HOTUBA YA KIONGOZI WA KAMBI
RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE.FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO
YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KATIKA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MWAKA WA FEDHA
2015/2016
(Inatolewa
chini ya Kanuni ya 99 (9), ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Mwaka 2013)
_________________________________
1. UTANGULIZI:
Mheshimiwa Spika,
Kwanza
kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunilinda na kunitunza
ili niweze kutumikia taifa langu. Napenda kuishukuru familia yangu kwa msaada
mkubwa na uvumilivu hasa katika harakati na shughuli zangu za kisiasa.
Mheshimiwa Spika,
Napenda
kuchukua nafasi hii pia, kuwashukuru watanzania wote kwa ujumla kwa kupokea na
kulea harakati za mabadiliko nchini. Shukrani hizi za pekee ziwafikie wenyeviti
wenza wa vyama vinavyounda UKAWA , Mhe. Prof Ibrahim Lipumba, Mhe. James Mbatia
na Mhe. Dk Emanuel Makaidi. Vilevile, kwa makatibu wakuu viongozi wa UKAWA Mhe.
Maalimu Seif Shariff Hamad, Mhe. Wilbroad Slaa, Mhe. Mosena Nyambabe na Mhe. Tozi Matwange. Aidha, shukrani hizi ziende kwa timu ya
wataalamu wa UKAWA, viongozi, watendaji, wanachama na wapenzi wa vyama vyetu
vinavyounda UKAWA vya NLD, CUF, NCCR-Mageuzi na CHADEMA. Niwatake wanachama na
wapenzi wa UKAWA kujipanga, kujituma na kujiandaa kushinda kwa kishindo na
kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa Tanganyika na Zanzibar.
Aidha,
shukrani za pekee ziende kwa wabunge wote wa Kambi ya Upinzani Bungeni
wanaounda UKAWA kwa kazi nzuri ya kutetea na kusimamia maslahi ya wananchi. Na
pia kwa watendaji wa Kambi ya Upinzani ambao wamekua msaada mkubwa kwetu na kwa
kazi yao nzuri kwa taifa letu.
Endelea.......
Endelea.......
Mheshimiwa Spika,
Napenda
kuwashukuru kwa kipekee, wananchi wa Jimbo letu la Hai kwa ushirikiano mkubwa
na imani waliyonayo kwangu kama mwakilishi wao. Niliwaahidi kuwatumikia kwa
moyo wangu wangu wote na naendelea kuwaahidi kuwa imani yao kwangu haitopotea
bure.
Mheshimiwa Spika,
Napenda
kuwashukuru kwa kipekee wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,
Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Peter Kayanza Pinda, Spika wa Bunge Mhe. Anna Makinda,
Naibu Spika Job Ndugai na Katibu wa Bunge Ndugu Dk. Thomas Kashilila pamoja na
wafanyakazi wa Bunge kwa ushirikiano mliotupa toka kuanza kwa Bunge la 10,
vilevile napenda kuwatakia heri Mhe. Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mhe. Spika
Anne Makinda katika maisha mengine nje ya siasa za Bunge kwani walishatangaza
kustaafu ubunge.
Mheshimiwa Spika,
Baada
ya shukrani hizo za kipekee napenda kunukuu maneno machache kutoka kwa Nelson
Mandela aliyepata kusema;
“I
learned that courage was not the absence of fear, but the triumph over it. The
brave man is not he who does not feel afraid, but he who conquers that fear.”
“Nimejifunza
kwamba ujasiri si kukosekana wa uoga bali ushindi dhidi ya uoga. Mwanadamu
jasiri si Yule ambaye hahisi uoga bali Yule anayeshinda uoga”
Vilevile
Nelson Mandela alipata kusema;
“When a man is
denied the right to live the life he believes in, he has no choice but to
become an outlaw.”
“Pale
Binadamu anaponyimwa kuishi maisha anayoyaamini, huwa hana njia bali kuwa
mvunjaji wa Sheria”
2. MWAKA WA TUMAINI JIPYA
Mheshimiwa Spika,
Huu ni mwaka
ambao nchi yetu itafanya uchaguzi Mkuu wa Kihistoria ambao utakitoa
chama ambacho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 50 na hivyo kujikuta kimechoka na kukosa mawazo mapya na ya kisasa
ya kuendesha na kuendeleza nchi yetu.
Ukweli huu mchungu ni vyema ukaanza kuwaandaa
kisaikolojia wote walioko kwenye mamlaka kutambua kwamba kubadilisha chama
kinachoongoza Taifa siyo jambo geni duniani. Ni fursa ya nchi kutafuta muelekeo
mpya wenye kujaza tumaini jipya, fikra mbadala na SHAUKU ya kuondokana na
uendeshaji wa kimazoea wa Serikali na maisha ya wananchi wake.
Nipende kuwahakikishia wote, hususan walioko
madarakani kuwa UKAWA umedhamiria kwa dhati kurejesha utawala bora wenye
kuzingatia haki na sheria, usimamizi makini wa rasilimali na tunu za Taifa na umekusudia
kujenga Tanzania mpya yenye mshikamano wa kweli, uhuru wa kweli, amani ya kweli
na ustawi wa wote bila kubagua kwa misingi ya kiitikadi, dini, kabila, jinsia
au rangi kama ilivyo leo.
