Saturday, May 21, 2016

HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI JUU YA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2015/2016 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017


UTANGULIZI
Awali ya yote naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na kuniwezesha kuwasilisha kwa mujibu wa Kanuni ya 99 (9) toleo la mwaka 2016 , maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani juu ya mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/2016 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini mwaka wa fedha 2016/2017.
Nitumie fursa hii pia kuwashukuru waheshimiwa wabunge na wote mliokuwa pamoja na familia yetu kwa hali na mali katika kipindi kigumu cha msiba wa baba yetu John Michael Dalali, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema.
Aidha niwashukuru wananchi wa Kibamba kwa kunichagua kuwa mbunge lakini pia kuchagua madiwani wa kata zote kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO YA BUNGE KUHUSU RICHMOND NA KUHUSU AKAUNTI YA ‘ESCROW’ YA TEGETA PAMOJA NA UMILIKI WA KAMPUNI YA IPTL
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kurejea maamuzi/maazimio ambayo Bunge hili Tukufu lilikwisha yafanya kuhusiana na mikataba ambayo Serikali inaingia na makampuni mbalimbali hasa kwenye sekta ya nishati na madini.
Mheshimiwa Spika, Taarifa mbili za serikali kuhusu utekelezwaji wa maazimio haya ziliwasilishwa Bungeni tarehe 28 Agosti, 2008 na tarehe 11 Februari, 2009. Taarifa moja ilikabidhiwa na kujadiliwa na Kamati, ambazo zililitaarifu Bunge kuwa utekelezaji wa Maazimio 10 kati ya 23 yaliyotolewa na Bunge, yalifanyiwa kazi hadi mwezi Februari, 2009 na Maazimio 13 bado yalikuwa hayajakamilika.
Mheshimiwa Spika, Bunge liliazimia kwamba taarifa za utekelezaji wa maazimio yaliyobaki ziwasilishwe kwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo hata hivyo kuanzia mwaka 2011 mpaka mwaka huu wa 2016 kamati hiyo haikuwasilisha taarifa yoyote bungeni ya kueleza kukamilika kwa utekelezaji wa maazimio husika hali ambayo inahitaji bunge kuingilia kati kuweza kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara ya 63 (2) na (3).

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani iliitaka Wizara ya Nishati na Madini na Serikali kwa ujumla kutoa majibu bungeni juu ya hatma ya maazimio 10 yaliyobaki: Azimio Namba 3,5,7,8,9,10,11,13,14 na 18 ili bunge liweze kuishauri na kuisimamia serikali kuhakikisha maazimio husika yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa haraka. Lakini hadi sasa tunaposoma hotuba hii maazimio hayo ya Bunge bado hayajatekelezwa na Bunge kupata mrejesho rasmi.

Mheshimiwa Spika, aidha Katika maazimio ya Bunge kuhusiana na fedha ufisadi uliofanyika katika akaunti ya “Tegeta escrow” na umiliki wa IPTL, maazimio yanayohusu sekta ya nishati na madini bado hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake, maazimio hayo yaliyotolewa na Bunge la Kumi, Mkutano wa Kumi na Saba katika kikao cha Ishirini kilichofanyika tarehe 29 Novemba, 2014 katika azimio namba 2,7 na 8.

Mheshimiwa Spika, Bunge katika azimio namba 2 liliazimia kwamba naomba kunukuu;
KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha jinsi ambavyo TANESCO imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama za umeme unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya Shirika hilo;
NA KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba TANESCO itaendelea kulipa fedha nyingi kwa ajili ya gharama za umeme huo wa IPTL;
HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitika kuona kwamba, mbali ya Serikali kushindwa kununua lakini bado inaendelea kulipia gharama za “capacity charges” na hivyo kuendelea kukiukwa kwa azimio ya Bunge. Hivyo basi tunamtaka Waziri alieleze Bunge ni kwa kiasi gani azimio hilo limetekezwa?

Mheshimiwa Spika, katika azimio namba 7 lililohusu kuwajibishwa kwa Mawaziri na watendaji wakuu wa wizara na Bodi ya Tanesco lilisema kwamba, nanukuu;
“KWA KUWA, vitendo vya kijinai wanavyohusishwa navyo viongozi wa umma na maafisa wa ngazi za juu serikalini vinakiuka pia maadili ya viongozi wa umma na kuwanyima viongozi na maafisa hao uhalali wa kuendelea kushikilia nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao;”
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais bila ya kujali nini Bunge lilikwisha azimia katika kikao ambacho na yeye alikuwa sehemu ya azimio hilo, lakini bado akamteua Mhe Prof. Muhongo kuendelea kuiongoza wizara hii. Kambi Rasmi ya Upinzani inaliona jambo hili kama ni dharau sana kwa Bunge na ni fedheha binafsi kwake.

Mheshimiwa Spika, Bunge katika azimio namba 8 la taarifa ya ukaguzi maalum kuhusiana na miamala iliyofanyika katika akaunti ya ‘escrow’ ya tegeta pamoja na umiliki wa kampuni ya Iptl iliazimiwa kwamba
“HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme”
Mheshimiwa Spika, Azimio hili linashabihiana na azimio namba 13 lililoazimiwa na Bunge wakati wa majadala wa taarifa ya kamati teule ya Richmond lililosema kwamba;
“……….. Kamati Teule inatoa wito kwa Serikali kuondokana na utaratibu huu usio na tija kwa kuzihusisha Kamati za Kudumu za Bunge kwenye hatua za awali za maandalizi ya mikataba hiyo. Aidha, Kamati Teule inatoa wito kwa Kamati zote za Bunge zihakikishe kuwa zinapitia mikataba mikubwa na ya muda mrefu ya kibiashara chini ya sekta zao ili kuliondolea Taifa mizigo isiyo ya lazima. Pale ambapo upatikanaji wa mikataba hiyo unakwamishwa kwa urasimu usio wa lazima Kamati zitumie utaratibu uliotumiwa na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara ya kuunda Kamati Teule yenye ufunguo wa mikataba iliyofichika”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imelazimika kunukuu maazimio hayo kutokana na ukweli kwamba Serikali imeshindwa kabisa kutekeleza maazimio ya Bunge, na badala yake mikataba hiyo inaendelea kutekelezwa kama ilivyoingiwa, mfano mzuri ni TANESCO kuendelea kuilipa IPTL fedha za capacity charge mpaka sasa. Jambo hili linazidi kuliondolea shirika hilo la umeme uwezo wa kuwahudumia wateja wake kwani haliwezi kuwekeza zaidi katika miundombinu za kusambaza umeme kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha.
Mheshimiwa Spika, mfano mwingine wa mikataba yenye mashaka ni ule wa Mchuchuma na Liganga ambao NDC iliingia ubia na kampuni ya kichina ya HONGDA SICHUAN LTD na kuunda kampuni ya Ubia ya Tanzania China Internatinal Mineral Resource Ltd- TCIMRL katika kampuni hiyo ya ubia HONGDA SICHUAN LTD inamiliki asilimia 80 na NDC inamiliki asilimia 20.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wabia wanakuja mikono mitupu bila hela, sasa mbia mkubwa anatafuta mtaji kwa kutumia rasilimali za Kampuni ya ubia kama dhamana. Hizi rasilimali za Kampuni ya ubia ni zile zinazotakiwa kuchakatwa na kuuzwa, katika mazingira yoyote yale tukakubali vipi kuwa ubia wa njia hii unainufaisha nchi?
Mheshimiwa Spika, kama tunaweza kutumia rasilimali zetu kama dhamana ni kwanini tuingie ubia na tusitoe ajira kwa wataalamu waliobobea katika fani hizo na sisi tukawa na umiliki wa asilimia 100?
Kambi Rasmi ya Upinzani inasema mikataba ya jinsi hii ndiyo itakayoliangamiza taifa letu, ni kwa nini wataalam wanaoingia mikataba ya namna hii wanatakiwa kuendelea kuwa maofisini?
Mheshimiwa Spika, licha ya ubabaishaji wa Kampuni hiyo ya Kichina bado ina uhakika kwamba mkopo wa kutumia rasilimali zetu ukipatikana ianze kuiuzia Tanesco umeme wa 600MW, hoja ya msingi je uhalali wa TANESCO kununua umeme wa Mchuchuma na Liganga utakuwa wapi?
Endelea.....

