Monday, June 6, 2016

RAIS MAGUFULI AOMBE RADHI WANAFUNZI KWA KAULI ZA UPOTOSHAJI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMARAIS MAGUFULI AOMBE RADHI WANAFUNZI KWA KAULI ZA UPOTOSHAJI

Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) tumeshtushwa na kauli za upotoshaji zilizotolewa jana na Rais John Magufuli alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati alipozindua ujenzi wa jengo la maktaba chuoni hapo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli amesikika na kunukuliwa akiwaambia wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuwa wasikubali kutumiwa na wanasiasa na pia waache siasa, badala yake wajikite katika kile alichokiita ni masomo.

Katika hilo, BAVICHA tunamwambia Rais Magufuli kama hakuwa na nia ya kupotosha na kuudanganya umma wa Watanzania na kuwahadaa wanafunzi wa vyuo vikuu, basi akiambie chama chake cha CCM kwanza kifute Idara ya Shirikisho la Vyuo Vikuu, ambacho ni chombo rasmi kilichopewa majukumu na vikao vya juu vya chama hicho kufanya siasa vyuoni.

Rais Magufuli anajua kwa sababu ni mjumbe wa vikao hivyo. Hata DC wa Kinondoni aliyemteua hivi karibuni, ni kiongozi katika idara hiyo.

Kama Rais anajua maana na tafsiri ya alichokizungumza, basi BAVICHA tunamtaka afute masomo ya siasa vyuoni. Kama hajui au amesahau, kuna wanafunzi wanaosoma masomo ya siasa, mfano Shahada ya Sayansi ya Siasa. Kama hataki wanafunzi wafanye siasa, awaambie watafanyia wapi mafunzo kwa vitendo.

Katika muktadha huo wa kauli za kupotosha na kudanganya umma alizotoa jana mbele ya wasomi, BAVICHA tunamtaka Rais Magufuli awaombe radhi wanafunzi wa vyuo vingine nchini kwa kuwaita kuwa ni vilaza huku akiwagawa katika makundi.

Ni aibu na jambo la fedheha kauli kama hizo za kibaguzi kutolewa na Rais wa nchi ambaye hao wote ni vijana wake ambao serikali anayoiongoza inapaswa kuwajibika kuwatumikia.

Kauli aliyoitoa jana Rais ni ya kuendeleza matabaka, madaraja na baguzi katika elimu ambayo isipokemewa inaligawa taifa.

Kauli hiyo si tu kwamba ni kinyume cha uungwana wa Watanzania bali pia kuendekeza kauli za kibaguzi ni kuvunja Katiba ya nchi.

Katika hali ambayo imetushtua zaidi, Rais Magufuli amepotosha hata sakata la wanafunzi wa UDOM, waliofukuzwa kikatili na Serikali yake kutoka chuoni ndani ya masaa 24 waliodai haki yao ya kufundishwa baada ya kukaa chuoni mwezi mzima bila kufundishwa.

Kama Rais Magufuli hajui au amesahau, BAVICHA tunamkumbusha kwamba wanafunzi hao walikuwa hawasomi masomo ya shahada, bali ilikiwa programu maalum ambayo ipo kwa mujibu wa Sheria iliyopitishwa mwaka 2014 na Bunge.

Sheria hiyo ya mabadiliko ya Sheria namba 4 ya Mwaka 2014 ilisainiwa Disemba 11, 2014 na Rais Kikwete na haijafutwa hadi tunapotoa taarifa hii.

Kama Rais Magufuli ameamua kuwabagua na kuwadhalilisha wanafunzi hao kwa kuwaita vihiyo, awaombe radhi kwa sababu wapo chuoni kwa mujibu wa sheria ambayo ilipitishwa yeye akiwa mbunge na waziri katika serikali hiyo. La sivyo vijana watakuwa na haki ya kutafsiri kuwa serikali iliyopeleka mswada wa sheria hiyo na wabunge walioitunga ni vihiyo?

Kama Rais Magufuli hawaombi radhi wanafunzi hao, tafsiri ya nani kihiyo itakwenda mbele hata kuhoji waliokuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri na Rais aliyesaini sheria hiyo iliyowaruhusu vijana hao kusajiliwa chuoni na kuanza masomo kwa gharama za serikali.

Aidha, BAVICHA inapenda kuhitimisha taarifa hii kwa kuhoji kauli ya Rais Magufuli alipoonekana kuhoji kuwepo kwa barabara hewa alizosema zipo nchini. Tunamtaka asiishie hapo, bali pia awaambie Watanzania barabara hizo zilijengwa na serikali ipi chini ya usimamizi wa waziri yupi, kama si yeye aliyekuwa Waziri wa Ujenzi? Msimamizi huyo naye anastahili kutumbuliwa kwa kusababisha barabara hewa.

Imetolewa leo Ijumaa, Juni 3, 2016 na;
Idara ya Uenezi na Uhamasishaji
BAVICHA-Taifa.

No comments:

Post a Comment