Saturday, July 18, 2015

Chadema: CCM kinafaa kuwekwa jumba la makumbusho

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka Watanzania kutokipigia kura ya ndiyo Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa madai kuwa chama hicho kimeshindwa kuongoza na kinastahili kuwekwa jumba la makumbusho kiwe kumbukumbu ya mateso ya Watanzania.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mkalamo kilichopo Kata ya Mkalamo, Mwenyekiti wa vijana wa Chadema Wilaya ya Korogwe, (Bavicha), Swed Magasa, alisema kuwa chama hicho sasa kinastahili kuwekwa makumbusho kwa ajili ya kumbukumbu kwa vizazi vijavyo kutambua jinsi kilivyowatesa na kuwanyanyasa Watanzania.

Magasa alisema endapo wananchi watakiondoa madarakani chama hicho mwezi Oktoba, ataishauri Chadema kukiweka katika jumba la makumbusho ili mabaya yake yasije kuigwa na vizazi vijavyo.

Hata hivyo, Magasa alisema CCM kitakumbukwa kwa jinsi kilivyofilisi na kuwafanya Watanzania kuwa masikini licha ya nchi yao kuwa na rasilimali za kutosha na jinsi kilivyoasisi vitendo vya unyanyasaji, ufisadi, rushwa na ukandamizaji wa wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Chadema, Jimbo la Korogwe vijijini, Peter Lameck, alisema chanzo cha matatizo ni mfumo wa CCM na sera zisizotekelezeka na kwamba njia mbadala ni wananchi kuachananacho na kuichagua Chadema.

Mwenyekiti wa wanawake wa Chadema mkoa wa Tanga (Bawacha), Mese Sanga, aliwakumbusha wananchi wakiwemo akinamama kutambua kuwa kura yao ndiyo ukombozi wa maisha yao na vizazi vyao na kwamba zawadi za khanga, vitenge, fulana na vitambaa visiwaponze.

Sanga aliwataka akinamama kupigakura za hasara Oktoba, wakikumbuka mateso wanayoyapata na kuwachagua wagombea kutoka umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa), ambao ndiyo suluhu ya matatizo yao.

Mmoja wa watia nia ya ubunge wa Jimbo hilo, Emmanuel Kimea, alisema endapo chama chake kitampitisha na wananchi wakamchagua kuwa mbunge atahakikisha haki ya kila mtu inapatikana ikiwemo huduma sahihi za afya, maji, barabara na elimu zinakuwepo kwa viwango stahiki.

No comments:

Post a Comment