Saturday, May 23, 2015

Mnyika anena kauli ya JK kuhusu wahisani

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Mnyika, amesema kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka wahisani waiheshimu serikali na kwamba wasitoe misaada kwa masharti, imetokana na hasira za rais baada ya kuanikwa na magazeti ya Marekani juu ya sheria zinazodaiwa kutungwa kwa ajili ya kuminya uhuru wa habari na utoaji wa taarifa.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, alisema kitendo cha wahisani kugomea kuchangia msaada wao katika mfuko wa bajeti kimesababishwa na kukithiri kwa ufisadi hasa katika sekta za maji, afya na kashfa ya Escrow.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mnyika alisema ufisadi uliofanyika kuanzia ngazi ya wizarani hadi kwenye halmashauri ambao umekwamisha miradi ya maendeleo maeneo mbali mbali nchini, umesababisha wahisani kuiwekea ‘mguu chini’ serikali ambayo badala ya kuchukua hatua, inaanza kugombana na nchi wahisani suala ambalo amedai kuwa litaiwekea mazingira magumu serikali ijayo.

“Kama Rais Kikwete angekuwa na dhamira ya dhati ya serikali yake kuwa na sauti anayotaka kutuaminisha sasa ili iheshimiwe, isichezewe, angeonesha kupitia bajeti hii ya sasa. Huwezi kusema kuwa nchi inaweza kwenda bila misaada ya wahisani wakati huo huo utekelezaji wa bajeti yake ya mwaka 2015/16 inayojadiliwa sasa bungeni bado inategemea wahisani hao hao wasaidie.

“Kama Rais Kikwete angetaka kudhihirisha kuwa serikali yake ni imara na inaweza kuifanya nchi ijitegemee bila kusubiri misaada ya wahisani angesema maneno haya na kufanya kwa vitendo kuanzia mwaka 2005 alipoingia madarakani au 2010 alipoingia madarakani kwa mara ya pili, vinginevyo kuisema sasa hivi wakati amebakiza miezi michache kuondoka madarakani ni kutaka kuitengenezea mazingira mabaya serikali ijayo ambayo haitakuwa ya CCM," alisema na kuongeza:

“Sasa baada ya ufisadi kuzidi kwenye serikali yake, huku kukiwa na udhaifu mkubwa wa uwajibikaji na hatua hazichukuliwi, wahisani wameamua kuweka msimamo hivyo imepelekea miradi mingi ya maendeleo kukwama, badala ya serikali kuchukua hatua, rais anawatishia wahisani, hizi ni hasira za Rais baada ya magazeti ya Marekani kumwanika kuwa serikali inatunga sheria mbaya za kuminya uhuru wa habari na utoaji taarifa."

“Kwa sababu CCM haiwezi kusaidia nchi hii kujitegemea suluhisho hapa ni kukiondoa madarakani chama hiki kwanza. Watanzania wajiandae kuiweka Serikali ya Ukawa ili ishughulikie na kuondoa ufisadi, ipanue wigo wa vyanzo vya ndani katika kuongeza mapato na kudhibiti matumizi makubwa ya anasa na kubadili mfumo wa utawala,” alisema Mnyika.

No comments:

Post a Comment