UAGIZAJI WA MAFUTA BILA USHINDANI
Mheshimiwa Spika, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wa Serikali ya Awamu ya Nne katika mabadiliko ya mwisho George Simbachawene, aliagiza mafuta kwa ajili ya miezi ya Septemba, Oktoba na Novemba 2015 bila ya ushindani.
Mheshimiwa Spika, uamuzi wa waziri huyo ambaye sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), ulisababisha mafuta hayo kununuliwa kwa Sh40 bilioni, ambayo ni mara mbili ya bei ambayo ingetumika kama zabuni zingeshindanishwa. Aidha, uamuzi huu ulisababisha wananchi kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kutokana na pamoja na mambo mengine kuongezeka kwa gharama za uagizaji.
Mheshimiwa Spika, wakati waziri akifanya uamuzi huo, tayari Ewura ilikuwa katika mchakato wa tenda za kuagiza mafuta hayo na tenda hizo namba 37, 38 na 39 za Septemba, Oktoba na Novemba, ambazo tayari zilikuwa zimepokelewa kwa ajili ya kushindanishwa.
Mheshimiwa Spika, historia inaonesha kuwa Sekta ya mafuta ndiyo kimekuwa kichaka kikuu cha kuficha ufisadi mkubwa, kwani waziri utetezi wake ni kuwa alifanya kwa nia njema. Hiyo nia njema ya Mhe Waziri ambayo haikuzingatia ushindani na kupuuza ushauri wa mamlaka husika inapimwa vipi? Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa; “Uamuzi wa waziri kupuuza ushauri wa Ewura ambayo ni mamlaka ya udhibiti, unaonyesha ipo haja ya uchunguzi juu ya nini kilimsukuma kuchukua uamuzi huu,” Hapa lipo jipu linalohitaji kutumbuliwa.
USHAURI WA JUMLA KATIKA SEKTA YA NISHATI
Mheshimiwa Spika, Unaposema Wizara ya nishati na madini kwa watanzania wengi jambo linalokuja vichwani mwao ni uzalishaji na uuzaji wa umeme wanaotumia katika shughuli zao za kila siku za uzalishaji na matumizi ya majumbani. Japokuwa wizara hii ina majukumu makubwa ya kuhakikisha rasilimali ya madini iliyopo hapa nchini, ile ambayo imeanza kuvunwa na ambayo hadi sasa haijaanza kuvunwa inatumika katika hali ambayo inatakiwa iwanufaishe watanzania wa sasa na wale ambao hawajazaliwa.
Mheshimiwa Spika,Umeme kama kichocheo cha maendeleo ya kukua kwa uchumi na vile vile kuongezeka kwa kipato cha wananchi kwa kuweza kumiliki na kuzitumia vyema rasilimali zinazowazunguka, hivyo basi hata rasilimali zingine kama madini haziwezi kuwa na thamani kama hakutakuwa na umeme wa kuwezesha kuzitoa huko ziliko na kuzipatia thamani inayostahili.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano ambao ni muendelezo wa miaka mitano iliyopita unakusudia kuwa Tanzania iendeshwe na uchumi wa viwanda. Katika kufika huko umeme wa uhakika katika sekta ya uzalishaji viwandani ni muhimu sana. Hatuwezi kuanzisha na kuendesha viwanda kwa kuwa na umeme usiokuwa na uhakikia, kufanya hivyo bidhaa zitakazozalishwa zitakuwa ni ghali sana kwa kulinganisha na uzalishaji bidhaa kama zetu toka nchi zingine jambo ambalo zitashindwa kushindana kwa bei sokoni.
Mheshimiwa Spika, Katika sekta ya Nishati, Mpango uliweka lengo la kuzalisha 2,780 MW za Umeme kwa kipindi cha miaka 5. Maana yake ni kwamba kila mwaka ilitakiwa kuzalisha 556 MW ili kufikia lengo lililowekwa na Mpango.

Mheshimiwa Spika, Utekelezaji- kwa kipindi cha miaka 5 zimeweza kuongezeka 496.24 MW katika uzalishaji wa umeme nchini. Hii maana yake ni kwamba kila mwaka tuliongeza uzalishaji wastani wa 100 MW za umeme nchini. Kwa mwenendo huu ili kufikia lengo la kuzalisha 2,780 MW tunahitaji miaka 13 ili kuweza kufikia lengo la Mpango wa miaka 5 ya awamu ya kwanza.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa maelezo mbele ya Bunge hili ni kwanini haikutekeleza lengo la Mpango wa Maendeleo la kuzalisha 2,780 MW za umeme?

MPANGO WA UMEME WA DHARURA
Mheshimiwa Spika, Mpango wa umeme wa dharura unaweza kutafsiriwa kama ni mapungufu ya sera ya nishati kutokuwepo kwa mpango wa muda mrefu ambao unaambatana na uzalishaji utakaoangalia mahitaji.
Mheshimiwa Spika, Kutokufanya vizuri kwa shirika letu la umeme kwa kiasi kikubwa kumetokana na Serikali kuingia mikataba na makampuni binafsi ili kuzalisha umeme wa dharura na kuliuzia shirika letu la umeme.

Mheshimiwa Spika, Hadi sasa mitambo ya kukodisha ambayo inazalisha umeme na kuuza kwa Tanesco ni; mtambo wa gesi wa Symbion 112MW, Aggreko Ubungo 50MW, Aggreko Tegeta 50 MW, Symbion Dodoma 50MW. Mipango mingine ya muda mfupi ni pamoja na Jacobsen (gas) awamu ya kwanza 100 MW ilikuwa USD 124 million Jacobsen awamu ya pili 150 MW ilikuwa USD 165 million.

