Thursday, January 28, 2016

Msimamo wa Ukawa, baada ya kutolewa na mbwa bungeni

VIONGOZI wa Vyama Vinavyounda Umoja wa Katiba (Ukawa), wakiongozana na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), walieleza kwamba kamwe hawataacha serikali iendelee kupoka haki ya kikatiba ya wananchi, kwa kuwazuia kutoa na kupata habari. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Viongozi hao waliwanyooshea vidole wabunge wa CCM kwamba ni wanafiki, kwa sababu wakati wao (wapinzani) wakijadiliana na Kamati ya Uongozi wa Bunge, walikuwa wakipokea ‘vimemo’ wakiwaomba waendelee kupambana kwa sababu hata wao hawapendi yanayoendelea kufanywa.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe, amesema wanalaani udharirishwaji waliofanyiwa wabunge wa upinzani bungeni, kwa kutumia askari wenye silaha mbalimbali na mbwa, kwamba ni ukiukwaji wa haki za bunge.

Amesema sababu zilizotolewa na serikali kuzuia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kurusha moja kwa moja matukio ya bungeni hazina mashiko na kwamba wamebaini mambo matano yanayoipa kiwewe mpaka kufikia hatua hiyo.

Hata hivyo amesema hawajasusia vikao vya bunge, leo wataendelea kushiriki shughuli za bunge kama kawaida lakini wakiendelea kudai haki za kikanuni na kikatiba kuzingatiwa, kwa maslahi ya watanzania wote.

Ametaja mambo hayo kuwa ni mjadala kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar, kasoro zilizojitokeza katika Uchaguzi Mkuu uliyomalizika Mwaka 2015, maamuzi yanayochukuliwa na baadhi ya viongozi wa serikali ya awamu ya tano, bila kuzingatia sheria, taratibu na kanuni mbalimbali kwa kisingizio cha ‘kutumbua majipu’.

Kiongozi mwingine wa Ukawa, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) amesema wabunge wengi kwa sasa wanaofanya siasa za kizazi kipya, hawatakubali kurudishwa enzi za ‘zidumu fikra za mwenyekiti’.

“Tuko tayari kuuawa sote lakini ifahamike hilo likitokea, wengine wataendelea kujitokeza kuendeleza madai mpaka haki itakapopatikana,” alieleza Mbatia.

No comments:

Post a Comment