Wednesday, February 3, 2016

Mbowe amweka Ndugai njiapanda.

Kivuli cha Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bunge, Freeman Mbowe, kimedaiwa kuwa moja ya sababu zinazofanya serikali ipunguze nguvu ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kutokana na kubaini kuwa alikuwa awe mwenyekiti wake.

Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bunge, Tundu Lissu, jana alisema ili Mbowe aweze kuwa mwenyekiti wa PAC ni lazima awe mjumbe wake, jambo ambalo limekuwa gumu baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kukataa kumpeleka huko.

Alisema Ndugai amefanya hivyo kwa madai kwamba amepokea amri kutoka mamlaka za juu asihamishe mjumbe yeyote wa Kamati za Bunge ambazo zimeshatangazwa.

“Mwanzo hatukufikiria kumpeleka Mbowe, lakini baada ya kuona kamati zilizochakachuliwa, moja ya 'possibilities' ni hiyo (kumpelekea kuongoza PAC) na ili aongoze lazima awe mjumbe (wa PAC) ila Ndugai anasema ameambiwa asimpeleke huko,” alisema Lissu.

Alisema endapo hawataafikiana na Spika na kufanya marekebisho ya wajumbe wa kamati kama wanavyotaka, kamwe hawatakuwa tayari kuongoza kamati hizo.

“Hili bunge litakuwa la kichekesho. Unasema hizi ni kamati za upinzani halafu unachagua nani ndiye aongoze, watuchagulie? Kwenye utararatibu wa Jumuiya ya Madola tunaojifanya tunafuata PAC inaongozwa na kiongozi wa upinzani.

"Ni kwa sababu huo ndio moyo wa serikali. Mapesa yote yako huko na lazima iendeshwe na mtu imara. Wameumia (serikali) sana kwa miaka 15 PAC na LAAC (Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa) zimewaumiza. Wanataka kuiua nguvu ya hizi kamati ili yabaki majina tu,” alisema Lissu.

Alisema wakifanya kile alichosema ndiyo serikali inataka watapeleka watu dhaifu na mambo mengi mabovu yatapita.

“Watakuja kusema mwenyekiti ni wa kwao, sisi tunasema tunataka mwenyekiti imara, Spika hawezi kutuchagulia viongozi dhaifu. Hizi kamati hazipaswi kuongozwa na watu dhaifu na hili limefanyika pia kwenye Kamati ya Katiba na Sheria, daktari wa binadamu amepelekwa huko na Lissu anapelekwa kupigania sheria za ushuru wa pombe za gongo, hatuwezi kukubali.

"Ukikubali umekwisha kabisa. Wasipokubali (kubadilisha wajumbe) hatutakubali uongozi tutaacha. Mimi mwenyewe sheria ndogo siendi, huko ni kupoteza muda. Nitaenda sheria na katiba na kushiriki mijadala, kura tu ndiyo sitopiga. Hoja yoyote ya kisheria ikiibuka bungeni nitaibuka na watashangaa,” alisema Lissu.

Mamlaka ya PAC kupelekwa PIC
Kuhusu Mamlaka ya PAC ya kusimamia mashirika ya umma na badala yake kupelekwa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), haitatekelezeka kwa sababu kanuni zinakataa.

“CAG anafanya uchunguzi wa hesabu za serikali kuu, serikali za mitaa na mashirika ya umma, akimaliza uchunguzi baada ya kupeleka kwa Rais analeta bungeni. Unapelekwa PAC na LAAC (Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa).

"CAG haripoti kwa Kamati ya Uwekezaji, anaripoti kwa PAC, Kamati ya PIC inapokea taarifa ya msajili wa hazina na taarifa za mwaka za mashirika ya umma, kama Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) na Tazara (Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia) na nyingine,” alisema na kuongeza:

“Taarifa ya CAG inakwenda PAC, huhitaji maneno ya (John) Joel (Naibu Katibu wa Bunge, anayeshughulikia masuaya ya Bunge). Unahitaji mambo ya kanuni na kuhoje je, CAG ataendelea kukagua taarifa za mashirika ya umma? Kama ndiyo taarifa zake zitaenda wapi? Kama unasema CAG hana tena mamlaka kukagua mashirika ya umma hapo sawa, akindelea kukagua atazipeleka PAC kwa sababu huko ndiko anaenda kuripoti.

