Tuesday, March 15, 2016

Lowassa analea amani ya nchi

KIMSINGI, kuna tofauti kubwa kati ya binadamu mmoja na mwingine kwenye mambo mengi. Hii ifahamike hivi, anaandika Adam Mwambapa.

Kama ilivyo kwangu na kwako, ndivyo ilivyompendeza Mwenyezi Mungu kwamba, binadamu tuwe sawa kwa mwonekano na maneno au pengine hata matendo; wakati kiundani ni tofauti kabisa.

Ni ukweli usiopingika nikisema, hata mapacha waliozaliwa siku moja na saa moja, isipokuwa kwa kupishana sekunde tu. Pia na wao hawako sawasawa kwa kila kitu.

Yule ni yule na huyu ni huyu. Waingereza wanatumia neno zuri sana, kuwakilisha utofauti wa kitu kimoja na kingine wakisema ‘unigue’.

Ndilo neno linaloonesha upekee wa mtu, na ndilo linaloleta tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine. Hata kama kimtazamo wako na mwonekano, vitu viwili utaviona ni kama viko sawa hivi.

Kwa Rais Dk. John Magufuli pia na kwa aliyekuwa mshindani wake wa jirani, katika mbio au kinyang’anyiro cha urais, kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Edward Lowassa; pia wana utofauti mkubwa na hawafanani.

Hata kama walikuwa na nguvu zinazokaribia kuwa sawa, wote wakitumia maneno ya kuleta mabadiliko, ingawa Magufuli aliiga, hawako sawa kwa mambomengi.

Lakini kuna tofauti ya ndani ambayo nguvu na mamlaka yao, kamwe haviwezi kuwa sawa. Kama nitakavyofafanua.

Kuna vitu vinajulikana zaidi kwa jina la ‘nafsi’ na kingine kinajulikana kwa jina la ‘nafasi’, asilani vitu hivi havifanani na vina maana tofauti pia. Ingawa, katika hali ya ubinadamu, wapo wanaovichanganya kwa kuvielezea maana yake iko sawa na vinafanana. Ukweli havifanani kabisa.

Wakati tafsiri nzuri ya ‘nafsi’ ni ‘hakika’. Tafsiri ya ‘nafasi’ ni ‘kujaaliwa’ au ‘Iliyojaaliwa/imejaaliwa. Kwa maana hiyo basi, ukiyachanganya, ukisema ‘nafsi nafasi’ maana yake ni ‘baraka’.

Na ukisema, ‘nafasi nafsi’ ni ‘neema’. Kwa maana ya kwamba, nafasi inachukua tafsiri ya neno lingine na kuwa eneo, wakati huo nafsi inaweza kuchukua tafsiri nyingine inayoweza kueleweka kama mtu.

Pengine niseme hivi, huenda nitaeleweka vizuri, katika kitu chochote ni lazima kuanze na vitu hivi viwili.

Ikiwa ilianza kuweko ‘nafasi’ kabla ya ‘nafsi’ kuwepo, basi nafasi ndicho kitu cha kwanza na ndipo nafsi hufuata baadaye. Vivyo hivyo, ikiwa kama nafsi ilianza kuweko mahali, basi nafasi ndiyo huja baada ya nafsi kuwepo.

Ni wachache sana wasiojua au kuelewa kuwa, kabla ya Dk. Magufuli kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya urais, Lowassa, tayari alikuwa kwenye eneo hilo.

Na alikuwa amechukua fomu na hivyo akatangulia kuwako na kuwa sehemu ya nafsi akiisubiri nafasi tu kupata alichokuwa akikihitaji; na baadaye ndipo akaingia Rais Magufuli kuchukua fomu.

Kilichofuata wengi wanafahamu fika kwamba, baadaye Lowassa aliingia kwenye mchujo mkali. Au wa kutopendwa na pengine kuhofiwa, na jina lake likafanyiwa figisu-figisu na kuondolewa.

Hali iliyompa nafasi Dk. Magufuli kuwa chaguo la Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuteuliwa kuipeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya urais, akiwabwaga wagombea wateuliwa wenzake.

Neema aliyoipata Dk. Magufuli, ndiyo naizungumzia kama ‘nafasi’ au ‘eneo’ kwa jinsi nilivyofafanua.

Ukilijua hilo, nakusihi ulijue na hili. Ni wachache sana mpaka hivi leo wanaoendelea kuamini wanapoiona amani ikiwa imetawala hapa nchini kiasi cha kutosha, wasijue imefikaje hapo ilipo na hata kudumu.

Wakati ilitazamiwa na ilishabashiriwa kuwepo na vita na machafuko mara baada tu ya uchaguzi mkuu kumalizika na kumpata rais.

Kwa wasioelewa au kama wanaelewa ila hawataki kuamini, amani hii imeletwa na kitu kinachoitwa ‘nafsi’. Ile iliyotangulia kuwako kabla ya kuja ‘nafasi’ iliyokuja baadaye.

Pamoja na kwamba nilisema kuwa, ‘nafasi’ na ‘nafsi’ havifanani, vinatofautiana na wala haviko sawa. Ila lazima vitu hivi viwili vishirikiane.

Kama ‘nafasi’ haiitaki ‘nafsi’ ni vigumu hali ya amani kupatikana na kuwepo eneo husika, muhimu ni kushirikiana na kuelewana kwa ukaribu kutokana na ule umuhimu wa utendaji wa kila kimojawapo.

Ili kuwepo au kuleta machafuko hapa nchini. Ni mpaka pale ‘nafsi’ itakapoanza kuona hakuna haja ya kuwapo na ‘nafasi’.

Au ‘nafasi’ itakapoona hakuna tena haja ya kushirikiana kwa lolote na ‘nafsi’, katika kuleta maendeleo na ufanisi wa pamoja. Likitokea hili ni hakika vita itatokea na machafuko kuibuka, jambo ambalo mpaka sasa naamini kuwa limeshikwa na ‘nafsi’ ambayo ingali inaheshimu uwepo wa ‘nafasi’.

Kwa tafsiri na maana hiyohiyo, nikimzungumzia Rais Magufuli, nasema kuwa ni mtu ambaye amepata nafasi ya urais kwa neema, nafasi ambayo haikuwa ya kwake.

Neema ilianza pale ambapo, yeye binafsi hakuwa na wazo la kuchukua fomu ya kutaka kugombea nafasi nyeti kama hiyo.

Nafasi ile, wapo waliotengewa na waliokusudiwa. Kwa ajabu ya wengi, majina yale ambayo kwa mujibu wa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mngeja; yalikuja yakiwa mfukoni mwa kiongozi mmojawapo aliyetaka watu wake wapewe nafasi.

Jambo ambalo wajumbe wengi walipingana nalo na lilileta mzozo mkubwa na hatimaye majina yale kukosa nafasi. Ndipo kwa nasibu, nafasi ikampata na kumwangukia rais wa sasa.

Kwa maelezo hayo, baraka za kiuongozi ni lazima na kwa vyovyote, zitaandamana au zitakuwa na ‘nafsi’.

Na ‘nafasi’ itabaki kuwa na neema tu na kwa kuendeleza utulivu na amani ni mpaka pale ambapo ‘nafasi’ itaona kuwa ni vyema kutenda au kushirikiana na ‘nafsi’ ili mambo yaweze kwenda na kusonga; nje ya hapo ni mambo kwenda kinyume na matarajio.

Ieleweke kuwa amani iliyopo na inayoendelea kuwepo hapa nchini, licha ya kwamba Mungu ndiye mleta amani na hali ya utulivu, lakini mara zote haji yeye ili watu tumshuhudie.

Daima hutumia watu tuliona nao na tunaoishi nao siku zote, na sasa amemtumia Lowassa kuleta amani kwa ile hali ya kukataa namna yoyote ya maandamano.

Kwa wale ambao pengine hawakukubaliana na uchaguzi ulivyokuwa na figis-figisu zozote zilizojitokeza wakati wote wa zoezi lile, pamoja na kwamba inadhaniwa serikali iliagiza magari mengi ya kivita, yakiwemo mengi ya kubeba maji ya washawasha.

Yote hayo hayana nafasi kwa wakati huu, maana hali ni shwari.

MwanaHalisi

No comments:

Post a Comment