Thursday, July 28, 2016

Mkakati mzito wa Chadema huu hapa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanzisha opereshani “Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania” (Ukuta) ikiwa ni sehemu ya maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi tarehe 23 – 26 mwezi huu, anaandika Pendo Omary.

Utekelezaji wa operesheni hiyo utaenda sambamba na chama hicho kufanya mikutano ya hadhara kuanzia tarehe 1 Septemba mwaka huu, huku viongozi wa chama hicho ngazi ya msingi hadi taifa wakitakiwa kukaa vikao vya kikatiba na kuelekezwa ajenda ya vikao hivyo kuwa ni kujadili hali ya siasa na uchumi.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa amesema, hatua hiyo imechukuliwa ili kujenga jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani.

“Ni wazi sasa kuwa, kuna tishio kubwa dhidi ya ukuaji wa demokrasia hapa nchini mwetu kutoka kwa viongozi wa serikali hii ya awamu ya tano ambao wanakandamiza demokrasia na madhara yameshaanza kulitafuna taifa letu,” amesema Mbowe.

Ametaja baadhi ya matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini kuwa ni; kupiga marufuko mikutano ya vyama vya siasa wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kufanya, kupiga marufuku urushwaji wa moja kwa moja wa mijadala ya Bunge na kudhibiti wabunge wa upinzani bungeni kupitia kwa Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika.

Matokeo mengine ni kuingilia mhimili wa mahakama, kupuuza utawala wa sheria, serikali kupeleka mswada kandamizi wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, serikali za mitaa kunyang’anywa mapato na serikali kuu na uteuzi wa wakurungezi, makatibu tawala wa wilaya bila kuzingatia sheria ya utumishi wa umma.

“Mbali na hayo, serikali pia imetoa maelekezo kupitia mawasiliano yake na mabalozi kuelekeza kuwa, kabala ya mabalozi au maofisa wa ubalozi kukutana na asasi zisizo za kiserikali au vyama vya siasa ni lazima kwanza waombe kibali cha serikali kupitia wizara ya mambo ya nje.

“Pia kwa sababu ya hasira ya kukataliwa na CCM, vikosi vya ulinzi na hasa Jeshi la Polisi vimekuwa vikishiriki katika vitendo kadhaa vya ukiukwaji wa haki za raia huko Zanzibar ambapo kwa zaidi ya miezi sasa, wamekuwa wakipita katika vijiji na kuwapiga, kuwatesa, kuwakamata, kuwatishia na hata kuharibu mali za wananchi na mifugo yao,” amesema Mbowe.

Mwanahalisionline

No comments:

Post a Comment