Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezindua operesheni maalum ya kuwaamsha wanawake nchini kote kwa nia ya kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 na kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kupiga kura nyingi za ndiyo kwa wagombea wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Aidha, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani , Mabele Marando, amewataka wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi katika daftari la wapigakura ili kufanikisha kumpeleka Ikulu mgombea atakayesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao unaundwa na Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.
Akizungumza katika uzinduzi wa operesheni hiyo inayofahamika kama ‘Operesheni Amsha Wanawake Tanzania’, kwenye viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam jana, Marando alisema ni vizuri wananchi wakajitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuacha kusikiliza majungu ya baadhi ya watu dhidi ya Ukawa. Alisisitiza kuwa umoja huo haujateteleka na utasimamisha mgombea mmoja wa urais.
Marando alisema madai kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, kuchukua fomu za urais ndiyo sababu Ukawa inatetereka yasiwashitue wanachama kwa kuwa huo ni utaratibu wa chama (CUF)ambao hauhusiani na mipango ya Ukawa.
Mkurugenzi wa bendi ya wanawake, Lilian Wasira, aliwataka wanawake wajitokeze kwa wingi kwa kuwa wao ndiyo wenye mchango mkubwa katika kupiga kura.
Alisema kuwa uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) umewafanya wanawake kubaki katika maisha ya kimasikini hivyo kupitia bendi hiyo itasaidia wanawake kuchagua rais kupitia ukawa na moja kwa moja kwenda ikulu na kubadirisha maisha yao kwa ujumla.
“Mimi ni mwanasheria lakini nimeamua kuimba ili wanawake wanielewe kwa sababu CCM imefilisika. Ikulu Oktoba 25, mwaka huu ni ya Ukawa,”alisema Wasira.
No comments:
Post a Comment