Wednesday, July 1, 2015

MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MASOKO YA BIDHAA YA MWAKA 2015 (COMMODITY EXCHANGE ACT,2015)

(Yanatolewa chini ya Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Bunge, toleo la mwaka 2013)
1.   UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, muswada huu ulio mbele yetu kwa malengo yake kama utasimamiwa vyema ni mzuri kwani utaboresha mifumo ya mauzo ya  mazao ya kilimo na bidhaa zingine kwa kadri mahitaji ya nguvu za soko yatakavyopelekea.  Katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara ya mwaka 2014/15 alieleza dhamira na uhitaji wa kuwepo kwa mfumo huu wa soko la bidhaa. Kwani alieleza uwepo wa kitu kinachoitwa COWABAMA -  
(Collective Warehouse Marketing Systems) na kueleza kuwa huo ni mwendelezo wa kuanzisha Soko la Mazao na Bidhaa (Commodity Exchange Market).

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haina pingamizi na muswada huu wa Sheria ya Commodity Exchange  kwani hili lilikuwa ni hitaji la wadau ambao wanashiriki katika mfumo mzima wa Stakabadhi za mazao Ghalani. Tunaamini kwa kiasi kikubwa wahusika katika mfumo huu wameshirikishwa kwa hatua zote za uandaaji wa muswada huu.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge lako ikiwa imefanya jitihada zozote za kuhakikisha kuwa elimu kwa umma hasa kwa wadau wote wa mfumo wa masoko ya bidhaa inatolewa.  Sheria nyingi zinazoletwa katika Bunge hili zimekua zikilalamikiwa kutowafikia walengwa na hivyo utekelezaji wake siku zote umekua ukileta migogoro isiyoisha na mwishowe kusababisha hasara si tu kwa wazalishaji bali pia kwa watumiaji wa mwisho. Ni mikakati gani imewekwa ili kuhakikisha kuna utoaji elimu endelevu katika masuala ya masoko ya bidhaa?
Mheshimiwa Spika, hali ya miundombnu nchini hasa usafiri wa barabara na reli ambao ndio tegemezi kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa hasa za kilimo ni mbaya na isiyoridhisha. Sote ni mashahidi kuwa , pamoja na Serikali kujisifu kwa kuweka mtandao mkubwa wa barabara lakini barabara hizi hazijajengwa kwa ubora na ziinaleta changamoto kubwa za usafirishaji wa bidhaa hasa kipindi cha mvua. Leo tunapotaka kupitisha muswada huu wa masoko ya bidhaa, ni kwa kiasi gani tumeandaa mikakati ya kuimarisha miundombinu ili wauzaji na wanunuzi wa bidhaa wasipate hasara? ikiwa tutaendelea kuwa na miundombinu mibovu kama ilivyo sasa, ni dhahiri kuwa hata utekelezaji wa Sheria hii utakua mgumu na hivyo kuwa na Sheria bubu isiyoendana na mahitaji ya masoko ya bidhaa na hivyo kudidimiza uchumi badala ya kuinua uchumi .

Inaendelea.....



Mheshimiwa Spika, maendeleo ya teknolojia katika masoko ya bidhaa ni mojawapo ya sababu zitakazoweza kufanikisha ama kufelisha utekelezaji wa Sheria hii. Ni kwa kiasi gani Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na ukuaji wa teknolojia utakaomwezesha mtumiaji wa masoko ya Bidhaa ya Tanzania kuendana na mtumiaji wa masoko ya bidhaa mahali pengine duniani?

