Thursday, June 18, 2015

Nape Nnauye tulia, Muosha Huoshwa. Dr.Slaa alisafiri kikazi

Baada ya Dr.Slaa kurejea nchini akitokea Bara Ulaya alipokuwa kikazi kulingana na ratiba yake ya kiutendaji ,Nape Nnauye amenukuliwa kwenye mikutano ya hadhara akitoa tuhuma za uongo na uzushi kuwa ameenda Ulaya kuomba fedha za kampeni na kupewa masharti hatarishi kwa nchi yetu na kudai kuwa yeye na chama chake wanao ushahidi

Inashangaza sana katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama tawala anapojikita katika uzushi na kuropoka uongo majukwaani badala ya kunadi sera na itikadi ya chama chake ,inakua msiba zaidi kwa vijana na kwa taifa inapokua kwamba aliyefanya hivi ni kijana msomi

Anaidhalilisha serikali yake kuwa haina uwezo wa kupata taarifa muhimu za usalama wa nchi.Kama Dr.Slaa anaweza kusafiri kutoka hapa Tanzania hadi Ulaya kisha anaomba fedha na kupewa masharti hatarishi bila usalama wa taifa kujua,bila balozi zetu nje ambako kuna Mwambata wa Jeshi(Defence Attache') kwenye balozi zetu zote huko nje ,je taifa letu ni salama? Je,usalama wa nchi yetu katika mikono ya CCM ni wa kiwango gani? Mbona hajakamatwa hadi sasa na badala yake viongozi wa chama tawala wanazusha na kuhadaa watu kuwa wanao ushahidi ambao walipaswa kuupeleka kwenye vyombo vya dola?

Ni vyema watanzania hasa wale wana-CCM waaminifu kabisa wakakumbuka kuwa ni Nape huyu huyu ambaye amekua mstari wa mbele kujifanya ana uchungu sana na CCM kiasi cha kuwatukana wana-CCM wenzake akina Edward Lowassa na pia kuwafanyia fitna vijana wenzake ndani ya chama akina Mwigulu Nchemba na January Makamba wanaonekana kufanya siasa za kisomi

Anachofanya sasa ni kutapatapa baada ya kujua mradi aliokua akizunguka nao nchi nzima wa kuvua gamba sasa unamtokea puani na hali yake kisiasa na mustakabali wa nafasi aliyonayo umefika ukingoni

Amegundua kuwa kashfa zake dhidi ya makada wenzake kuwa 'Hawasafishiki hata kwa dodoki" zinaelekea kumrudia sasa anaamua kutafuta uongo na uzushi kama ilivyo kawaida ya wanasiasa waliofilisika kisiasa

Mathalani,Mwana-CCM na Mtanzania makini atajiuliza kama makada wenzake ni wachafu na wanakichafua chama chake ,je yeye aliyeanzisha chama cha CCJ na kutaka kukipasua chama cha Mapinduzi ana maadili au usafi kiasi gani cha kuwatukana wenzake kuwa ni magamba wasiosafishika kwa dodoki?

Je,kwa mradi wake wa chama cha CCJ alichokiasisi akiwa ndani ya CCM atasafishika hata kwa Msasa?

Tumshauri,tumuonye na kumuelekeza kijana huyu mwenzetu katika siasa za kisayansi na kuitendea haki fursa aliyopewa ili vijana tuendelee kuaminika na kupewa mamlaka katika vyombo vya maamuzi

Tutaendelea kukutana Mitandaoni na majukwaani sasa

Aluta Continua,Victory Ascerta.....

Ben Saanane

No comments:

Post a Comment