Mheshimiwa
Spika,
Kutokana
na umuhimu wa mwaka huu kuwa wa uchaguzi Mkuu kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu
nitajikita zaidi kwenye eneo hilo. Lengo ni kuweka rekodi sahihi kuwa sisi
Kambi ya Upinzani tulionya sana na kwa muda mrefu kuhusu umuhimu wa uwazi na
maandalizi shirikishi ya mapema ili kulihakikishia taifa mserereko salama wa
mpito, yaani “smooth transition” kutoka awamu ya nne ya Utawala wa nchi yetu
kwenda awamu ya tano. Mpito salama ambao utatokana na kuwepo kwa uchaguzi huru,
wa haki na uwazi.
3. DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA
KURA (BVR)
Mheshimiwa Spika,
Tume Taifa ya
Uchaguzi imeanza zoezi la kuandikisha upya wapiga kura katika mfumo mpya wa
kielectronic ambao unajulikana kama BVR na zoezi hili lilianzia katika mji wa
Makambako mkoani Njombe Mwezi Februari 2015 na Sasa linaendelea kwenye baadhi
ya Kata za Mikoa ya Lindi, Mtwara,
Ruvuma, Iringa na Mbeya .
3.1 Hujuma za Serikali dhidi ya Tume :
Mheshimiwa Spika ,
Pamoja na kuwa tarehe ya uchaguzi mkuu ilijulikana tangu
tulipomaliza uchaguzi mkuu uliopita, Serikali ama kwa makusudi ama kwa
kugubikwa na misukumo ya kimaslahi, imeshindwa kukamilisha daftari la kudumu la
wapiga kura kwa wakati muafaka. Pamoja na mengine, Ucheleweshaji wa kuandikisha
wapiga kura umesababishwa na Tume kutopewa fedha na Serikali kwa wakati
muafaka. Mwezi Februari 2013 wakati Rais Kikwete akizindua vitambulisho vya
taifa alisema vitambulisho hivyo ndivyo vitakavyotumiwa katika kura ya maoni na
uchaguzi mkuu. Hata hivyo Serikali haikufanya uratibu wa Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Tume ya Uchaguzi ili taasisi mbili
zishirikiane na kukamilisha zoezi hili.
NIDA haikupewa fedha za kutosha kukamilisha zoezi la kuandikisha na
kutoa vitambulisho vya taifa. Tume ya Uchaguzi ikaanzisha mchakato wa kuandikisha
wapiga kura bila kutengewa fedha za kutosha za kununulia vifaa, kuajiri na
kuwapa mafunzo wafanyakazi husika, na kutoa elimu kuhusu kujiandikisha kwa
wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Hivi sasa serikali inaonekana kuwa na matatizo makubwa ya
fedha baada ya wahisani kusitisha kutoa fedha za msaada wa bajeti kwa sababu ya
ufisadi wa kutisha wa Tegeta Escrow Account.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na ukweli kuwa Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi inahitaji Tume kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga kura angalau mara mbili kati
ya uchaguzi mkuu na unaofuata; Kwa makusudi Serikali iliamua kuivunja sheria ya
kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa ,Kitendo hiki kina malengo na nia mbaya ya kutaka kuongezea
muda wa utawala wa Rais Kikwete kwa kisingizio kuwa uchaguzi mkuu hauwezi
kufanyika kwani daftari la kudumu la wapiga kura bado halijakamilika kuboreshwa.
3.2 Udhaifu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika BVR.
Mheshimiwa Spika ,
Pamoja na zoezi kuanza kwa kusuasua ni wazi kuwa Tume
haina watumishi wa kufanya kazi katika
zoezi hili muhimu kwa uhai wa Taifa , pamoja
na ushauri wa mshauri Mwelekezi kutoka Kampuni ya IPSITI ya Nchini Marekani na ambayo ripoti iliwasilishwa kwa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi mwezi Januari 2015 , Mshauri ambaye Tume ilimpa majukumu ya
kuwashauri na kumlipa mamilioni ya fedha za walipa kodi na hata alipowashauri Tume
kuwa wanahitaji kuwa na zaidi ya watumishi 10,000 kwa ajili ya kuhakikisha kuwa
zoezi hilo linaweza kufanyika kwa ufanisi na kufanikiwa kwa nchi nzima.
Mshauri huyo mwelekezi alienda mbele zaidi na kuwaambia
Tume kuwa Ni lazima watumishi hao wawe wamepatiwa mafunzo ya kina kuhusu jinsi
ya kuweza kutumia mfumo huu mpya wa BVR kuandikisha wapiga kura na hata jinsi
ya kutumia mashine zenyewe .
Mheshimiwa Spika,
Jambo la kusikitisha ni kwamba Watumishi wa Tume ambao
wameanza kufanya kazi ya kuandikisha wapiga kura wamepatiwa mafunzo kwa muda wa siku moja au mbili tu kabla ya zoezi la kuandikisha wapiga kura
kuweza kuanza , kati yao wapo watanzania ambao wamepewa kazi hiyo na hawajawahi
kutumia Kompyuta kabisa katika maisha yao na hata hizi mashine ni mara ya
kwanza kuonekana na kutumika Nchini mwetu, na hivyo kulifanya zoezi kuwa gumu
zaidi kutokana na watumishi kutokupata mafunzo ya kutosha na hivyo kuweza
kuwasaidia katika kutumia mashine za BRV na hata wanapoanza kupata uzoefu muda
wa kuandikisha unakuwa umeisha ,yaani siku saba.