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuletwa kwa Sheria hii katika Bunge lako, ni dhahiri kuwa ili sheria hii iweze kutekelezwa kwa kiwango kinachotakikana, kanuni na miongozo yake ni lazima iwepo. Ikiwa Sheria hii italetwa na kanuni zitachelewa kutungwa, basi utekelezaji wake hautakua na maana yoyote na hivyo kuchangia kwa migogoro na migongano ya kisheria

2.   MAPITIO YA MUSWADA

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 5 cha muswada kinachohusu malengo ya mdhibiti yanayohusiana na masoko ya bidhaa. Kambi Rasmi inapenda kupata taarifa ya kina kwani Mdhibiti ambaye ni CMSA yeye hana bidhaa bali bidhaa zinazotakiwa kuingia katika soko ambalo liko chini yake ziko chini ya mamlaka zingine ambazo zimeanzishwa kisheria na zinazo kanuni zake za uendeshaji; mamlaka hizo ni kama vile bodi ya Korosho, Bodi ya Kahawa, Bodi ya nafaka na  Mazao mchanganyiko: Hivyo basi  kwa kuangalia majukumu ya mdhibiti katika sheria hii ni dhahiri kuwa taasisi hizo hazitakuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria zilizozianzisha.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi inaungana na wadau ambao wameliona tatizo hizo la kuziweka pembeni mamlaka na wakala za Serikali kama ambavyo baadhi yake  zilivyoainishwa hapo juu, kwani kuna bidhaa ambazo zinatakiwa ziingie katika mfumo mzima  au mnyororo wa uongezwaji wa thamani  kabla ya kuwekwa katika soko la bidhaa. Na hapa Wizara mbalimbali zinahusika, na Waziri aliyetajwa ni Mmoja tu Waziri wa Fedha. Hii inaweza kukwamisha utekelezaji wa mfumo huu ambao tunaamini kuwa ni kwa faida ya wazalishaji wa bidhaa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo kuhusiana na suala hilo la kutokutambuliwa na sheria kwa watendaji wengine wa Serikali ambao ni nguzo pia katika kuhakikisha bidhaa inauzwa, au wako karibu na wazalishaji.
Mheshimiwa Spika, katika kifungu cha 6 kinachohusu majukumu au kazi za mdhibiti, limetumika neno “Institutions” lakini neno hilo halijatolewa tafsiri, hivyo basi ni muhimu neno hilo likatolewa tafsiri  yake ili kuondoa mkanganyiko kwa wadau wa Sheria hii.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 8(3) kinasema kwamba
“A company which is licensed as a commodity exchange shall not appoint any person to the position of Chief Executive Officer or Managing Director, senior management or the Board of Directors, change a substantial shareholder or change the organization structure without obtaining prior confirmation of the Authority”.
Mheshimiwa Spika, ni vyema Kambi Rasmi ya Upinzani ikapata maelezo ya kina kuhusiana na katazo hilo kwani kampuni pindi inaposajiliwa kwa mujibu wa sheria za makampuni sura ya 212, inakuwa na bodi yake na inakuwa na mamlaka kamili, na pia katika utendaji wake wa kazi bodi ndiyo yenye mamlaka ya kuteua nani awe ni mtendaji mkuu wa kampuni husika kwa vigezo walivyoweka wao.

