taarifa hizo za Uongo na Uzushi uliosambazwa kwa makusudi na kwa nia ovu(Maliciously) hasa kipindi hiki ambacho Watanzania Wamejiandaa kikamilifu kutekeleza haki yao ya Kikatiba ya kukusanyika na kupaza sauti zao kupinga Uvunjaji wa katiba na sheria za nchi ifikapo Septemba 01,2016.

Aidha,Watunzi wa Uongo na Uzushi huu wameendelea kuonesha dharau kwa Watanzania kwa kudhania kuwa hawawezi kutofautisha kati ya Tiketi ya Ndege na "Boarding Pass" iliyotengenezwa kwa njia ya Kompyuta kisha kuisambaza na kuupotosha Umma kuwa ni Tiketi ya Ndege.

Kwa kawaida "Boarding Pass" hupatikana siku ya Safari.

Mwenyekiti Wa Taifa Mhe.Freeman Mbowe yupo mstari wa mbele na anaendelea kutekeleza Majukumu yake kuhakikisha Maazimio ya Kamati Kuu juu ya Uanzishwaji na Utekelezaji wa Operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania(UKUTA) inafanyika kwa ufanisi na kwa kiwango cha juu.Hadi sasa Mwenyekiti anaendelea na vikao vya Kimkakati ndani ya Kanda ya Kaskazini kama ilivyopangwa kwa na pia viongozi wenzake ambao ni wajumbe wa Kamati Kuu waliotawanyika nchi nzima wanaendelea kuongoza vikao vya Kimkakati katika Kanda,Mikoa na Wilaya zote Nchini

Mwisho,Sambamba na Jeshi la Polisi kufanya Uenezi wa Operesheni UKUTA kwa kutojua kama umma ulivyoshuhudia kwenye vyombo vya habari jioni hii,Ofisi ya Mwenyekiti Taifa inapenda kuutahadharisha Umma juu ya Propaganda chafu zinazofanywa na Serikali na Chama Tawala kwa Kushirikiana na Vyombo vya Dola katika jitihada za kuupotosha Umma baada ya kuona Vitisho vilivyotolewa na Viongozi wa Serikali hasa Rais Magufuli na hata Jeshi la Polisi kwa kuwakamata na kuwatisha Viongozi Wetu na Wananchi wasio na hatia vimeshindwa kuonesha Dalili za Kuwarudisha nyuma Watanzania katika kutetea Katiba na Sheria za Nchi

Tunawatakia Maandalizi mema katika Ulinzi wa Katiba na Sheria za Nchi

Ahsanteni.

Imetolewa Na:
Ofisi Ya Mwenyekiti Taifa-Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA).

No comments:

Post a Comment