Aidha , baadhi ya Wapiga picha wameshindwa kutimiza
majukumu yao kwa wakati kwani wanashindwa kutumia Kamera ambayo wamepewa kwa
ufanisi na hivyo kulifanya zoezi kwenda taratibu sana na foleni kuwa ndefu
vituoni.
Mheshimiwa Spika,
Tume haisemi kweli kuhusiana na zoezi hili. Mara kadhaa,
viongozi wa Tume wamekuwa wakitoa kauli kadhaa zisizotekelezeka na kisha kuzibadilisha
bila maelezo yenye mantiki. Tume imeendelea kusisitiza kuwa zoezi hili litaweza
kukamilika kwa muda uliopangwa bila kuweka hadharani imani hiyo inatokana na
nini ilhali mazingira yote ya kisayansi yanaonyesha kinyume. Ikiwa Tume ina nia
ya kuwapa fursa ya kujiandikisha Watanzania wote takribani milioni 24 wenye sifa
na haki ya kupiga kura, haiwezekani ikakamilisha mchakato mzima kabla ya kuanza
kwa kampeni mwezi wa Agosti 2015 labda pengine miujiza ifanyike.
Mheshimiwa Spika,
Tume haitaweza kuandikisha wapiga kura wote kwa muda wa
siku saba ambazo imeweka kwa kila kituo .— Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Lubuva alipokuwa anamkaribisha Waziri Mkuu
Pinda kuzindua rasmi uandikishaji wa wapiga kura katika Mji wa Makambako
alisema kuwa tarehe 24 /2/2015 waliweza
kuandikisha wapiga kura 3,014 katika vituo 55. Yaani kila mashine moja ilikuwa
na uwezo wa kuandikisha wastani wa wapiga kura 54 kwa siku, hii maana yake ni
kuwa kama tume ikiweza kupata mashine zote 7750 ilizoagiza kwa wakati na kuwa
na jumla ya mashine 8000 inaweza kuandikisha wapiga kura 432,000 kwa siku na
hivyo kwa siku 7 za ratiba ya tume kwa kutumia mashine zote 8000 wataweza
kuandikisha wapiga kura 3,024,000 tu.
Mheshimiwa Spika ,
Ili kuandikisha wapiga Kura 24,000,000 wanaokisiwa,
itahitajika wastani wa siku 56 kila mashine kuandikisha kwenye vituo nchi nzima
ili kukamilisha zoezi hilo na bila mashine kuharibika.
Na hivyo ni ukweli uliowazi kuwa mpaka tarehe ya mwisho
ambayo haijajulikana kwani Tume haijasema itaandikisha wapiga kura mpaka lini ili
kuwe na muda wa kuhakiki Daftari lenyewe , kwa mwendo huu wa kuandikisha wapiga
kura 54 kwa mashine moja kwa siku, lengo la kuandikisha wapiga kura wote 24
milioni halitawezekana kwa muda huu ambao Tume imelitangazia taifa.
Mheshimiwa Spika,
Zoezi hili linaendelea kufanyika licha ya Tume kutokuwa
na vifaa vya kutosha kama ambavyo iliomba ipatiwe na serikali BVR kits 10,500
lakini serikali ikawaahidi kuwapatia KITS 8000 na ambazo mpaka leo hazijafika
nchini zote kwa kuwa serikali ilichelewesha fedha makusudi na hivyo Mkandarasi
akasimamisha uzalishaji wa mashine hizo hadi Serikali ilipomalizia malipo hayo
mwezi Machi mwaka huu na hii ni kwa mujibu wa Randama ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ambayo wamesema , nanukuu uk.10 ‘Baada ya kupatikana fedha kidogo kwa ajili
ya uendeshaji, zoezi la Uboreshaji limeanza tarehe 23 Februari,2015 katika Mkoa
wa Njombe , Halmashauri ya Mji wa Makambako na baadaye mikoa mingine itafuata
kulingana na kufika kwa BVR Kits 7,750 zilizobaki.’ Mwisho wa kunukuu. Hii ni taarifa ya tume ya April ,2015.
Mheshimiwa Spika ,
Tume kwenye randama yao wameendelea kueleza kuwa ,
nanukuu uk.10 ‘Awali Tume ilipanga kutumia BVR kits zipatazo 10,500 kwa nchi
nzima,lakini baadaye zilipunguzwa hadi BVR kits 8,000 baada ya majadiliano na
Serikali’ Hii maana yake ni kuwa Serikali iliamua makusudi kupunguza
BVR kits hizo bila kujali ushauri wa kitaalamu wa Tume. Na hata baada ya
kupunguza mashine hizo bado ilishindwa kuzilipia kwa wakati ili kuiwezesha tume
kuandikisha wapiga kura kwa mujibu wa kalenda yao jambo ambalo sasa linatishia
uhakika wa kuwepo kwa uchaguzi Mkuu hapo Mwezi Octoba.