Mheshimiwa Spika, Sekta ya uzalishaji wa umeme imekuwa ndiyo sekta yenye ukiritimba, jambo linalopelekea kuwa sekta yenye rushwa kubwa kubwa, jambo hilo linasababisha wawekezaji wengi wanaotaka kuzalisha umeme kushindwa kufanya hivyo. Mfano mzuri ni mvutano mkubwa uliokuwepo kati ya RUBADA na TANESCO kuhusu uzalishaji wa umeme wa maji kwenye mabonde ambayo yanamilikiwa na Mamlaka hiyo.
Mheshimiwa Spika, Moja katika ya rasilimali kuu za Bonde la Rufiji ni chanzo cha uzalishaji umeme wa maji, kwa utafiti uliofanywa na RUBADA mwaka 1984 kwa kutumia kampuni ya Norway ya Norconsult kwenye Rufiji Basin Hydropower Master Plan ilionesha kuwa bonde lina vyanzo vikuu vinane vya uzalishaji wa umeme na vyanzo hivyo ni; Stiegler's Gorge, Mpanga, Ruhudji, Mnyera, Iringa, Lukose, Kihansi and Kilombero.
Mheshimiwa Spika, Bonde la Mto Rufiji linauwezo wa kuzalisha umeme wa mpaka 2729MW bila ya kuathiri shughuli zingine za kiuchumi. Lakini kwa sasa Bonde la Mto Rufiji lina mabwawa matatu tu yanayotumika kwa ajili ya uzalishaji wa umeme ambayo ni Kidatu, Kihansi na Mtera ambayo yanazalisha umeme wa 460 MW tu.
Mheshimiwa Spika, Inasadikiwa kwamba Tanzania inauwezo wa kuzalisha umeme wa maji wa 4700MW kwa kutumia mabonde yake ya mito sita, ambayo ni;Rufiji, Pangani, Kagera, Malagarasi, Ruvuma na Rumakali . Kwa Bonde la Mto Rufiji kuhusu uzalishaji wa umeme hapa nchini, mradi wa STIEGLER’S GORGE pekee toka miaka ya 1980 upembuzi yakinifu ulikwishafanywa na kuonekana kuwa ndio chanzo ambacho kingeweza kuzalisha umeme wa kutosha kwa mahitaji ya matumizi yote ya viwandani na majumbani kwa gharama nafuu. Chanzo hiki ndicho kilikuwa chanzo cha uhakika kwa kuiweka Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa Kati.
Mheshimiwa Spika,Kwa mujibu wa upembuzi yakinifu uliofanyika miaka hiyo ya 80 inaonesha kuwa mbali ya Stiegler’s Gorge RUBADA inavyanzo vingine vya kuzalisha umeme wa maji, ambavyo ni;
Mpanga linauwezo wa kuzalisha….. 165MW
Ruhundji linauwezo wa kuzalisha….. 685MW
Mnyera ………………………. 485MW
Lukose …………………………………….130MW
Kilombero (Kingenenas&shughuli falls)…464MW
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kuelezwa toka upembuzi huo ufanyike ni hatua gani tena imeishafanyika kuona vyanzo hivyo vinatumika kuzalisha umeme kwa matumizi ya maendeleo?
Mheshimiwa Spika, Miradi ya uzalishaji umeme wa maji kama huu tunaousema wa Stiegler’s Gorge zipo pia katika nchi za Brazil kwenye bwawa la Itaipu linalozalisha 10,200MW, China yenye mabwawa matatu yanayozalisha 22,500MW na nchini Venezuela yenye bwawa la Guri lenye kuzalisha umeme 10,200MW.
Mheshimiwa Spika, Umeme uzalishwao kwa kutumia nguvu za maji (hydroelectric power) huu ni uzalishaji rahisi na unatunza mazingira, tofauti na aina zingine za uzalishaji wa umeme ambazo kwanza sio endelevu.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa ni dhahiri toka utafiti ulipofanyika hadi sasa ni muda mrefu sana na Serikali imekwishatumia mabilioni ya fedha kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme, jambo ambalo kama uamuzi ungefanyika kabla kwa sasa tusingekuwa tunahangaika na matatizo ya umeme kwa utafiti uliofanyika wa chanzo hicho cha Stiegler’s Gorge tungekuwa na umeme wa kutosha na pengine tungekuwa tunauza kwa majirani zetu.
KAMPUNI YA KUZALISHA UMEME WA MAJI -Aldwych International Ltd
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Aldwych International Ltd ya Uingereza ndiyo iliyokuwa inashughulika na kuendeleza mradi wa umeme wa Ruhudji toka mwishoni mwa mwaka 2006.
Mradi wa Ruhudji wa uzalishaji 360 MW, kwa mujibu wa Power system Master Plan (PSMP) mwanzoni ulipangwa kumalizika 2014. Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuelewa hadi sasa utekelezaji wa mradi huo na Kampuni tanzu ya Aldwych International Ltd ambayo itaingia ubia na Tanzania iitwayo Ruhudji Power Development Company Limited, (RPDC) umefikia kiwango gani?
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuiasa Serikali kwamba miradi kama hiyo ya uzalishaji umeme wa muda mrefu inatakiwa kuwa makini na aina ya mkataba “Implementation Agreement and Power Purchase Agreements” utakaoingiwa isije ikawa kama mikataba iliyopo ya umeme wa dharura.

Mheshimiwa Spika, Ni ukweli kuwa mizania ya TANESCO inaonesha kuwa shirika hilo limekuwa likifanya biashara kwa hasara kutokana na gharama za uzalishaji kuwa kubwa kuliko bei ya kuuzia umeme huo hasa ni kwa umeme unaozalishwa na wazalishaji binafsi na kuiuzia TANESCO.

SHIRIKA LA MAENDELEO YA PETROLI TANZANIA-TPDC
Mheshimiwa Spika, Shirika hili la mafuta ndilo lililo na jukumu la msingi la kuhakikisha kuwa raslimali ya mafuta na gesi iliyo hapa nchini inajulikana ilipo na inajulikana kiasi cha hazina kilichopo na inavunwa na nani na watanzania watanufaika vipi na raslimali hizo. Katika kutekeleza hayo yote shirika kwa mwaka wa fedha 2015/16 liliomba kiasi cha shilingi bilioni 12 kama fedha za maendeleo, lakini hadi kamati za Bunge zinakutana hakuna hata shilingi iliyokuwa imetolewa na hazina kama fedha za maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha TPDC imetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.5 fedha za maendeleo zikiwa ni fedha za ndani, kati ya fedha hizo shilingi milioni 700 ni ujenzi mtandao wa kusambaza gesi asili kwa mikoa ya Mtwara na Lindi na shilingi milioni 800 ni mradi wa kuchakata gesi asili na kuwa kimiminika kwa ajili ya kuisafirisha nje na ndani ya nchi ikiwa imesindikwa, na shilingi bilioni 9.2 fedha za nje.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani imeeleza hapo awali kwamba kazi ya kusimamia kwa kuelewa rasilimali ya mafuta na gesi ilipo na ni kiasi gani kilichopo ni kazi inayohitaji rasilimali. Kitendo cha kukosa fedha kwa ajili ya kutekeleza jukumu hilo ni dhahiri kwamba makampuni yanayojihusisha na biashara hiyo, ambayo kwayo ni lazima yawe na fedha za kutosha ni rahisi kuiweka TPDC mfukoni mwake na mwisho wa siku watanzania wakakosa kunufaika na rasilimali hizo.

