Friday, April 15, 2016

UKAWA wasoma bajeti ya maendeleo Kinondoni, wananchi kutibiwa bure

VYAMA vinavyounda Umoja wa katiba ya wananchi, (Ukawa) kwa mara ya kwanza vimesoma bajeti yake huku wananchi wa manispaa hiyo wakipewa nafuu katika huduma za afya, na kipaumbele kikiwa ni elimu.

Kwa bajeti hiyo, sasa wananchi wa Manispaa hiyo watapewa kadi maalum itakayolipiwa Shilingi 40,000 kwa mwaka ili kuwawezesha kutibiwa bure katika hospitali za serikali.

Hayo yamebainishwa leo na Meya wa Manispaa ya Kinondoni Boniface Jacob, wakati alipokuwa akisoma bajeti ya mwaka 2016/2017 ya shilingi 248.47 billioni.

Akitoa mchanganuo wa fedha za bajeti hiyo Jacob, alisema, shilingi 64 billioni zinatokana na mapato ya ndani ya Manispaa, shilingi 182 billioni inatoka serikali Kuu, shilingi 1.4 billioni ni michango ya nguvu za wananchi na shilingi 12.2 bilioni inatokana na mapato ya mfuko wa barabara.

Kwa mujibu wa Jacob, bajeti hiyo imeelekezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu ambayo imetengwa shilingi 10 billioni kwa kutoa madawati 30,000 kila kata ambapo mahitaji ni madawati 28,000 kwa kila kata hivyo bajeti hiyo imepangwa kumaliza changamoto hiyo.

Jacob ameongeza kuwa bajeti hiyo itawezesha kuboresha miundombinu kwenye shule za msingi na sekondari ikiwa pamoja na kuhakikisha kila shule ya kata inakuwa na maabara.

Ameeleza kuwa katika kuhakikisha Manispaa inakuwa safi, kwenye bajeti hiyo imetengwa shilingi 2 billioni za kununua malori 25 ya taka ambapo kila kata itapewa moja na shilingi 400 milioni imetengwa kwa ajili ya kununua gari la maji taka na shilingi 1.2 billioni kwa ajili ya kununu gari mbili za kusaga taka.

Bajeti hiyo imetenga shilingi 1.6 bilioni kwa ajili ya kukarabati masoko.

Kwa upande wa miundombinu, bajeti hiyo imepanga kutengeneza barabara saba na kununua magreda yakayofanya ukarabati kwenye barabara za manispaa hiyo.

No comments:

Post a Comment