Wednesday, October 14, 2015

TAMKO KUHUSU UTEKWAJI NYARA WA MGOMBEA MBUNGE JIMBO LA MTWARA MJINI KUPITIA CHADEMA Ndugu JOEL ARTHUR NANAUKA


Ndugu wanahabari, wananchi wa jimbo la Mtwara Mjini na watanzania kwa ujumla: ninaitwa Raymond Mwakasitu. Ni mwanasheria na mshauri wa Ndugu Joel Arthur Nanauka ambaye ni Mgombea ubunge Jimbo la Mtwara Mjini kupitia CHADEMA. Nimeamua kutoa tamko rasmi kwa niaba ya mteja wangu, ambaye siku chache zilizopita alipatwa na tukio la kinyama, baya, na la udhalilishaji wa utu wake.
Utangulizi
Naomba nianze tamko langu kwa utangulizi mfupi juu ya kilichotokea bila kuingilia taratibu za kiuchunguzi ambazo ninaamini zinaendelea chini ya Jeshi la Polisi. Mteja wangu, Ndugu Nanauka, alipatwa na tukio ambalo kwa mazingira ya kutokea kwake, maelezo yake, na hali aliyokutwa nayo, tunaamini kwamba alitekwa kwa lengo ya kuutishia maisha na uhai wake. Ndugu Nanauka alitekwa nyara siku ya tarehe 5/10/2015, kuteswa, na  kutelekezwa baada ya masaa kama 36 na watu wasiojulikana.

Siku ya tukio, mteja wangu, baada ya shughuli za kampeni, alielekea nyumbani majira ya saa kumi na mbili jioni kwa ajili ya mapumziko. Majira ya saa kumi na mbili na nusu, Ndugu Nanauka aliaga kwa meneja wake wa kampeni (Bi Anna Deo), kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu (SMS), akimtaarifu kwamba anakwenda kuonana na mtu ambaye amekua akihitaji kuonana nae kwa muda wa kama wiki mbili hivi bila mafanikio kutokana na ugumu wa ratiba zake.
Hata hivyo, masaa yalizidi kwenda pasipo mteja wangu kurudi nyumbani jambo lililoleta mashaka na hivyo kutaka kujua kulikoni. Alipotafutwa kwa njia ya simu yake ya mkononi haikua inapatikana hewani na hiki kikaleta mashaka zaidi. Meneja wake wa kampeni alinitaarifu kuhusu kutoonekana kwake majira ya kuelekea saa nne usiku. Taratibu za kisheria zinahitaji taarifa zitolewe kituo cha Polisi yanapokua yamepita masaa 24 tangu mtu inayehisiwa kapotea, alipoonekana kwa mara ya mwisho. Hivyo basi, nilishauri waendelee kuvuta subira kidogo kabla ya kutoa taarifa. Hata hivyo, kwa kutambua nafasi ya mteja wangu kama mgombea ubunge na ukweli kwamba hakua  na kawaida ya kutoka nyumbani usiku au kwenda mahali bila taarifa, niliwashauri waende kutoa taarifa kituo cha polisi ilipofika majira ya saa sita usiku. Mteja wangu amekua akizingatia tahadhari zote za kiusalama hivyo asingeweza kwenda mahali pasipo taarifa sahihi, tena akiwa mwenyewe, na simu yake ikiwa imezimwa.
Mteja wangu alitafutwa usiku ule wa Jumatatu ya tarehe 5 na siku iliyofuata bila mafanikio. Siku ya Jumatano tarehe 7/10/2015 majira ya saa kumi na mbili asubuhi  alipatikana akiwa ametelekezwa kwenye kituo cha afya kiitwacho Bursa Clinic pale Mtwara mjini. Ndugu Nanauka alikua taabani, hajitambui, amechafuka, shati lake limechanika na akiwa hana nguvu kabisa. Alipatiwa huduma ya kwanza kwenye kituo hicho na baadaye kuhamishiwa hospitali ya mkoa ya Ligula. Kutokana na hali aliyokua nayo, na ukweli kwamba usalama wa afya yake haukufahamika, ilionekana ni vema akapatiwa matibabu na vipimo vya hali ya juu zaidi ili kunusuru maisha yake. Hivyo basi, alihamishiwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipopetibia kwa siku kadhaa. Tukio hili ni la kinyama, la kudhalilisha na limeleta masikitiko na hamaki kubwa kwa ndugu za mteja wangu na wana mtwara kwa ujumla wao.

Hali iliyokuwepo kabla ya Kutekwa kwa Ndugu Nanauka
Siku chache kabla ya tukio nililolieleza hapo juu, mteja wangu, familia yake, na hata baadhi ya watu walio katika timu yake ya kampeni, walipata vitisho vilivyoonesha kwamba kuna njama zilizokua zinafanywa dhidi yake. Kwa mfano, watu kadhaa walio karibu na mteja wangu walipokea simu za vitisho dhidi ya uhai wao. Pia walitishwa kwamba mali zao zingeharibiwa. Mzazi wa mteja wangu (Mzee Nanauka) alitishiwa kwamba nyumba yake  ingechomwa moto.

Kama vile haitoshi, nakumbuka siku ya tarehe 3 meneja wa kampeni za Joel (Bi Anna Deo) alinitaarifu kwamba alipokea simu ya vitisho toka kwa mtu aliyemtaja kwa jina na nilimshauri atoe taarifa kituo cha polisi. Bi Anna alitoa taarifa na upelelezi ulifanyika na mhusika huyo alikamatwa na jeshi la Polisi. Nimeeleza haya yote ili tuone picha halisi ya tukio zima lililompata mteja wangu. Mazingira haya yanaonesha kila dalili kwamba alitekwa nyara kama mwendelezo wa mfululizo wa vitisho alivyokua kavipata dhidi ya usalama wake.

Mwenendo wa Uchunguzi wa tukio
Nimekua nikifuatilia mwenendo na taarifa ya upelelzi/uchunguzi wa tukio zima ili nikiamini kwamba wale waliohusika na unyama na udhalilishaji huu wanafikishwa mbele za haki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.  Taarifa za mwanzo zilizotolewa na jeshi la polisi, akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Henry Mwaibambe, zimenukiliwa zikisema polisi wanachunguza tukio ili kubaini kama kuna ukweli. Kauli za polisi zinaoenesha kwamba tayari wana mashaka na uhalisia wa tukio la kutekwa kwa Ndugu Nanauka kutokana na maelezo kwamba kumekuwepo na tetesi zinazoonyesha huenda tukio hilo lilipangwa kutokana na mazingira ya kutoweka kwake hadi kupatikana akiwa katelekezwa kituo cha afya.

Nikiwa kama mwanasheria, maelezo haya ya jeshi la polisi yamenishangaza kwani nilitegemea polisi wafanye kazi yao kikamilifu na kuthibitisha kilichotokea badala ya kuanza kueleza hisia na tetesi za tukio. Uhai na usalama wa Ndugu Nanauka (kama ilivyo kwa mtanzania yoyote yule) ni jambo la kupewa uzito na umuhimu unaostahili. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (ibara ya 14) inaweka wazi kwamba, “kila mtu ana haki ya kuishi na kupata kwa jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria”.
Maelezo ya polisi na kile ambacho kimeandikwa baadhi ya vyombo na mitandao ya kijamii, yanatoa picha kwamba mteja wangu anahusika na kutekwa kwake. Jambo hili limeibua maswali mengi kwa wananchi wa Mtwara na umma kwa ujumla kujiuliza inawezekanaje mtu akafanya njama za kutekwa kwake na kufanyiwa unyama kuhatarisha maisha yake. Ninasikitika kwamba taarifa hii ya awali ya jeshi la Polisi, imepelekea watu wengi kuamini kwamba mteja wangu hakutekwa bali kafanya ujanja wa  kujiteka ili kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
Kama vile haitoshi, baadhi ya vyombo vya habari vimekua vikiripoti tukio hili kwa mwelekeo huohuo ambao ni wa kupotosha na kudhalilisha huku ukisababisha maumivu ya kihisia kwa mteja wangu, familia yake na wananchi walioguswa na tukio hili. Vyombo vya habari vinapotoa taarifa yenye kuleta maswali au inayoonyesha kuegemea upande mmoja (hasa kwa tukio lenye utata kama hili), kuna uwezekano mkubwa wa kuleta machafuko au migongano isiyo ya lazima katika jamii hasa kipindi hiki cha kulekea uchaguzi mkuu ambapo kuna hali ya taharuki (tension) katika jamii. Taarifa hizi zenye kuonesha mkanganyiko wa tukio zinatolewa na jeshi la polisi na vyombo vya habari, bila kuzingatia kwamba mteja wangu na walio karibu naye, walishapata vitisho dhidi ya usalama wao na taarifa zilishatolewa polisi na kupelekea mmoja wa wahusika kukamatwa. Nilitegemea msingi huo wa taarifa za awali, utumike kuharakisha na kurahisisha uchunguzi wa tukio hili badala ya kuanza kulielezea kwa hisia kwamba hakuna ukweli katika tunachoamini kilichompta mteja wangu.  

Tukio la Kutekwa na Uhusiano wake na Uchaguzi:
Siku moja baada ya Ndugu Nanauka kupatikana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara alinukuliwa kupitia taarifa ya habari ya saa mbili usiku katika kituo cha ITV akisema kwamba, kuna utata katika tukio lililompata mteja wangu. Katika maelezo yake, alisema kwamba, kuna maelezo kwamba mteja wangu alishatangaza kujitoa kugombea ubunge Mtwara. Kama vile haitoshi, alisema kwamba mteja wangu, alitangaza kumuunga mkono mgombea wa CUF siku mgombea wa urais kupitia UKAWA (Mh Lowasa) aliopofika Mtwara. Maelezo haya yanashangaza na yanaibua maswali:
 • Nani aliyemtaarifu kamanda wa polisi kwamba mteja wangu alisema anamuunga mkono mgombea wa CUF?
 • Pili, Na kama aliambiwa, alitafuta uthibitisho wa alichoambiwa?
 • Tatu, hata kama mteja wangu alitangaza hivyo au la, hicho kinausikaje na usalama wake na uchunguzi wa kutafuta ukweli kuhusu kilichompata?

Ukweli ni upi?
 • Jimbo la Mtwara Mjini kama yalivyo baadhi ya majimbo mengine Tanzania bara, umoja wa vyama vinavyounda UKAWA, vilishindwa kuafikiana ni chama gani shiriki kisimamishe  mgombea kutokana na sababu kadha wa kadha. Hivyo, hadi mteja wangu anapatwa na tukio la kutekwa, vyama vya CUF, NCCR na CHADEMA vilikua na wagombea katika jimbo hili tofauti na maeneo mengine ambapo wamesimamisha mgombea mmoja.
 • Hata hivyo mteja wangu, tofauti na wagombea wenzake, na kwa kuheshimu makubaliano ya vyama husika, na kwa kuelewa kwamba viongozi wa juu wa UKAWA walikua bado wanaendelea na mazungumzo ya kutafuta muafaka; hajawahi kufanya kampeni kama mbunge na badala yake amekua akiwasaidia kampeni wagombea wa udiwani katika jimbo hilo.
 • Baada ya kuona muda unasogea sana bila muafaka na ukweli kwamba uchaguzi unakaribi sana; ukichanganya na hali ya kisiasa ilivyokua na kwa kauli zisizo na staha za wagombea wenzake, hakutamani kuona umoja wao unashindwa katika jimbo hili kwa kukosa muafaka. Kwa nia njema kabisa, aliamua kutangaza kujitoa kwenye kinyang'anyiro hicho ili kunusuru UKAWA. Hii ilikua ni siku kama nne kabla ya kutekwa kwake.
 • Hata hivyo, chama chake (CHADEMA) kupitia viongozi wake wa Mtwara na kwa maagizo ya uongozi wa Taifa, baada ya kauli yake, kilimtaka kuendelea na kampeni kwani walikubaliana na wenzao kwamba majimbo waliyokosa muafaka kila chama kiendelee kusimamisha mgombea wake. Hivyo hakua na sababu ya kujitoa. Pia wananchi wengi wa Mtwara walionesha kutokukubaliana naye na walinukuliwa kwenye vyombo vya habari wakilalamika na kumtaka arudi wenye uchaguzi kwani wao ndio watakaofanya maamuzi.
 • Siku mteja wangu alipotekwa, ndio siku alikokua amerudi rasmi kwenye kampeni kama alivyoagizwa na chama chake na kwa kutii matakwa ya wananchi wa Mtwara.
 • Siku ambayo mgombea Urais wa UKAWA alipofika Mtwara, kulikua na mikutano ya ndani kati ya wagombea wote watatu pamoja na viongozi wa UKAWA waliotoka makao makuu kutafuta mwafaka. Hata hivyo, mwafaka haukupatikana na mgombea Urais hakutoa kauli ya mwisho ya nani ni mgombea ubunge wa Mtwara bali aliwaita jukwaani wagombea wote watatu. Mteja wangu hakutangaza katika kikao cha ndani wala katika mkutano wa kampeni kwamba anamuunga mgombea mwingine mkono. Alichokisema na ambacho amekua akikisema siku zote kabla hata ya kuchukua fomu ni kwamba, yeye atakua tayari kumuunga mkono mgombea yeyote atakayeteuliwa na UKAWA iwapo haitakua ni yeye. Kauli iliyotolewa na polisi kwamba alitangaza kumuunga mkono mgombea mwenzake wa CUF siku Mh Lowasa alipokwenda Mtwara, sio ya kweli na ni ya upotoshaji. Tunajiuliza, nini malengo ya kauli hii katika mazingira ya kutekwa kwa mteja wangu?

Hivyo basi, nawasihi Jeshi la Polisi Mtwara, kuchukulia tukio la kutekwa mteja wangu kwa umuhimu na uzito wake na lione wajibu wa kufuatilia na kuchunguza kwa umakini mkubwa ili kupata ukweli. Jeshi la polisi zichukulie taarifa zozote zinazoashiria kutokuwepo kwa usalama wa raia, akiwemo mteja wangu. Mteja wangu, akiwa kama mgombea ubunge, anastahili kupatiwa ulinzi dhidi ya chochote kile kinachohatarisha maisha na uhuru wake. Kitendo alichofanyiwa, kimepelekea mteja wangu kujiona hayupo salama na hivyo kumuweka katika wakati mgumu kisiasa na hata maisha yake ya kawaida kama raia mwema wa nchi yake.

Ukweli ni kwamba, Ndugu Nanauka hakujiteka bali alitekwa na watu waliokua na dhamira ovu dhidi yake.  Walilenga kumwathiri, kumwondolea ujasiri na kumpotezea imani kwa wapiga kura wa Mtwara ili aonekane ni kiongozi asiyeaminika. Taarifa nyingine yoyote ile, ina lengo la kupotosha ukweli wa tukio hili na kulifanya lionekane halina uzito, ni la kizushi na kupuuzwa. Jambo hili lina lengo la kushusha hadhi na heshima yake katika jamii kama kiongozi wa kisiasa. Kwa wanaomfahamu mteja wangu, wanatambua kwamba ni mtu mwaminifu na mwadilifu katika jamii. Amefanya kazi nyingi na amekua kiongozi maeneo mengi kwa uaminifu mkubwa usiotiliwa shaka. Hana haja yoyote ya kujitengenezea tukio la kutekwa ili kujiongezea umaarufu wa kisiasa au kutafuta huruma ya mtu yeyote yule. Pamoja na mambo mengine,mteja wangu, kupitia taasisi yake, amesaidia kusomesha vijana wa Mtwara zaidi ya mia tatu tangu mwaka 2008. Uongozi anaoutafuta kama mbunge, una lengo la kuendeleza dhamira na nia yake njema ya kuwatumikia wananchi wa Mtwara na watanzania kwa ujumla wao, na sio vinginevyo.
Hitimisho:
 • Kama mwanasheria wa Ndugu Nanauka, ninalaani vikali kitendo alichofanyiwa mteja wangu na ninawasihi Jeshi la polisi litimize wajibu wao na kuwachukulia hatua wahusika. Hali kadhalika, ninaliomba jeshi la polisi Mtwara, litoe taarifa kamili na ya kueleweka kuhusyu mteja wangu na kuuambia umma nini kilitokea.
 • Pili, ninalaani vikali taarifa zozote zinazosambazwa juu ya mteja wangu kwamba alipanga kutekwa kwake kwa sababu za kisiasa. Wanaosambaza habari hizi, ni watu wasio na huruma wala utu kwa kushindwa kuthamini usalama na uhai wa mteja wangu
 • Kwa kua afya ya mteja wangu inazidi kuimarika, ni matarajio yangu kwamba ataendelea na kampeni za ubunge siku chache zijazo kama atakavyoshauriwa na watabibu. Hivyo niwatoe hofu na shaka wananchi wa Mtwara Mjini juu ya ushiriki wake katika uchaguzi. Mgombea wao bado anashiriki uchaguzi huu na ataendelea na kampeni hadi dakika ya mwisho. Ikimpendeza Mungu, atashinda na atawaongoza katika kujiletea maendeleo ya jimbo lao.

Kwa niaba ya mteja wangu, familia yake, na wananchi wenye mapenzi mema, tunamshukuru Mungu kwamba hali ya afya ya Ndugu Nanauka inaendelea vema, imeimarika na Mungu ameuhifadhi uhali wake ambao ni wazi ulikua kwenye hatari ya kupotea. Ninawashukuru wote waliompa msaada wa hali na mali pamoja na watabibu waliomsaidia kwa utaaalamu wao kuhakikisha anapona.

Mungu awabariki

Raymond Mwakasitu   
Mshauri na Mwanasheria wa Ndugu Joel Nanauka

Tarehe 13/ 10/ 2015

No comments:

Post a Comment