Mheshimiwa Spika, Aidha, kulingana na mazingira ya kampuni ni jukumu la kampuni husika au wanahisa ambao ni wakurugenzi kuingiza mwanahisa au kumtoa kulingana na Articles of Association (makubaliano yao)  zinavyosema. Sasa kitendo cha kuomba ruhusa kwanza kwa Mdhibiti wa Uendeshaji wa Soko la Bidhaa ni kuingilia mambo binafsi ya Kampuni husika. Tukumbuke kuwa Mtendaji Mkuu ni mwajiriwa na si mmiliki pale ambapo  mmiliki akiona mtendaji mkuu hafanyikazi wala kutekeleza majukumu yake kwa maslahi ya wanahisa hivyo ni jukumu la Bodi ya wakurugenzi kuchukua maamuzi.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 3 na 4 cha muswada kinatoa ishara kama kwamba (makampuni yote) wale wote waliopata leseni “licensees” za soko la bidhaa ni mali ya Mamlaka,  tukumbuke kwamba wadau wakuu wengi ni sekta binafsi hivyo kuiambia sekta binafsi isibadilishe mfumo wa utendaji kazi na watendaji wake, ni kuingilia masuala binafsi ya kampuni. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema, Jambo hili halikubaliki kabisa na hivyo basi vifungu hivyo vifutwe kwa lengo la kuleta tija.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 9 (1) (b), (c) katika muswada bado vinaingilia mamlaka binafsi ya Kampuni na pia vinaweka ulinzi ambao utasababisha watendaji kujiona nao ni wamiliki na hivyo kuathiri utendaji kazi wao. Hoja ya Msingi ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani ingependa kuuliza ni kwanini ulinzi huo wa nafasi ya Mtendaji Mkuu hadi kuwekwa katika Sheria? Ni kweli kwamba haina ushindani pale wenye kampuni wanapotaka kufanya mabadiliko ya uongozi? Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kufuta vifungu hivyo vya ulinzi wa nafasi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 67 cha muswada ambacho kinaelekeza kutumia maelezo ya kifungu cha 66(c ) cha sheria ya CAPITAL MARKET kuhusiana na tafsiri ya maneno ya mienendo mbalimbali ambayo hairuhusiwi kwenye biashara ya masoko ya bidhaa. Katika hilo Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kitendo cha kutumia  rejea ya sheria nyingine “cross reference” ya sheria nyingine kwenye sheria hii ni uzembe, kwani sio mara zote mtumiaji wa sheria hii atakuwa katika nafasi ya kuwa na sheria nyingine ambayo inafanyiwa rejea.

Aidha, Mheshimiwa Spika, kifungu hicho hicho kimetumia maneno “manipulation, rigging Bucketing and Cornering” lakini kwa bahati mbaya katika kifungu cha 2 cha muswada kinachohusu tafsiri ya maneno, maneno hayo hayapo. Pia kwa kuwa tunatarajia sheria hii iwe toshelevu katika matumizi yake. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuhakikisha kwamba kila kifungu katika sheria hii kijitosheleze badala ya kufanya rejea katika kifungu kingine cha sheria nyingine.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 70 cha muswada kinachohusu “liability to pay damages” kuwa mtu yeyote atakayekutwa na hatia katika sehemu nzima ya XIII mbali ya kosa la kijinai kwa kosa husika  pia atalazimika kufidia hasara iliyotokea katika manunuzi. Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kwamba kwa kuwa kitendo chochote cha kupanga kinachopelekea hasara kwa bidhaa hasa za kilimo. Maana yake ni kuhatarisha maisha ya mkulima, hivyo basi adhabu kali inatakiwa kutajwa kwenye sheria hii. Kwani adhabu ilivyowekwa katika muswada huu wa sheria haiko wazi ili kuwafanya wenye nia ovu kushtuka.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 82 cha muswada kinachohusu ulinzi “immunity” kuwa mamlaka, afisa au mtumishi yeyote hatahesabika ametenda kosa kwa kutenda au kutokutenda jambo na kupelekea hasara wakati akitimiza wajibu wake kwa nia njema, hadi pale itakapo bainika kuwa alikuwa ana nia mbaya.

Mheshimiwa Spika, kifungu hiki kama ambavyo kwa sheria nyingine zilizopita Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa haikubaliani na kifungu cha aina hii kwani kinahalalisha uzembe. Kwa sekta ya afya,  uzembe wowote unagharimu maisha ya mtu na pia hapa tukiachia sheria kuwa na kifungu hiki, maana yake tunatoa mwanya wa kutokuwajibika na mwishowe ni hasara na inaweza leta athari kubwa  kwa wanunuzi wa bidhaa na mara zote hasara inapelekwa kwa mzalishaji hasa mkulima kwa kuwa yeye ndiye mnyonge katika mfumo wa masoko ya bidhaa za kilimo. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kifungu hiki kifutwe.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema  hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

…………………………………
David Ernest Silinde (Mb)
K.n.y Waziri Kivuli- Wizara ya Fedha
29.06.2015


No comments:

Post a Comment