Mheshimiwa Spika,
Tume haijatoa taarifa za kutosha kwa wadau wote kuhusu
teknolojia ya BVR, kampuni inayotengeneza mashine zinazotumiwa, kampuni gani
iliyopewa tenda ya programu ya kompyuta (software) itakayoendesha na kusimamia
daftari la kudumu, taratibu za kuhifadhi kumbukumbu, usafirishaji wa kumbukumbu
kutoka vituo vya kuandikisha wapiga kura, mashine za kutambua wapiga kura siku
ya uchaguzi na kadhalika.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana
na tume kukosa mashine hizo imeamua kupunguza siku za kuandikisha wapiga kura kutoka
14 za awali na sasa wanaandikisha kwa siku 7 tu kwa kituo jambo ambalo limeanza
kuwa na madhara kwani wapiga kura wengi wanaachwa bila kuandikishwa. Mfano
mzuri ni Wilayani Namtumbo ambako mkandarasi aliyepewa jukumu la kubeba vifaa
alihamisha bila kujali kuwa kuna wananchi ambao walikuwa kwenye misururu ya
foleni vituoni humo.
Mheshimiwa Spika,
Tume pia haijatoa taarifa juu ya vituo vya kuandikishia
wapiga kura na idadi ya wapiga kura inayotegemea kuandikisha kila kata. Katika
zoezi la majaribio la uandikishaji wapiga kura katika Jimbo la Kawe wilaya ya
Kinondoni, Tume iliandikisha wapigakura katika kata ya Bunju na Mbweni. Katika
kata hizo Tume iliandikisha wapigakura 15,123 na kuvuka lengo iliyojiwekea la
wapiga kura 14,312 kwa karibu asilimia 6. Hata hivyo matokeo ya Takwimu za
Sensa ya watu ya mwaka 2012 yanaonesha kuwa kata ya Bunju ina wakazi wenye sifa
za kuwa wapiga kura 42,227 na Mbweni wapigakura 9,650. Idadi hii haijajumlisha
watu waliohamia maeneo hayo baada ya sensa. Walioandikishwa katika kata mbili
za Kawe ni chini ya asilimia 30 ya wapigakura wanaostahiki kuandikishwa.
Mheshimiwa Spika,
Siku 7 hazitoshi kuandikisha wapiga kura wote kwa kila
kata, na hasa ikizingatiwa kuwa Tume inaandikisha wapiga kura msimu wa masika
wakati wananchi wengi wako katika shughuli za kilimo na vituo viko nje hivyo
kuathiri utendaji kazi. Kwa hiyo muda wa
ziada unahitajika kuwaandikisha.
Matatizo yanayojitokeza katika zoezi la uandikishaji
wapiga kura yanaonesha wazi kuwa daftari la wapiga kura halitakamilika ili
litumiwe katika zoezi la Uchaguzi Mkuu. Ni vyema Waziri Mkuu na Serikali mkakubali
ukweli huu kuwa bila mkakati wa makusudi wa kuiwezesha na kuisimamia Tume ya
Taifa ya Uchaguzi , hakuna uchaguzi Octoba.
Mheshimiwa Spika,
Kama kuna jambo litawasha nchi hii ni mkakati wowote wa
kujaribu kuongeza muda wa kuwepo madarakani Serikali ya awamu ya nne. Chaguzi
kwa mujibu wa Katiba siyo jambo la kuchezea hata kidogo. Tume na Serikali
zimekuwa zikitoa majibu mepesi tena wakati mwingine ya kejeli kwa maswali
magumu. Ni dhahiri, tume imetumika kama “mshirika na msiri” wa Serikali. Tume
inajua uchafu na ufisadi mwingi unaogubika uagizaji na uingizaji wa BVR kits
lakini imeendelea kudumisha siri hii.
Kuhairisha uchaguzi kwa uzembe wa aina hii haikubaliki.
Ni vyema Bunge lako likajadili kwa kina ratiba ya uchaguzi mwaka huu na wote
waliozembea na kulisababishia Taifa hofu ya kiwango hiki wawajibishwe haraka.
Aidha, tume nzima ya uchaguzi ijitafakari kama kweli ina weledi wa kuendelea
kuwepo na kusimamia uchaguzi mkuu ujao bila kusababisha machafuko makubwa
nchini,
Mheshimiwa Spika,
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ,Tulisema kuwa kura ya maoni haitawezekana kufanyika tarehe 30 mwezi
Aprili , lakini serikali na tume hii hii iliendelea kutubeza. Rais, Waziri Mkuu,
Mawaziri na hata Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi waliendelea kusisitiza kuwa
kura ya maoni ya Katiba pendekezwa itafanyika. Tarehe 30 Aprili kura ya maoni haikufanyika
na haijulikani hatma yake. Fedha za walipa kodi zimepotea kwa mabilioni. Hakuna
aliyewajibika.... huo ndiyo utawala wa Rais Kikwete. Hii ndiyo CCM.
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kupata majibu kutoka serikali hii ya CCM kwenye
mambo yafuatayo;
i.