"Wana mawazo kwamba kwenye mashirika ya umma kuna uchafu sana na huu uchafu umekuwa ukitumiwa na PAC kwa sababu ni ya upinzani na kwamba upinzani wamekuwa wakiutumia kuwapiga (serikali)."

AWAFAGILIA Zitto, DK.SLAA.
Lissu alisema Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, ni baadhi ya wabunge wenye weledi mkubwa ambao wamewahi kuongoza PAC na LAAC na kuiumiza serikali, jambo ambalo alisema sasa wanalikimbia.

“Tumekuwa na majadiliano na Spika na yeye amebanwa kweli kweli kwa sababu anaambiwa na mamlaka za juu hapana. Sisi hatuko tayari kwa kamati kama PAC na LAAC kuchaaguliwa mwenyekiti na CCM,” alisema.

Dk. Slaa na Zitto, alisema wanajua kuibua uchafu ndiyo maana kamati hizo zilipata heshima kwa sababu ya kuendeshwa na watu wenye weledi na watawala wanajua hilo. Alisema wamefanya hivyo ili wasipatikane tena watu wenye weledi wa aina ya Dk. Slaa na Zitto.

Kwa nyakati tofauti, Zitto aliongoza kamati ya Hesabu za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma (POAC), kabla ya kubadilishwa na kuwa PAC wakati Dk. Slaa aliongoza LAAC.

Juzi, Joel alisema ni kweli PIC wamepewa jukumu hilo hatua iliyochukuliwa kutokana na Kanuni za Bunge toleo la Januari 2016.

Alisema uamuzi wa kupeleka jukumu hilo PIC, umetokana na pendekezo la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), kutokana na PAC iliyopita kushindwa kutimiza majukumu iliyopewa.

“Ni kweli, kabla hujaniuliza fanya utafiti ujue ni kitu gani kilikuwa kinaendelea zamani. Ujue ni kwa nini PAC ilipewa hilo jukumu halafu uniambie PAC walilitekeleza jukumu walilopewa? Kuna majukumu walipewa na hawakutimiza,” alisema Joel.

Alipoulizwa majukumu ambayo hawakutimiza, Joel alisema “Hayo hayo ya kukagua mashirika na ndiyo maana CAG akashauri ianzishwe kamati nyingine.”

Alipofuatwa jana kutoa ufafanuzi wa hoja za Lissu, Joel alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu hatotenda haki kwao.

Zitto afunguka
Ziitto, aliyekuwa Mwenyekiti wa PAC kwenye Bunge la 10, alisema si kweli kwamba kuna jukumu walilopewa na kushindwa kulitimiza.

“Tulitimiza majukumu yetu yote, na ili tufanye kazi yetu kwa ufanisi, tuliigawa kamati, eneo moja likawa chini ya makamu mwenyekiti (Deo Filikunjombe- sasa marehemu) na moja chini yangu. Deo mashirika na mimi serikali.

“Hata hivyo kazi ilikuwa kubwa na muhimu kugawa PAC kuwa na PIC na PAC. PIC ya sasa haina mamlaka ya kushughulikia hesabu za mashirika ya umma kwa mujibu wa kanuni. Kamati za hesabu ni mbili tu, PAC na LAAC,’ alisema.

Aliongeza kuwa: “Iwapo Bunge linataka PIC ishughulike na hesabu za mashirika ya umma itabidi iitwe (Public Investment Accounts Committee) na itabidi iongozwe na mbunge wa upinzani na si kutoka CCM.

“Kanuni za Bunge za sasa hazielekezi PIC kushughulikia taarifa ya CAG kuhusu hesabu za mashirika ya umma. Pia kanuni haziipi PAC mamlaka hayo, kimsingi kikanuni hivi sasa hesabu za mashirika ya umma hazina kamati.”

Kwa mujibu wa Kanuni za kudumu za Bunge, toleo la Januri 2016, nyongeza ya nane sehemu ya nne, inasema kanuni za kudumu za Bunge zinazosimamia matumizi ya fedha za umma zitakuwa PAC na LAAC.

Nipashe ilimtafuta Mbowe kuzungumzia suala hilo, alipokea simu yake na kusema hayuko eneo zuri anatoka kanisani na akiwa vizuri atazungumza.

KURUGENZI IKULU
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, alipoulizwa kuhusu taarifa zinazodaiwa kuwa zimetoka juu, alisema Kurugenzi yake haina taarifa yoyote kama Rais John Magufuli alitoa amri ya kutorudiwa upangaji wa wajumbe wa kamati za Bunge.


CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment