Tuesday, March 1, 2016

Mbowe amshitaki Magufuli kwa maaskofu

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amemshitaki Rais John Magufuli mbele ya maaskofu kadhaa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Mbowe amedai kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano imekuwa ikiwatimua watumishi mbalimbali wa umma bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza kupitia kampeni ya kupambana na ufisadi, inayotambulishwa kwa kaulimbiu ya ‘utumbuaji majipu’.

Akizungumza jana katika ibada maalumu ya shukrani kwa kumaliza uchaguzi mkuu salama, iliyofanyika kwenye Usharika wa Nshara wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT na kuhudhuriwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Frederick Shoo, na maaskofu wastaafu Dk. Erasto Kweka na Dk. Martin Shao, Mbowe alisema (wapinzani) hawaridhishwi na hatua ya serikali ya Rais Magufuli kuendeleza timuatimua na kuwasimamisha kazi watumishi wa umma 160 tangu aingie madarakani bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema wapinzani wako tayari kuipongeza serikali wakati wowote inapofanya mambo mazuri kwa manufaa ya taifa, lakini kwa sharti kwamba mara zote iwe inahakikisha sheria za nchi zinasimamiwa, mali na rasilimali za umma zinalindwa na kila kitu kinafanyika kwa kuzingatia taratibu zilizopo.

"Kutokana na hali ya sintofahamu kutamalaki katika taifa kwa sasa, hakuna mtumishi wa umma aliye na amani kutokana na mfumo unaoitwa kutumbua majipu. Tunasikia watumishi wa umma wakifukuzwa kazi bila kusikilizwa.

“Mpaka sasa kuna watumishi 160 wamefukuzwa na wengine kusimmishwa. Lakini pia zaidi ya taasisi na idara za serikali zipatazo 20 hazina uongozi…hii si sahihi,” alisema.

Katika ibada hiyo, Mbowe alikuwa ameongozana na wabunge 16 na makada wengine mbalimbali wa Chadema, alitoa sadaka ya Sh. milioni 279 kwa ajili ya kusaidia ukarabati na upanuzi wa jengo la Bethel lililoko Hai.

"Sisi tunamshukuru Mungu leo kwa kuwa tuko salama ndiyo maana tunatoa sadaka. Sadaka yetu tunaielekeza kwenye upanuzi na ukarabati wa jengo hili la Betheli la Usharika wa Nshara. Kwa hiyo, nawaomba sana viongozi wa dini na Watanzania kuliombea taifa kutokana na hali inayoendelea," alisema Mbowe.

Kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema wabunge 42 wa Chadema wamemuunga mkono kwa kuchangia kanisa hilo Sh. milioni 131.5; mwanasiasa mkongwe na mfanyabiashara, Philemon Ndesamburo alimchangia Sh. milioni 50; marafiki zake wa Arusha Sh. milioni 49.9; Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Edwin Mtei Sh. milioni mbili; makada wengine wa Chadema Sh. milioni 15 na Kamati ya Maandalizi Sh. milioni 41.

Katika hatua nyingine, Mbowe alitumia nafasi hiyo pia kuzungumzia mgogoro wa uchaguzi wa kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuitupia lawama CCM kwa madai kuwa ndio wanaokwamisha kwa maslahi yao.

Alisema jambo hilo pia linasikitisha kwa sababu sasa ni miezi minne imepita huku haki ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kuwa na Meya wao ikiendelea kuminywa kutokana na CCM kutoheshimu demokrasia na kutaka waendelee kuongoza licha ya wananchi kufanya uamuzi wao kupitia sanduku la kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Chadema na Chama cha Wananchi (CUF) vinavyoshirikiana kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ndivyo vyenye idadi kubwa ya madiwani kulinganisha na CCM, hivyo kwa mujibu wa Mbowe, CCM wamebaini kuwa hawawezi kushinda na sasa wanajitahidi kadri wawezavyo kukwamisha uchaguzi huo.

ASKOFU SHOO AZUNGUMZIA UTUNZAJI MAZINGIRA
Awali, akihubiri katika ibada hiyo, Askofu Dk. Shoo alielezea kusikitishwa kwake na uharibifu wa mazingira unaoendelea nchini.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya eneo la ardhi liko katika hatari ya kugeuka jangwa na dalili zake ni kuongezeka kwa joto duniani na mabadiliko ya tabia nchi.

"Bado hatujawa mawakili wema wa mazingira. Ukame, mafuriko, kupotea kwa rutuba na ubora wa ardhi na mabadiliko ya tabia nchi ni matokeo ya sheria za mazingira kutosimamiwa ipasavyo kukabiliana na hali hii. Sheria ziko nyingi, lakini hakuna utayari wa moja kwa moja wa kuwajibika katika kuzitekeleza," alisema Askofu Shoo.

Akifafanua Zaidi, kuhusu uharibifu huo, Dk. Shoo alisema zaidi ya hekta 400,000 za misitu huteketea kila mwaka, ndiyo maana kanisa limeamua kujikita katika kutoa elimu na kupiga kelele ili mamlaka zinazohusika zichukue hatua.

No comments:

Post a Comment