Mheshimiwa Spika, katika biashara yoyote kuonesha hali yoyote ya unyonge maana yake ni kuweka haki zako rehani, na vivyo hivyo TPDC kukosa fedha za miradi ya maendeleo ni kuweka sekta hii ya mafuta rehani.

Mheshimiwa Spika, Ukosefu wa fedha unaolikumba shirika hili ndio unaopelekea mapato ya gesi kutokukusanywa kwa kadri mikataba na sheria zinavyosema. Kwa mujibu wa taarifa ya TPDC inaonesha kuwa Songas inadaiwa jumla ya shilingi 50,275,344,006/-na Pan African Energy inadaiwa jumla ya shilingi 60,665,839,011/-. Kwa kampuni zote hizo zinadaiwa na TPDC jumla ya shilingi bilioni 110.94 Je, kwa mwendo huu gesi hii inaweza kuwa na manufaa kwa wananchi, Kama madeni yanashindwa kudaiwa kwa kusimamia mikataba iliyopo?

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni kwamba TPDC imeshindwa kupokea Gawio lake toka kwa songas lenye thamani ya dola za kimarekani 467,997 na hivyo kuzidi kuwa hoi kifedha. Kambi Rasmi ya Upinzani inaliangalia hili la TPDC kushindwa kupata stahili zake kutoka kwenye makampuni hayo ya gesi kutokana na ukweli kwamba mikataba iliyoingiwa pengine kuna vifungu vinavyoshindwa kutoa kazio la mikataba au ni kutokana na watendaji kuwekwa kwa mtindo wa kubebana na hivyo kushindwa kutimiza majukumu yao ya kimsingi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema Serikali wakati inajumuisha itoe majibu kwa hoja zote tajwa kwani Katika Bajeti zetu za nyuma tulizungumzia kuhusiana na muundo mpya wa utendaji wa TPDC ambao ulikuwa unatia mashaka lakini ulipata Baraka zote za Wizara ya Nishati na Madini.

SEKTA YA MADINI
Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imejaaliwa wingi wa madini ya kila aina, hata hivyo, madini haya hayatatusaidia sana kama hatua madhubuti hazitachukuliwa dhidi ya mapungufu yaliyomo kwenye sera ya madini inayojenga mazingira mazuri kwa wageni kumiliki utafutaji na uchimbaji madini hapa nchini dhidi ya ushiriki wa wazawa.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya mapungufu hayo kama yalivyobainiwa na Kambi Rasmi ya Upinzani ni:
Serikali imekabidhi utafutaji na uchimbaji madini mikononi mwa sekta binafsi ndani ya utandaawazi ulimwenguni, pasipo kuzingatia kuwa sekta binafsi ya Tanzania bado ni changa kushindana na makampuni ya kimataifa.
Kuwalipisha wazawa na wageni ada na tozo sawa kwenye madini kama vile wageni wana haki sawa na wazawa, kwenye rasilimali zinazopatikana nchini Tanzania.
Serikali kutumia misamaha ya kodi kwenye sekta kama njia ya kuvutia wawekezaji badala ya kutengeneza mazingira wezeshi, kama vile nishati na miundombinu ya uhakika katika maeneo ya uchimbaji na hivyo kupelekea sekta kutokutoa pato stahiki kwa nchi. n.k

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali, kwanza kurekebisha mapungufu ya kisera kwani Duniani kote rasilimali zinazoisha kama madini kipaumbele kinawekwa kwa wazawa badala ya wageni. Kwa njia hiyo ndipo rasilimali hizi zitakuwa na thamani na faida kwa watanzania.

