Monday, July 13, 2015

Zitto amemtuma ofisa wake kuisemea CHADEMA kuhusu Lowassa!

Ofisa mmoja wa chama kiitwacho ACT ambaye mara kadhaa amenukuliwa akiwa ni msemaji wa chama hicho ameandika na kueneza habari mtandaoni kuwa kada mwandamizi wa CCM Edward Lowassa anahamia CHADEMA!

Inashangaza kidogo! Ama ni kwamba wahusika wa chama hicho hawana uratibu wa mawasiliano kiasi kwamba kila mtu anaweza kujiandikia tu au wanaendelea kukubuhu katika siasa nyepesi.

Itakumbukwa juzi mara baada tu ya majina 5 ya makada wa CCM yaliyokuwa yamepitishwa kwenye CC ya chama hicho kuwa yamejulikana (kwa kadri ya utaratibu wao) Kiongozi Mkuu wa ACT Zitto haraka haraka kama ilivyo kawaida yake akakimbilia mtandaoni kuandika kuwa Edward Lowassa anajiunga na ACT na atakabidhiwa kadi.

Wafuasi wa Zitto kwa kuendekeza siasa nyepesi za umaarufu wa mtu, wakakimbilia nao mitandaoni kusema kuwa tayari Lowassa ameshajiunga na ACT na kwamba ni Mgombea urais na 'taswira na nuru' ya chama tayari kapewa cheo cha Uwaziri Mkuu, alas!

Hawakuishia hapo. Wakaenda mbali hata kughushi nembo ya moja ya mashirika makubwa ya habari duniani kisha wakaandika mambo yanayokidhi matamanio yao, kwamba Lowassa kahamia ACT na Zitto kamkabidhi kadi.

Sasa haijajulikana hiyo kauli ya Zitto imeishia wapi ndani ya masaa 48 tu ghafla ofisa wake amekwenda mitandaoni akijigeuza kuwa msemaji wa taasisi isiyomhusu kuwa Lowassa amehamia CHADEMA.

Tumsaidie Zitto asiendelee kufanya siasa nyepesi. Alikuwa mtu wa kwanza kumkaribisha Lowassa kwenye chama chake mapema kabla hata hajachukua fomu ndani ya CCM. Sasa awaambie watu wake vizuri hilo 'deal' limeishia wapi?

Taarifa kutoka vyanzo vyangu zinasema kuwa Lowassa atafanya mkutano na waandishi wa habari kesho saa 3 huko Dodoma. Atakachozungumza anakijua vizuri yeye labda na watu wake pia.

Habari hizo kwamba Lowassa amehamia CHADEMA hazina ukweli wowote. Zinatengezwa na kupikwa na hao 'vijana' kwa maslahi wanayoyajua wao.

Kwa kushirikiana na vyama washirika wenza katika UKAWA, tunaendelea na maandalizi ya kwenda kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kushika dola na kuongoza serikali kuwatumikia Watanzania. Kila kitu kinakwenda sawa. Maandalizi karibu yote yamekamilika...ni #UKAWAJulai 14.

Hilo ndilo suala la msingi kwa sasa. Baada ya giza totoro la siasa za ghiliba, rushwa na hila huko Dodoma kwa takriban mwezi mzima, wananchi wanasubiri nuru ionekane Julai 14 kupitia UKAWA. Yamebakia masaa mchache kuuona mwanga unaosubiriwa na Watanzania wote wapenda mabadiliko ya kimfumo na kiutawala, si mabadiliko ya majina na sura za watu kutoka mfumo ule ule uliotukwamisha hapa tulipo.

Makene

1 comment:

  1. naiamini chadema kwa kweli ipo vizuri timu sasa imetimia kuingia kwa lowasa ndio mmemaliza kazi kabisa. ikulu lazima mwaka huu

    ReplyDelete