Thursday, October 15, 2015

SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZA MSIBA WA DK. ABDALLA KIGODA


CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO 

(CHADEMA)



SALAMU ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA DK. ABDALLA KIGODA

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kwa masikitiko na majonzi makubwa ametuma salaam za rambirambi na pole kwa familia, Rais wa Nchi na Mwenyekiti wa CCM na wananchi wa Jimbo la Handeni, kufutia kifo cha aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdalla Kigoda.

Katika salaam hizo Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa kifo cha Dk. Kigoda kimeacha pengo kwa serikali na chama chake kwa sababu alikuwa ni kiongozi msomi na mzoefu hivyo kuwa sehemu ya watu wengine kuendelea kujifunza.

“Dkt. Kigoda atakumbukwa kwa namna ambavyo akiwa mmoja wa mawaziri wa wapya katika serikali ya awamu ya tatu ya Rais Mkapa baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 alisimamia masuala ya ubinafsishaji na hatimaye kuibuka kwa sekta binafsi nchini.

“Kigoda atakumbukwa kwa namna alivyokuwa akitumia uwezo wake wa kitaaluma katika nafasi alizoshika serikali na bungeni, mathalani akiwa Waziri wa Viwanda na Biashara na wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Fedha na Uchumi,” amesema Mbowe.

“Kwa masikitiko na majonzi makubwa natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki kwa kuondokewa na mpendwa wao, kiongozi katika maisha. Mwenyezi Mungu awatie nguvu katika wakati huu wa majonzi ya msiba huo mkubwa.

“Kwa niaba ya CHADEMA, pia natoa salaam za rambirambi na pole kwa Rais Jakaya Kikwete akiwa kama kiongozi mkuu wa serikali ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kwa kuondokewa na msaidizi wake serikalini na mgombea ubunge wa chama hicho, Jimbo la Handeni.

Aidha, Mwenyekiti Mbowe pia ametoa pole kwa wananchi wa Jimbo la Handeni kwa kuondokewa na aliyekuwa mbunge wao kwa muda mrefu kuanzia mwaka 1995 hadi 2015 ambapo alikuwa ameteuliwa na chama chake kugombea nafasi hiyo kwa mara nyingine tena.

Chama kupitia ofisi ya Katibu Mkuu, kitashiriki mazishi ya marehemu Dkt. Kigoda

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema.


Imetolewa leo Oktoba 14, 2015 na;
Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments:

Post a Comment