WACHIMBAJI WADOGO WADOGO
Mheshimiwa Spika, unaposema sekta ya madini, kwa uelewa wa haraka wa watanzania waliowengi maana yake ni wachimbaji wadogo. Hii inatokana na ukweli kwamba wachimbaji wadogowadogo ndio ambao mchango wao unaonekana wazi katika maendeleo ya nchi yetu, hata kama sio kwenye ukokotozi wa pato la taifa. Lakini ukweli ni kwamba maisha ya watu wengi yanabadilishwa na wachimbaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa ruzuku kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili kuwawezesha kuimarisha mazingira ya kazi zao. Lakini kumekuwa na malalamiko kuwa utoaji wa ruzuku hiyo hauna utaratibu unaoeleweka kwani walengwa hawanufaiki na fursa hiyo. Malalamiko haya yanatolewa na wachimbaji wadogo wanaotoka kanda ya ziwa (Shinyanga, Geita, Mwanza, Mara, Simiyu na Kagera) ambao ni takriban 80% ya wachimbaji wadogo nchi nzima. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza utaratibu unaotumika kwao kupatiwa ruzuku hiyo ya Dolla za Marekani 100,000 kwa kila mwaka, bila ya kuwepo uratibu na utaratibu unaoeleweka lazima upendeleo utakuwepo kwa watu walio karibu na watendaji wa wizara katika kupata fedha hizo.
Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wapo karibu kila sehemu ya nchi yetu, na malalamiko ya wachimbaji hao kwamba hawatendewi haki na Serikali kwa kuwatoa au kuwafukuza katika maeneo ambayo wamegundua kuwa kuna madini. Kilio hicho kipo pia katika mgodi wa Busekela Mkoa wa Mara, Wilaya ya Musoma Vijijini unaomilikiwa na Kampuni ya Dolphine Mines, lakini wachimbaji wanaozunguka mgodi huo wanasumbuliwa sana japokuwa mgodi huo unajulikana ni wa wachimbaji wadogo,lakini Serikali inashirikiana na Kampuni hiyo ya Dolphine kuwanyanyasa wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, Aidha huko huko Musama Vijijini, Jimbo la Butiama kuna mgodi ambao upo katika kijiji cha Nyamikoma, Kata ya Kyanyari kuna Kampuni ya madini ya M/S HENAN AFRO ASI-GEO ENGINEERING (T) Co. LTD ambayo sasa ni takribani miaka 8 wanafanya utafiti na muda wa utafiti ulitakiwa umalizike mwaka huu mwezi wa Mei, lakini Mkuu wa wilaya alitoa kibali bila ya utaratibu cha kuwaongezea muda wa utafiti kwa barua yake ya tarehe 27/4/2017 yenye Kumb. Na. AB. 128/270/01/A/66 kwenda kwa Afisa Tarafa wa Tarafa ya Makongoro. Utafiti huo umeharibu sana miundombinu ya barabara na mazingira.
Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wadogo wa Geita wamekosa maeneo ya kufanyia shughuli zao kutokana na ukweli kwamba maeneo waliyokuwa wanafanyia shughuli zao yamehodhiwa na Mgodi wa Geita Gold na watu wengine ambao wamepewa umiliki na Serikali lakini maeneo hayo hayatumiki.
Mheshimiwa Spika, ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kuwapatia wanachi maeneo ambayo hayatumiwi na mgodi ili wajasiriamali waweze kufanyakazi yao.
Mheshimiwa Spika, kuna tatizo lingine ambalo wachimbaji wadogo na wananchi wa Geita wanakutana nalo na Mhe. Makamu wa Rais alitoa ahadi kwamba mabaki ya mchanga unaotoka migodini (Magwangala) watapewa wananchi ili wafanye uchenjuaji upya wa kutafuta dhahabu kutoka kwenye mchanga huo. Ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Tarime ina mgodi wa North Mara ambao sasa unaitwa ACCACIA, ulianza rasmi mwaka 1994 lakini ulikuta wananchi katika eneo hilo la Nyamongo wakiwa wanachimba madini eneo la Nyarugusu na Nyabirama. Baada ya wawekezaji kupewa leseni, Dar es Salaam walitwaa eneo hilo bila kuwaachia wananchi wa Tarime hata eneo la mita tano kuchimba.
Mheshimiwa Spika, matokeo yake ni wananchi kuuawa kila mara kwa kisingizio cha kuingia mgodini. Tangu mwaka 1994 zaidi ya watu 400 wamekwisha uawa na wengine wengi wamebaki na vilema vya maisha na bila kutafuta suluhisho. Mgodi wa Nyamongo tofauti na migodi mingine uko katikati ya makazi ya watu, hivyo wananchi walitakiwa kuhamishwa kwa kulipwa fidia ili kupisha shughuli za uchimbaji kama inavyosema Sheria ya madini ya mwaka 2010. Lakini hadi sasa watu wanaishi mita takriban mbili kutoka mgodini kinyume cha sheria inayosema wawe umbali wa mita 200 kutoka eneo la mgodi.
Mheshimiwa Spika, ukifanyika ulipuaji wa miamba athari kubwa zinawakumba wakazi hao ikiwemo kuathirika kiafya kutokana na vumbi kali, wengine kupatwa na mistuko ya moyo, nyumba zao kuwa nyufa n.k
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inazo taarifa kuhusu Kamati ya Kupitia Matatizo yote yanayowakabili wananchi wa Nyamongo na Kampuni ya ACCACIA iliyoundwa na Mheshimiwa Waziri. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka taarifa hiyo iharakishwe ili kunusuru majanga yasiendelee kwani tayari mauaji yanaendelea, ambapo kijana mmoja alipigwa risasi na askari hivi karibuni.
MALALAMIKO YA KAMPUNI YA BISMARK HOTEL (MINING) LIMITED
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa taarifa ilizonazo ni kuwa kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya Kampuni ya uchimbaji madini ya Bismark Hotel (Mining) Limited dhidi ya Kampuni za madini za Pangea Minerals Limited, Barrick Exploration Africa Limited na Acacia Mining PLC (zamani Barrick Gold PLC) ambapo kampuni hizo za kigeni ziliingia kwenye makubaliano ya pamoja na kampuni ya Bismark ya kupangisha eneo la kuchimba madini la Mgusu huko Geita mwaka 1995.
Mheshimiwa Spika, mgogoro huu kwa upande mmoja unaihusisha Wizara ya Nishati na Madini ambapo imedaiwa kutoa tafsiri tofauti ya kifungu cha 15(2) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kuhusiana na muda wa eneo lililokwisha muda wake wakati wa kuhuisha leseni za utafutaji madini kuwa wazi kabla ya kuruhusiwa maombi mapya katika eneo husika. Hii ni kutokana na matakwa ya kisheria kutoa miezi minne kabla ya kutoa leseni nyingine katika eneo ambalo leseni yake imefikia kikomo.
Mheshimiwa Spika, taarifa zinaonesha kuwa sehemu ya eneo la Mgusu leseni yake ilifikia kikomo lakini kabla ya miezi minne kumalizika ikatolewa leseni mpya kwa Barick Gold/Acacia Mining PLC badala ya kampuni ya Bismark ambayo ilitii matakwa ya kisheria kusubiri muda wa miezi minne umalizike kabla ya kupeleka maombi mengine Wizarani kuomba kuhuisha leseni yao ya awali.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa kauli hapa Bungeni kutokana na sakata hilo kwa kuwa serikali yenyewe kupitia Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikitoa mara kwa mara tafsiri tofauti ya kifungu cha 15(2) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Aidha Waziri atoe kauli mbele ya Bunge lako tukufu kuhusu hatua gani zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya Eng. John M. Nayopa ambaye ametuhumiwa kuhusika katika sakata hili wakati wote na taarifa zake kupelekwa TAKUKURU na kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali.
Mheshimiwa Spika, ni vema na ni sahihi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuishauri Wizara kuhakikisha inalimaliza jambo hili kwa wakati ili kuhakikisha pande zote mbili haziendelei kutumia gharama kubwa wakati huu ambapo bado inaonekana kuna mgogoro na pia kuhakikisha kuwa mwenye haki yake katika jambo hili anaipata kwa wakati.

TAKA SUMU ZINAZOTOKA KATIKA MGODI WA GEITA NA TATIZO LA MPAKA KAKOLA
Mheshimiwa Spika, mtaa wa Nyakabale, kata ya Mgusu ni mtaa uliokuwepo hata kabla ya uwepo wa Kampuni ya uchimbaji madini ya Geita kuanza shughuli zake katika wilaya hiyo. Katika umilikishaji Mgodi, ilikuja kubainika kuwa Kata ya Mgusu imo ndani ya mipaka ya Mgodi na pia wako karibu na shughuli za mgodi.
Mheshimiwa Spika, katika shughuli za mgodi, lilichimbwa bwawa kubwa ambalo linatumika kumwaga taka zitokanazo na uchenjuaji wa dhahabu. Taka sumu hizo zimekuwa na madhara makubwa sana ya kiafya kwa wakazi wa Mtaa wa Nyakabale. Kwa kuwa imeshindikana kwa mgodi kutoa fidia iliyo timilifu kwani Mgodi unadai kuwa eneo hilo unalimiliki kihalali wakati makosa ya yalifanywa na Serikali kwa kujua au kutokujua wakati wanatoa haki ya umiliki kwa mgodi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulichukulia kwa umuhimu wa kipekee suala la ulinzi wa afya za wakazi wa Mtaa huo wa Nyakabale. Ni muhimu sana kwani uwepo wao hapo sio kwa bahati mbaya bali ni haki yao kutoka kwa mababu zao.
Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwa wakazi wa Mtaa wa Nyakabale, kwa mkoa wa Shinyanga, Jimbo la Msalala Kijiji cha Kakola kinakabiliwa na tatizo la Mgodi wa Bulyanhulu kuweka mipaka kuzunguka kijiji kizima wakati wao wanafanya shughuli zao katika eneo dogo tu. Jambo hili linawafanya wanakijiji cha Kakola kukosa huduma stahili, na wao kuweza kuendeleza eneo hilo. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa suluhisho kwa wanakijiji hao, kwani makosa yalifanywa na Serikali wakati wanatoa ardhi kwa mgodi. Sambamba na hilo wakazi wengi katika kijiji hicho wanafanya kazi za uchimbaji madini, hivyo hawawezi kupewa leseni ya kufanya kazi hiyo kwani kijiji kizima inaonesha kinamilikiwa na mgodi wa Bulyanhulu.
WAKALA WA USAMBAZAJI UMEME VIJIJINI-REA