Mashine za BVR zitawasili lini nchini
kwa ukamilifu wake?
ii.
Tume itamaliza lini (tarehe)
kuwaandikisha Watanzania wote wenye sifa ya kuwa wapiga kura katika Daftari la
wapiga kura?
iii.
Ni lini Watanzania ambao watakuwa
wameandikishwa kwenye Daftari la wapiga kura watapata fursa ya kuhakiki Daftari
la wapiga kura kwa mujibu wa sharia na zoezi hili litachukua muda gani?
iv.
Je, Tume itaweza kufanya maandalizi mengine
ya kina ya uchaguzi Mkuu na ikizingatiwa kuwa muda wote itakuwa inaendelea
kuandikisha wapiga kura?
v.
Tume itaweka lini hadharani mpango
mzima na ratiba za utekelezaji kuelekea uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Octoba 2015
ambapo kwa mujibu wa sharia zimebaki siku pungufu ya 100 kwa kampeni za
uchaguzi kuanza.
3.3 Mpango haramu wa Tume: Watanzania
2.9 milioni kutokuandikishwa:
Mheshimiwa Spika,
Kutokana
na kukosekana kwa muda na vifaa vya kutosha kwa ajili ya kuandikisha wapiga
kura wote wenye sifa kwa mfumo wa BVR , Tume imeshaamua kwa makusudi
kutokuwaandikisha wapiga kura zaidi ya milioni
2.9 katika zoezi linaloendelea. Hii ni kwa mujibu wa taarifa rasmi za Tume
ya Taifa ya Uchaguzi iliyoko kwenye Randama yake. Nanukuu uk.10 ‘Tume
ya Taifa ya Uchaguzi inakadiria kuandikisha wapiga kura 21 milioni kati ya
watanzania 23.9 milioni wenye sifa za kuwa wapiga kura, kulingana na Takwimu za
Sensa ya watu na Makazi ya Mwaka 2012. Makisio ya wapiga kura inazingatia wale
ambao hawatajiandikisha kutokana na Voter Apathy’
Mheshimiwa Spika,
Tafsiri
ya kuwaacha bila kuwaandikisha Watanzania 2.9
Milioni kama Tume inavyosema kwenye randama yake kwa hoja ya ‘Voter Apathy’, maana yake ni sawa na
kuacha mikoa zaidi ya sita ya Tanganyika bila kumwandikisha mwananchi hata
mmoja. Mikoa hiyo (kwenye mabano ni takwimu za wenye sifa za kuandikishwa kwa
mujibu wa sensa ya 2012) Lindi (0.518
milioni), Singida (0.698 milioni),
Njombe (0.392 milioni), Katavi (0.271 milioni), Rukwa (0.472 milioni) na Iringa (0.524 milioni).
Mheshimiwa Spika,
Tume
inataka kuhalalisha kuacha kuandikisha Watanzania wengi kiasi hicho kwa hoja
dhaifu kama hiyo? Kazi ya Tume ni kuwaandikisha Watanzania wote wenye sifa na
hivyo basi Tume inatakiwa kuhakikisha kuwa inatoa elimu kwa umma, hamasa na umuhimu wa kujiandikisha katika Daftari
la Kudumu la wapiga kura kwa Watanzania na sio kukaa kimya bila kufanya
matangazo ya kina ya kuwahamasisha wananchi kama wanavyofanya sasa na kuishia
kujificha kwenye kichaka cha ‘Voter Apathy’
hali hii haikubaliki hata kidogo.
Kambi Rasmi ya Upinzani,
tunataka kujua kutoka serikalini Tume imetumia kigezo gani cha kusema kuwa
zaidi ya asilimia 12.1 ya Watanzania wote wenye sifa za kuandikishwa kuwa
wapiga kura hawatajiandikisha mwaka huu? Imefanya utafiti huo lini, na ripoti
yake iko wapi? Au huu ni mkakati wa makusudi ambao unaoratibiwa na serikali ya CCM na Tume wa kupunguza wapiga
kura baada ya Tume kutokupewa vifaa
vya kutosha kwa ajili ya kuwaandikisha watu
wote wenye sifa?
Ama
huu ndio mpango mzima wa hujuma ambao
unaendana sambamba na kupunguza muda wa kuwaandikisha wapiga kura kutoka siku
14 kama ilivyokuwa imepangwa awali na kuwa siku 7 za sasa ?
Aidha, tunaitaka
serikali kutoa majibu ya kina imejipanga vipi katika kuwahamasisha,
kuwaelimisha na hatimaye kuwaandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura
Watanzania wote wenye sifa za kuandikishwa kwa muda wa siku saba ambazo tume
imeweka kwa kila kituo?
3.4 Takwimu za Tume ni Utata Mtupu:
Mheshimiwa Spika,
Kwa
Mujibu wa Takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni kuwa uchaguzi Mkuu wa mwaka
2005 Watanzania waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 16.4 Milioni na waliojitokeza kupiga kura walikuwa 11.3 milioni, Uchaguzi Mkuu wa Mwaka
2010 walijiandikisha watanzania 20.1
Milioni na waliopiga kura walikuwa 8.3
Milioni .
