Wednesday, May 6, 2015

Tamko la Kamati Kuu ya CHADEMA - Mei 5, 2015


Tamko la Kamati Kuu ya CHADEMA - Mei 5, 2015


C/HQ/ADM/KK/08 05/05/201

MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHADEMA ILIYOKUTANA DAR ES SALAAM, MEI 3-4, 2015.

Ndugu waandishi wa habari
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imekutana katika kikao chake cha kawaida kwa mujibu wa Katiba ya Chama kuanzia tarehe 03-04/05/2015 pamoja na masuala mengine imejadili na kufanyia maazimio mambo yafuatayo;

Uteuzi wa wagombea ndani ya chama

Kamati Kuu imeazimia mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu kwa ajili ya uteuzi wa ndani ya chama uanze ili watia nia katika maeneo mbalimbali wachukue fomu za udiwani, uwakilishi na ubunge na imetoa ratiba rasmi ya kuanza kwa zoezi hilo (Ratiba imeambatanishwa).

UKAWA

Kamati Kuu imepokea na kujadili mwenendo wa majadiliano na makubaliano ambayo hadi sasa yameshafikiwa na vyama vinavyounda UKAWA (NLD, NCCR- Mageuzi, CUF na CHADEMA), ambapo imewapongeza viongozi wakuu wa vyama vyote kwa hatua ambayo wameshafikia na imewataka wamalize masuala machache yaliyobakia ndani ya wakati ili waweze kuwatangazia Watanzania wanaoendelea kuunga mkono umoja huo wa dhati.

B. V.R, Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu

Kamati Kuu imepokea taarifa ya kina kuhusu mwenendo wa shughuli ya uandikishaji wapiga kura kwa mfumo wa BVR unaonedelea katika maeneo mbalimbali ambapo baada ya mjadala, imejiridhisha kuwa hadi sasa hakuna dhamira ya dhati ya kisiasa wala maandalizi ya kutosha yakiwemo matakwa ya kisheria, kitaalam na kibajeti ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa Katiba ..

Kutokana na taarifa hizo, Kamati Kuu imeridhika kuwa iwapo Watanzania hawatahamasishwa na kuamuka kudai haki yao ya kikatiba ya kuandikishwa na kupiga kura, zipo dalili za wazi kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) chini ya Jaji Damian Lubuva inaweza kusababisha majanga makubwa kama ambavyo Tume ya Uchaguzi ya Kenya chini ya Bwana Kivuitu ilisababisha nchini humo mwaka 2008, Jaji Lubuva anajiandalia mazingira ya kuwa ‘Kivuitu wa Tanzania’.

Mbali na kukubaliana na hatua ambazo zimeshachukuliwa na UKAWA katika jambo hili hadi sasa, katika hali inayoendelea kwenye mikoa ambako sasa uandikishaji unafanyika baada ya Mkoa wa Njombe, imeazimia ifuatavyo;

Watanzania wote wenye sifa ya kuwa wapiga kura wanaandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi.

1.3 Kuhusu Kura ya Maoni

Kamati Kuu pia imejadili kwa kina namna ambavyo mazingira ya kisheria na uhalisia wa mwenendo wa kisiasa na kiuchumi nchini kwa sasa hauruhusu Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa, isipokuwa hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Octoba 2015 kwa mujibu wa Katiba.

Hivyo kikao kimeazimia kuwa chama kiendelee kusimamia msimamo wa UKAWA uliotolewa hivi karibuni kuwa Kura ya Maoni isifanyike pamoja na Uchaguzi Mkuu lakini pia kwa vyovyote vile kura ya maoni iwe mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Octoba 2015.

1.4 Kuhusu hatma ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015

Kamati Kuu ilipokea taarifa ya kina namna ambavyo hadi sasa maandalizi ya msingi yanayotakiwa kisheria kwa ajili ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu hayajafanyika kama vile maandalizi ya vifaa, fedha , kutangaza Majimbo na Kata Mpya , kutangaza vituo na kusuasua kwa zoezi la Uandikishaji wapiga kura .

Katika jambo hili Kamati Kuu imeazimia kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu LAZIMA ufanyike mwezi Octoba kwa Mujibu wa Katiba na Serikali ya CCM isijiandae kutumia kisingizio chochote kuahirisha kwa sababu uchaguzi sio jambo la dharura, bali lilijulikana miaka 5 iliyopita.



Aidha imeitaka Serikali ya CCM chini ya Rais Kikwete kuacha hila zozote za kutaka kujiongezea muda wa kukaa madarakani, ikiwemo kutaka kupeleka ‘Muswada wa Marekebisho ya Katiba Bungeni’ ili kujihalalishia kuongeza uhai wa Serikali ya Kikwete.

Kamati Kuu imeitaka serikali kuchukua hatua za dharura kunusuru shilingi kwani athari zake ni kubwa sana kiuchumi na kijamii na zitasababisha mfumko wa bei .

Kamati Kuu imeazimia na kulaani tabia ya Rais wa nchi kusafiri ovyo nje ya nchi wakati ipo katika kipindi kigumu ikiwa na matatizo makubwa ambayo yanahitaji uongozi thabiti wa Mkuu wa nchi.

Sekta ya usafirishaji Nchini

Kamati kuu ilipokea ,kujadili na kutafakari hali halisi ya sekta ya usafirishaji nchini na kubaini udhaifu mkubwa ambao upo ndani ya sekta hiyo kutokana na usimamizi dhaifu wa watu ambao walipewa dhamana ya kusimamia sekta hiyo kuanzia waziri wa uchukuzi ambaye ameshindwa kabisa kuisimamia sekta hiyo , hali hiyo imepelekea sekta hiyo kukosa mwelekeo na kusababisha madhara mengi kwa wananchi kutokana na ajali za kila siku kuanzia vyombo vya Majini na Barabarani.

Kamati kuu imebaini athari ambazo zimewakumba watanzania kutokana na Mgomo wa Madereva kama vile wagonjwa kushindwa kufika hospitalini, maiti kushindwa kusafirishwa na kuzikwa , wanafunzi ambao wanafanya mitihani ya kidato cha sita kushindwa kufika kwenye vituo vyao hali iliyopelekea kushindwa kufanya mitihani yao , kuathirika kwa uchumi na wananchi kuathirika kisaikolojia.

Baada ya tafakuri ya kina, Kamati Kuu imeazimia kuunga Mkono madai ya Madereva kwani ni halali na hivyo ni lazima serikali iyatekeleze madai yao yote ya muda mrefu , kuendelea kuyapuuza madai hayo ni kukubali kuendelea kuhatarisha maisha ya Abiria ambao wanasafiri kutokana na ajali za kila mara, hivyo ili kuokoa maisha ya wasafiri, Madereva wasikilizwe na wapatiwe ufumbuzi wa madai yao yote kuanzia mikataba ya ajira, maslahi yao na kulipwa ujira unaolingana na kazi zao.

Imetolewa leo

Freeman Mbowe
……………………………

Mwenyekiti wa CHADEMA (T)


No comments:

Post a Comment