Mheshimiwa Spika,wakala huyu alianzishwa kwa sheria Na 8 ya mwaka 2005 na alianza kazi rasmi Oktoba mwaka 2007, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2003. Lengo likiwa ni kuwapatia wananchi waishio vijijini nishati bora. Pamoja na umuhimu wa wakala huyu bado serikali haijaonyesha kwa vitendo kuwa ina nia ya kusaidia wakala huyu ili aweze kutimiza majukumu yake kikamilifu na hasa linapokuja suala la kuupatia fedha kama zinavyoombwa na zinavyopitishwa na Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 wakala alitengewa jumla ya shilingi 420,492,701,200/- kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake. Lakini kwa mujibu wa taarifa ya utendaji ya Wakala ni kwamba hadi Desemba 2015 zilikuwa zimepokelewa jumla ya shilingi 141,163,133,226/- tu ambazo ni sawa na asilimia 34. Kati ya fedha hizo hakukuwa na fedha zozote zitokanazo na tozo ya mafuta.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa takwimu za wakala wa Uagizaji mafuta kwa pamoja (PBPA) zinaonesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2015/16 wakala uliingiza mafuta ya Petrol jumla ya tani 571,681, mafuta ya Diesel tani 1,052,129 na mafuta ya taa tani 12,238.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sheria ya fedha iliyopitishwa na Bunge lako tukufu ilitoa haki kwamba kila lita moja ya mafuta ya petrol na mafuta dizeli ikatwe shilingi 100 na shilingi 150 zikatwe kwa kila lita moja ya mafuta ya taa, na zipelekwe kwa wakala wa umeme vijijini kwa ajili ya kuimarisha usambazaji wa umeme vijijini.
Mheshimiwa Spika, kwa mahesabu ya tani hizo zilizoagizwa na wakala ni kwamba tozo za mafuta ya petrol na diesel kwa jumla ya tani 1623810 ni shilingi 162,381,000,000/- na kwa tani 12,238 za mafuta ya taa sawa na shilingi 1,835700,000/-. Na hivyo jumla ya fedha za tozo tokana na mafuta ni shilingi 164,216,700,000/-

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba kwa mwelekeo gharama za miradi ya umeme ambayo inatekelezwa na makandarasi mbalimbali ni dhahiri fedha hizo kama kweli zilitolewa ni uhakika kwamba madeni inayodaiwa wakala yasingekuwepo.
Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mhe Waziri alieleze Bunge ni kiasi gani hadi sasa cha fedha za tozo ya mafuta kati ya fedha tajwa hapo awali kimepelekwa REA.

Mheshimiwa Spika,kwa mwaka huu wa fedha REA imetengewa jumla ya shilingi 587,613,169,000/- zikiwa na feha za maendeleo, na kati ya fedha hizo shilingi 53,213,169,000/- ni fedha za nje.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya wakala inaonesha kuwa kuna miradi inayoendelea ya kuweka umeme ya kutoka mwaka wa fedha 2015/16 na bado REA haijamaliza kuwalipa wakandarasi wa miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2016/17 REA imetengewa jumla ya shilingi 587,613,169,000/- kama fedha za maendeleo. Aidha, kwa kipindi cha mwaka 2015/16 kuna miradi ya umeme iliyokuwa inatekelezwa kwa mwaka huo na wakandarasi hawakulipwa, na hivyo kufanya Ankara ambazo hazijalipwa (outstanding invoices) zenye thamani ya shilingi bilioni 94, na miradi mipya ambayo inatakiwa kutekelezwa katika bajeti ya mwaka huu wa 2016/19 ina thamani ya shilingi bilioni 512.143.

Mheshimiwa Spika, kama fedha za miradi ya nyuma zitalipwa, miradi ya mwaka huu itakuwa na nakisi ya shilingi bilioni 18.63 kwa maana kuwa Ankara zisizolipwa ukijumlisha na miradi mipya ukilinganisha na bajeti ya maendeleo iliyotengwa kwa mwaka huu.

SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA- STAMICO

Mheshimiwa Spika, STATE MINING CORPORATION (STAMICO)ni shirika la umma lililo chini ya wizara lilianzishwa chini ya sheria ya makampuni sura 257 ya mwaka 1972 na pia sheria hiyo ikafanyiwa marejeo au marekebisho 2014. Sera mpya ya madini ya mwaka 2009 ambayo iliifuta sera ya madini ya mwaka 1997, lengo kuu la sera hiyo mpya ilikuwa ni kuifanya serikali kushiriki katika uwekezaji wa madini kwa kupitia taasisi zake kama sera hiyo inavyosema.
Mheshimiwa Spika, Ili kwenda sambamba na sera hiyo ya madini ya mwaka 2009, Bunge lilitunga sheria mpya ya madini ya mwaka 2010 ambayo iliweka kifungu ambacho kinaipa haki Serikali kupitia taasisi zake kujihusisha na uwekezaji katika madini. Katika kufanya hivyo, STAMICO ikawa ndio taasisi ya Serikali inayoendesha jukumu hilo na likafanyiwa maboresho ya kimuundo.
Mheshimiwa Spika, Serikali kuwekeza katika sekta ya madini na kuweza kuwa na ushindani katika sekta kunahitaji mtaji mkubwa sana. Hivyo basi kitendo chochote cha kutokuiwezesha vya kutosha STAMICO ni kuipa uhuru wa kuendelea kupokea mshahara bila ya kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, katika maombi ya fedha kwa mwaka 2016/17 inaonesha kwamba STAMICO imetengewa fedha za matumizi ya kawaida tu, na fedha hizo kwenye kitabu cha IV cha Matumizi ya Wizara na taasisi zake kwa kulinganisha takwimu hizo utakuta tofauti ya shilingi 36,265,000/- (Randama Tshs 4,634,402,000/- Vol. IV inaonesha Tshs.4,670,667,000/-)
Mheshimiwa Spika, Dhana ya uanzishwaji wa STAMICO kwa mujibu wa sheria ilikuwa ni kuwa itakuwa na uwezo wa kushindana au kufanya biashara ya uchimbaji wa madini kwa niaba ya Serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa kwa kuwa kila kitabu kina zama zake, kwa sasa hiyo dhana ya STAMICO kuwa ya kibiashara imepitwa na wakati na ili kuifanya kuwa hivyo itabidi bajeti zetu za Serikali za miaka kama 20 ndizo ziwekezwe STAMICO, na ukweli jambo hilo haliwezekani.
Mheshimiwa Spika, taarifa zinaonesha kuwa STAMICO ilikabidhiwa mgodi wa TULAWAKA ukiwa unafanya kazi kwa maana ya mitambo na magari na fedha kwa ajili ya pale mgodi utakapofungwa kurudisha mazingira katika uhalisia wake kwa mujibu wa hitajio la sheria ya Mazingira.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua Annual turnover ya Mgodi huo tangu uchukuliwe na STAMICO ni kiasi gani? Aidha, Kambi inataka kujua ni shilingi ngapi Kampuni ilipewa na AFRICA BARRICK GROUP kama fedha za kufunga Mgodi kama mgodi huo ungetumiwa na Kampuni ya ABG hadi mwisho? Je, kwa hali ilivyo sasa mgodi huo unatakiwa kufungwa lini?
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa kwa Tanzania rasilimali madini ambayo hadi sasa imewekezwa na kuchimbwa na makampuni makubwa toka nje ni chini ya asilimia 5 ya rasilimali yote ya madini ambayo bado haijachimbwa. Hivyo basi, kwa mujibu wa taarifa ya Mtafiti wa masuala ya madini James Morrissey juu ya jinsi gani rasilimali zinavyoweza kuwa chachu ya maendeleo; kwamba ni lazima thamani kubwa ya rasilimali ibaki kwenye nchi husika kama mapato kwa Serikali. Jambo hili ni tofauti na hali halisi ilivyo kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kukosa rasilimali za kutosha kwa STAMICO kufanya kazi, imeilazimu STAMICO kuchukua migodi ambayo wahusika wamemaliza kuchimba au kiasi kikubwa cha rasilimali kimeondolewa na mabaki ndiyo STAMICO inapewa, kwa lugha rahisi ni kuwa STAMICO inakuwa kama fisi ambaye kazi yake ni kuvizia mifupa baada ya simba au chui kula minofu yote. Utaratibu huu unaliingizia Shirika letu hasara kubwa kwani mgodi unapofungwa, inawalazimu kuhakikisha eneo husika linatimiza masharti ya Kimazingira la kurudisha eneo hilo katika hali yake ya kiuhalisia.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri Serikali kuwa ili Tanzania inufaike na Raslimali zetu za madini, ni dhahiri kuwa hatuwezi kushindana na makampuni ya kimataifa kama vile Geita Gold Mine, AngloGold Ashanti, ACACIA, RESOLUTE, Anglo American, Anglo Platinum, De Beers, Empire Zinc Company, Energy Resources of Australia n.k. Ni ukweli kwamba kama mshindani wako umemshindwa basi inabidi uungane nae.
Hivyo basi, Mheshimiwa Spika, ni ushauri wa Kambi Rasmi kuwa STAMICO badala ya kulazimisha kuwa itakuwa ni kampuni ya taifa kuwekeza kwenye madini ni bora Serikali ifanye utaratibu wa kupata hisa kwenye makampuni hayo ya madini na sisi tuweze kuwa na uwakilishi kwenye bodi zao za uendeshaji pamoja na timu za utawala wa Kampuni hizo.
Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo ni dhahiri kama nchi mbali ya makampuni ya nje kuchimba madini ni dhahiri kile tulichokuwa tunakikosa kama nchi cha kuelewa ukweli wa kinachopatikana, tutakuwa katika hali ya uelewa wa nini kinaendelea katika uzalishaji na stahiki ya nchi itapatikana kama mikataba inavyosema.
SEKTA YA UZIDUAJI (EXTRACTIVE INDUSTRIES)
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2015 Bunge lako tukufu ilipitisha miswada mitatu ya sekta ya uziduaji (Extractive industries). Miswada hiyo ni Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2015 (The Tanzania Extractive Industries (Transparency and Accountability) Act 2015, Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi ya mwaka 2015. (The Oil and Gas Revenue Management Act 2015), Sheria ya Petroli ya mwaka 2015- (The Petroleum Act 2015).
Kwa utaratibu wa kawaida ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa sheria zinazopitishwa na bunge hili zinatekelezwa kwa haraka na kwa umahiri. Kambi ya upinzani ingependa kutaarifu bunge lako tukufu kuwa mwaka mmoja baada ya kupitishwa kwa sheria ya Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2015 (The Tanzania Extractive Industries (Transparency and Accountability) Act 2015, haijaanza kutekelezwa.
Hii inatokana na Wizara ya Nishati na Madini kuendeleleza urasimu, kung’ang’ania na kuhodhi madaraka iliyopewa Kamati tekelezi (TEITI Multi Stake Holder Group) kwa mujibu wa sheria hii. Kambi ya upinzani inaomba itoe mifano kuonyesha jinsi gani kucheleweshwa kwa sheria hii inahatarisha ukuaji na usimamizi wa sekta.
Kifungu namba 4 ya sheria hii inasema ifuatavyo:
There shall be a Committee to be known as the Tanzania Extractive Industries(Transparency and Accountability) Committee(2) The Committee shall be an independent Government entity which shall be an oversight body for promoting and enhancing transparency and accountability in the extractive industry.
Mheshimiwa Spika, Licha ya kipengele hiki kutambua nafasi ya kamati tekelezi (TEITI MSG) chini ya Jaji Mstaafu Mark Bomani,kwa ucheleweshaji huu imenyimwa fursa ya kusimamia na kuhakiki mapato ndani ya sekta hii. Kamati hii haina meno wala ujasiri wa kuwahakikishia Watanzania kuwa inathibiti vilivyo rasilimali zake.
Mheshimiwa Spika, Mwezi Septemba 2015 Tanzania ilifungiwa na bodi ya kimataifa inayosimamia uwazi katika sekta ya uziduaji(Extractive Industry Transparency Initiative). Kwa barua iliyoandikwa na Mwenyekiti Mhe Claire Short uamuzi huo ulichukuliwa baada ya Wizara ya Nishati na Madini kuchelewesha mchakato wa kupatikana kwa mkaguzi wa mahesabu kwa mahesabu ya 2012/13. Hii iliitia Tanzania aibu mbele ya jumuia ya kimataifa hasa kwa kuwa tumekuwa tukijitambulisha kuwa mfano wa uwazi na uwajibikaji. Tatizo la manunuzi litatuliwa tu kama kamati tekelezi (MSG) itapewa mamlaka kamili ya kusimamia manunuzi yake bila kuingiliwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, Kamati tekelezi (MSG) imeshindwa kuajiri ndani ya sekretariati yake, wataalamu wake wenyewe na kutegemea wafanyakazi toka serikalini. Utamaduni ya kutumia wafanyakazi toka Wizara ya Nishati na Madini inaifanya kamati hii kutoweza kuzisimamia serikali na makampuni ipasavyo.Hii pia inatokana na Kamati hii kunyimwa uhuru wa kusimamia rasilimali yao wenyewe hata zile zinazotokana na wafadhili kama EU,Benki ya Dunia na Canada. Kwa utaratibu ulioko kila kitu lazima lazima kiidhinishwe na Wizara ya Nishati na Madini ingawa fedha wanaziomba kamati tekelezi (TEITI MSG) kutoka kwa wafadhili.
Mheshimiwa Spika,Mwishoni mwa Machi 2015, Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT) iliitaka African Gold Mine (kwa sasa Acacia) kuilipa Serikali kodi ya Dola za Marekani 41.25 milioni (zaidi ya Sh89 bilioni), baada ya kugundua udanganyifu katika ulipaji wa kodi kwa miaka minne mfululizo.
Hata hivyo ripoti zilizochapishwa na kamati tekelezi (TEITI MSG) katika miaka yote hiyo hazigundua mapungufu hayo. Hii inaonyesha udhaifu mkubwa katika uendeshaji na usimamizi wa ukaguzi wa mahesabu ya sekta ya madini na mafuta. Ni maoni yetu kuwa hii ingeweza kuepukika ikiwa kutakuwa na wafanyakazi wenye weledi pamoja na rasilimali za kutosha.
Mheshimiwa Spika, Wakati taasisi nyingi za serikali zinakosa rasilimali fedha, kamati Tekelezi(TEITI MSG) ni chombo kinalalamikiwa na wafadhili kwa kurudisha kapuni fedha kwa kushindwa kuzitumia. Hii inatokana na kutoka wataalamu wa kutosha na uoga wa kufanya maamuzi ndani ya secretariat. Pia inatokana na urasimu wa kuidhinisha matumizi ndani ya Wizara ya Nishati na Madini.
Kwa mwaka 2015/16 pekee, Umoja wa Ulaya na Shirika la maendeleo Canada zilitoa takribani Euro 1,400,000. Nusu ya fedha hizi zinarudishwa kwa wafadhili bila maelezo ya kuridhisha, huku ikionyesha udhaifu mkubwa wa watendaji kutimiza wajibu wa kuimarisha kazi ya udhibiti wa mianya ya kupotea mapato ya serikali.
WAKALA WA JIOLOJIA TANZANIA (GST)
Mheshimiwa Spika, wakala wa Jiolojia Tanzania ulianzishwa chini ya sheria ya wakala wa Serikali Namba 30 ya mwaka 1997 (CAP 245) kupitia katika tangazo la Serikali Namba 418 la Desemba 09,2005, na kuzinduliwa rasmi mwaka Juni 23, 2006. Aidha, ni kwamba tangu enzi za Mkoloni kitengo cha maabara ya madini kilikuwepo na kilianzishwa rasmi mwaka 1925 na kilikuwa kinafanya kazi zake kikiwa hapa Dodoma na majukumu yake ya msingi hadi leo hayajabadilika sana bali yameboreshwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya wakala huyo ni pamoja na kukusanya, kuchambua, kutafsiri na kutunza takwimu na taarifa mbalimbali za jiosayansi, kutengeneza ramani mbalimbali za jiosanyansi zinazoainisha uwepo wa madini ya aina mbalimbali, kusambaza ramani, taarifa na takwimu kwa wadau ili ziweze kutumika kwa shughuli mbalimbali, kutoa ushauri wa kitaalam kwa wachimbaji madini wakubwa na wadogo na pia kwa kwa sekta ya ujenzi.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya utekelezaji ya Wakala kwa mwaka wa fedha unaomalizika wa 2015/16 unaonesha kuwa katika fedha zilizotengwa za matumizi mengineyo ya shilingi 4,433,482,000/- lakini hadi mwezi March, 2016 ni jumla ya shilingi bilioni 1 tu sawa na asilimia 22.55. Aidha, wakala haukutengewa fedha yoyote kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kwa mwaka wa fedha unaotarajiwa kuanza mwezi wa saba wakala unaomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi 4,417,444,000/- lakini kama ilivyokuwa mwaka jana haikutengwa hata shilingi moja kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kabisa kwamba Tanzania imebahatika kuwa na madini ya kila aina, hivyo basi ni jukumu la wakala huyu kufanya utafiti na kubaini kila eneo lina madini ya aina gani na kwa kiasi gani na matumizi ya madini hayo na ni njia gani inatakiwa kutumika katika uchimbaji wake. Kitendo cha Serikali kutokutoa fedha yoyote kwa ajili ya kupata vifaa vya kisasa vya kutafuta na kupimia sampuli za miamba au udongo kwa kulinga aina ya madini yanapopatikana ni kuifanya sekta ya madini kuendelea kuhodhiwa na wale wenye uwezo wa kifedha tu.
Mheshimiwa Spika, Kwani makampuni makubwa yanapata leseni ya kuchimba aina moja ya madini lakini ukweli ni kuwa katika mchakato wa kuchimba madini hayo, yanakuwemo madini mengine yanayoambatana na madini yaliyoombewa leseni, hivyo nchi ndiyo inapoteza na inakuwa ni faida kwa wenye leseni kwani wanachukua madini hayo bure kabisa. Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza kwamba Wakala huyu ili kazi yake iwe ya manufaa kwa Taifa na kwa jamii ni lazima apatiwe fedha za maendeleo ili rasilimali hizo ziweze kujulikana zilipo, na kiasi kilichopo na pia thamani yake ijulikane na hivyo mfanyabiashara apate stahili yake na Serikali ipate stahili yake.
Mheshimiwa Spika, kutokuwezeshwa kwa wakala huyu maana yake ni kwamba tutaendelea kuona kwamba rasilimali za madini tulizonazo hazitusaidii kama nchi.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati na Madini ina wajibu muhimu wa kusimamia maendeleo endelevu ya rasilimali za nishati na madini ili kuwezesha maendeleo ya nchi na kuboresha maisha ya wananchi. Hata hivyo mpaka sasa haijawezesha upatikanaji wa nishati kwa bei nafuu wala haijahakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za nishati na madini.
Mheshimiwa Spika, hali hii inahitaji mabadiliko makubwa ya kimfumo na kufungua ukurasa mpya kama taifa kuepusha laana ya rasilimali. Nyenzo mojawapo ya mabadiliko ya kimfumo ni katiba ya wananchi na si katiba inayopendekezwa. Katiba mpya itaweka misingi bora ya nchi na wananchi kunufaika na rasilimali badala ya sheria dhaifu, mikataba mibovu na mianya ya ufisadi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha,
…………………………
John John Mnyika (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-
Wizara ya Nishati na Madini
19.05.2016

No comments:

Post a Comment