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
inataka majibu ya swali hili, Tume inaposema kuwa Mwaka 2015 itaandikisha
wapiga kura 21 Milioni , maana yake
ni kuwa tangu mwaka 2009 ambapo ndio ilikuwa mara ya mwisho kuandikisha wapiga
kura, watanzania ambao umri wao umeongezeka na hivyo kuwa na sifa za kuandikishwa
kwenye Daftari ni 0.9 Milioni tu au kuna mchezo mchafu ambao
umepangwa kuchezwa na Tume ikishirikiana na Serikali ya CCM? Ama serikali na
Tume inataka kusema kuwa tangu 2009 Watanzania ambao walikuwa wamejiandikisha wamefariki dunia na hivyo kufanya idadi ya watu wenye za kujiandikisha kuwa
kiasi hicho?
4.
MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU ,2015.
4.1 Tume haijapewa fedha kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi Mkuu.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na ukweli kuwa muda haupo upande wetu lakini mpaka
sasa hakuna maandalizi yoyote ambayo yamefanyika na yenye kuashiria kuwa
uchaguzi mkuu unaweza kufanyika mwezi Octoba,2015 kwa mujibu wa Katiba .Ukweli
huu umethibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwenye randama yao
walipoandika, nanukuu uk.13 ‘Kwa upande wa Maandalizi ya Kura ya Maoni
na Uchaguzi Mkuu,2015 Tume hatujapokea fedha hadi sasa’
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inajiuliza Kama serikali haijaipatia Tume fedha kwa ajili ya maandalizi ya
Uchaguzi Mkuu, wanategemea miujiza gani kuwa ifikapo Octoba uchaguzi Mkuu
utafanyika? Ni lini Zabuni zitatangazwa kwa ajili ya wakandarasi mbalimbali
ambao watasambaza vifaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu, na tarehe ya kuwapata hao
wazabuni ni lini ?
Mheshimiwa Spika,
Wakati Serikali hii ikishindwa kuipatia fedha Tume ya
Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu Octoba, 2015
ili uweze kufanyika katika mazingira ya amani, haki na utulivu, Serikali hii ya CCM imeamua kuwekeza na kujiandaa
kupambana na wananchi wake, hii ni kutokana
na ukweli kuwa ,wakati Tume inakosa fedha za kulipia vifaa kwa ajili ya
kuandikisha wapiga kura na kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu , tuna taarifa
kuwa Serikali imeamua kuagiza zaidi ya magari
777 kwa ajili ya Jeshi la Polisi, kuanzia yale ya Maji ya kuwasha, Doria na
shughuli za Ukaguzi katika Mwaka huu wa Fedha.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni , inajiuliza kwamba hivi ni nini kipaumbele chetu kama
taifa kwa sasa? Je, ni kuandaa mazingira ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu kwa
hali ya haki, amani na utulivu? Au ni kujiandaa kuuvuruga uchaguzi huo? Ndiyo
maana tunashuhudia jitihada hizi za kujiandaa kupambana na wananchi wakati uchaguzi
Mkuu utakaposhindikana kufanyika kwa sababu ya kukosekana kwa maandalizi
thabiti na ya kina ya kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi huo? Na hizo ndio sababu
za serikali hii ya CCM kukataa kufanya maandalizi ya kina kwa ajili ya Uchaguzi
Mkuu na kuwekeza katika Mapambano?
4.2 Aibu ya Tume na Madeni :
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na Tume ya Uchaguzi kutokupewa fedha kwa ajili ya
maandalizi ya Uchaguzi Mkuu na Serikali hii ya CCM , bado Tume wanadaiwa madeni
na wakandarasi ambao walisambaza vifaa
kwa tume kwenye Chaguzi mbalimbali zilizopita, madeni hayo ya Tume yanathibitishwa
na maandishi ya Tume kwenye randama yao uk .13 nanukuu ‘Hata hivyo kuna Wazabuni
waliotoa huduma ambao wanatudai fedha kiasi cha USD 8,377,134.56.....’ Hizi
ni sawa na Shilingi Bilioni 16.754
kwa viwango vya bei ya soko leo kutokana na kudorora kwa shilingi, laiti kama deni
hilo lingeweza kulipwa mapema kabla ya Shilingi kudorora na kuporomoka tusingekuwa
na deni kubwa kiasi hiki leo hii.
Aidha kutokana na Tume kudaiwa kiasi hicho cha fedha
wakandarasi wameshindwa kuiamini tume na ndio maana haikopesheki tena na hivyo
kushindwa hata kuanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu Octoba 2015, kwa njia ya
Mkopo,hawana pa kukopa!
Mheshimiwa Spika,
Ukiangalia Jedwali
Na:4 Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Mwaka 2015/16 kwenye randama ya
Tume utaona kuwa fedha iliyoombwa ni kiasi cha shilingi 192.409 Bilioni, na fedha hizo zimeombwa kwa ajili ya Mishahara 2.144 bilioni, Matumizi mengineyo 2.302 bilioni na kiasi cha shilingi 187.962 bilioni kwa ajili ya
uendeshaji wa Uchaguzi Mkuu.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inauliza hivi deni la zaidi ya bilioni
16 ambazo tume inadaiwa na wakandarasi hazitalipwa mwaka huu wa Fedha? Na
kama zitalipwa zitatoka fungu gani hasa ikizingatiwa kuwa tayari Tume imeshatoa
rai kuwa fedha zake ziwekwe kwenye Fungu
61 na sio Mfuko Mkuu wa Hazina ambao ulikuwa ukitumika kama kichaka cha
kuficha ukweli katika bajeti zilizopita.
4.3 Fedha za Uendeshaji Uchaguzi Mkuu hazina Mchanganuo:
Mheshimiwa Spika,
Tume ya Taifa ya uchaguzi wameomba kupatiwa kiasi cha
shilingi 187.962 Bilioni kwa ajili
ya uendeshaji wa Uchaguzi ambao unapaswa kufanyika Octoba ,2015 kwa mujibu wa Katiba
yetu, fedha hizi hazina maelezo wala mchanganuo wake kuwa zinaombwa kwa ajili
ya kulipia kitu gani hasa , ni Mawakala ,vifaa vya uchaguzi au ni kwa ajili ya
kulipia posho kwa wasimamizi wa uchaguzi huo?
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupatiwa mchanganuo wa kasma
229914 :Uendeshaji wa Uchaguzi Mkuu kiasi cha sh.187,962,160,000
hizi ni fedha kwa ajili ya vitu gani na hasa ikizingatiwa kuwa Tume
haijatangaza zabuni kwa ajili ya vifaa vya Uchaguzi Mkuu, wamekokotoa kiwango
hicho kutokana na msingi upi? Au wamefanya mazoea ? wamezingatia kiwango cha
kuporomoka kwa shilingi na hasa kwa vifaa ambavyo tutalazimika kuagiza kutoka
nje ya Nchi ?
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa randama ya Tume imeonyesha kuwa Tume tayari
imeshafanyia maboresho sheria na kanuni za uchaguzi, na hiyo ipo uk 12 wa
randama , naomba kunukuu ...’imeanza pia kufanya Maboresho ya Sheria
na Kanuni za Uchaguzi...’ Kambi rasmi ya Upinzani inataka kujua ni lini
sheria hizo zitawasilishwa Bungeni? kwani kwa mujibu wa Katiba chombo chenye mamlaka ya Kuboresha ama kubadilisha sheria ni
Bunge na sio chombo kingine chochote kile , na hasa ikizingatiwa kuwa hili ni
Bunge la Bajeti na la mwisho kabla ya uchaguzi Mkuu Octoba 2015. Maboresho hayo
ya sheria yatafanyika wapi na kupitishwa lini ?
Mheshimiwa Spika,
Tume pia imeonyesha kwenye randama yake kuwa kuna mpango
wa kupitia upya mipaka na majina ya majimbo ya Uchaguzi , nanukuu randama uk.12
.....’kupitia
mipaka na majina ya Majimbo ya Uchaguzi na kuyarekebisha ....’ Kambi
rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata majibu ni majimbo yapi ambayo
yatahusika na mpango huu wa Tume na hasa ikizingatiwa kuwa tayari vyama
vimeshaanza michakato yake ya ndani ya kutafuta na kuteua wagombea wa nafasi za
Udiwani, Ubunge,Uwakilishi na Urais. Ni vyema Tume ikayatangaza mapema Majimbo
hayo ili wananchi pamoja na wadau wa uchaguzi (Vyama vya siasa) wakapata muda
wa kutosha wa kujiandaa na hasa kuandaa wagombea katika Majimbo hayo.
Kambi rasmi ya Upinzani , inakubaliana na rai ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama ilivyo kwenye
randama yake uk.14 nanukuu ‘Fedha kwa ajili ya shughuli za Uchaguzi
ziwekwe kwenye Fungu 61 badala ya kuwekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina, ili
kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kulingana na Ratiba’ Kwani ni
ukweli uliowazi kuwa Mfuko Mkuu wa Hazina umekuwa kama kichaka cha kuficha
mambo na hasa ikizingatiwa kuwa hata bajeti ya mwaka 2014/2015 Kambi rasmi ya
Upinzani tulipohoji ziko wapi fedha za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu tuliambiwa
kuwa ziko Mfuko Mkuu wa Hazina jambo ambalo halikuwa kweli na ndio maana Tume
haijapewa hata senti moja kwa ajili ya Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa octoba
2015 .
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni , inaitaka serikali
kufuata ushauri wa Tume ya Uchaguzi wa kuhakikisha kuwa haiongezi maeneo ya
utawala tunapokaribia Uchaguzi kwani kunaifanya Tume kushindwa kupanga mipango
yake katika kuandaa uchaguzi Mkuu .
5.
