Sunday, June 5, 2016

Watendaji K’ndoni watangaziwa kiama

BONIFACE Jacob, Meya wa Manispaa ya Kinondoni amewatangazia kiama watendaji wa kata na mitaa ambao wanaihujumu serikali katika ukusanyaji mapato na kukwamisha shughuli za serikali,anaandika Pendo Omary.

Jacob ametoa kauli hiyo leo, wakati wa mkutano wake na watendaji hao, uliohudhuriwa pia na Ally Hapi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.

Kwa mujimu wa Jacob, mpaka sasa tayari watendaji watatu wamefukuzwa kazi na wengine watatu kusimamishwa kupisha uchunguzi kwa sababu ya kuhusika na kutuhumiwa kufuja fedha za maendeleo zinazotolewa na Halmashauri.

“Tayari wapo watendaji wa mitaa na kata waliochukuliwa hatua za kinidhamu. Watendaji wa kata waliofukuzwa ni; Ernest Missa, Ally Bwamkuu na Shabani Kambi yeye amesimamishwa. Watendaji wa mitaa waliosimamishwa ni; Dustan Kikwesha na Richard Supu huku Aneth Lema akifukuzwa,” amesema Jacob.

Jacob amesema watendaji hao wametuhumiwa kusababisha upotevu wa fedha zinazotolewa na Halmshauri zaidi ya Sh. 400 Milioni hali inayochangia kukwamisha maendeleo.

Wakati watendaji hao wakifukuzwa kazi na wengine kusimamishwa, Jacob amesema “kabla ya kumaliza mwaka wa fedha 2015/2016, tuna zaidi ya Sh. 60 Bilioni mitaani hazijakusanywa. Kuna watendaji wengine wanaona sio wajibu wao kuzikusanya.

“Kwa mfano mpaka sasa kata zinazoshika mkia kwa ukusanyaji duni wa kodi ya majengo ni; Mburahati Sh. 1,965,147 Milioni, Kibamba Sh. 1,832,150 Milioni, Mabibo Sh. 1, 824, 803 Milioni, Mabwepande Sh. 1,754,067 Milioni na Kimara Sh. 235,832. Kwa mtu ambaye hatusaidii kwenye jukumu hili tutamtafutia kazi nyingine ya kufanya,” amesema Jacob.

Aidha, amezitaja kata ambazo zimefanya vizuri katika ukusanyaji wa kodi ya majengo kuwa ni; Msasani Sh. 822,581,821, Sinza Sh. 518,136,560, Mikocheni Sh. 215,986,462, Mbezi Juu Sh. 116,170,484 na Bunju Sh. 86,772,400.

Kwa upande wake Hapi amesema “watendaji wetu wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea. Nimeamua kuisaidia Halmashauri ya Kinondoni. Afisa biashara tumemwondoa. Haendani na kasi yetu. Kuna watendaji wanawanyanyasa wananchi, wanawatoza fedha hawawapi risiti. Ninatoa onyo.”

MwanaHalisiOnline

No comments:

Post a Comment