KURA YA MAONI
5.1 Kura ya maoni haipo kwa mujibu wa sheria ;
Mheshimiwa Spika ,
Pamoja na utamaduni wa Serikali hii wa kuvunja sheria
zilizotungwa na Bunge lako kuwa ni jambo la kawaida , tumeshuhudia kuvunjwa kwa
sheria ya kura ya maoni kwa kiwango ambacho hakivumiliki tena .Hali hiyo
imeipelekea hata Tume ya Uchaguzi kushindwa kuendela kuvumilia uvunjwaji huu wa
sheria unaofanywa na serikali hii ya CCM na ndio maana sasa wameamua kuuweka
ukweli hadharani na kwa sauti kuu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa randama, Tume iliandaa swali la kura ya
maoni kama sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 ilivyowataka kufanya tangu
Octoba, 2014. Na Tume imesema hivyo kwa mujibu wa nyaraka zake kwa Bunge, naomba kunukuu tena Randama ya Tume ya
Uchaguzi uk.12 ‘Tume tayari zimekutana na kuandaa swali la Kura ya Maoni na
kulichapisha kwenye gazeti la serikali la
tarehe 17 Octoba,2014’..
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 ,
iliyotungwa na Bunge hili iliweka bayana
muda maalum wa kuchapisha swali la kura ya maoni, kutoa elimu kwa umma na siku
ya kufanyika kwa kura ya maoni. Kwa masikitiko ni kuwa muda wa kufanya yote
hayo kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni umeshapita tayari.
Mheshimiwa Spika,
Sasa ni dhahiri na ni ukweli mtupu kwa mujibu wa sheria
ya kura ya maoni kuwa , Haiwezekani tena
kwa kura ya maoni kufanyika sasa au baadaye bila kwanza sheria ya kura ya maoni
ya mwaka 2013 kuletwa hapa Bungeni kwa ajili ya kurekebishwa ili kuruhusu kura hiyo
ya maoni kufanyika .
5.2 Elimu kwa Umma juu ya kura ya Maoni ni utata mtupu:
Mheshimiwa Spika,
Jukumu la kutoa elimu kwa umma kuhusu kura ya maoni ni
jukumu la Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na asasi ambazo zimeidhinishwa na
Tume kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni, na sio jukumu la Serikali .
Mheshimiwa Spika,
Kwa kipindi kirefu sasa tumeshuhudia kwenye baadhi ya vyombo
vya habari na hasa Magazeti, Redio na Television wakiendelea na vipindi vya
elimu juu ya kura ya maoni na msisistizo mkubwa ni kupiga kura ya ndiyo ya
Katiba Pendekezwa , na hata kwenye maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano kwaya ya
vyombo vya dola ambayo ilishirikisha Jeshi, Polisi na usalama wa Taifa , na wao
kwenye wimbo wao ambao waliimba mbele ya Rais Kikwete waliweka msisitizo wa kupiga
kura ya ndiyo kwenye katiba pendekezwa, ilihali hivi ni vyombo vya dola na
ambao havipaswi kufanya kazi hiyo ya kushawishi umma kufanya uamuzi ambao
wanautaka wao na walioandaa kwaya hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Hatujashangazwa na taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi
iliyoko kwenye randama yake kuwa haijawahi kupokea fedha kwa ajili ya kuendesha
zoezi la kura ya maoni ,na hii ni kutokana na ukweli kuwa kura hiyo ya maoni
haiwezekani kufanyika kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni, na hii inathibitishwa na randama ya Tume ambao
uk 12 wanasema kuwa, naomba kunukuu ‘kwa upande wa maandalizi ya kura ya maoni
na Uchaguzi Mkuu, 2015 Tume hatujapokea fedha hadi sasa’ .
Mheshimiwa Spika,
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,inataka kufahamu ni nani anayegharimikia gharama za matangazo hayo na fedha
hizo zimetoka kwenye kasma au fungu lipi la bajeti?Je? anayefanya kazi hiyo
amesajiliwa na Tume kwa mujibu wa sheria ? Na kama siyo ni kwanini Tume
imeendelea kukaa kimya huku sheria ya kura ya maoni ikiendelea kuvunjwa ? Ofisi
ya Waziri Mkuu imeshachukua hatua gani mpaka sasa kuzuia uvunjwaji huo wa
sheria ya kura ya maoni?
5.3 Sherehe za Muungano wa miaka 51 na Kura ya Maoni ya
Katiba :
Mheshimiwa Spika,
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Tunajiuliza , hivi wale waliokuwa kwenye ile kwaya iliyokuwa uwanja wa
Taifa na kutambulishwa kuwa ni kutoka vyombo vya dola , bado ni askari wetu na
ambao tunategemea kuwa sehemu ya kusimamia haki kama hiyo kura ya maoni itafanyika
? Serikali imeweka utaratibu gani wa kuhakikisha kuwa wale wote ambao waliweka
msimamo wao hadharani kuwa kura ya maoni ni lazima kila mwananchi akapige kura ya ndiyo; kama walivyoimba
uwanja wa taifa; wanaondolewa kwenye utaratibu mzima wa kuwa sehemu ya
wasimamizi wa kura ya maoni? Haki iko wapi kama hawa ndio vyombo vyetu vya
dola, ambao wanaopaswa kutokufungamana na upande wowote wa kisiasa kwa mujibu
wa sheria ?
5.4 Tume ya Uchaguzi imeweka msimamo kuwa Hakuna kura ya Maoni bila sheria
kurekebishwa na Bunge :
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na madhaifu yote ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ,
kuna jambo moja ambalo walau Tume wamekubaliana nasi kama Kambi rasmi ya
Upinzani Bungeni , wananchi, wanaharakati na viongozi wetu wa dini na hasa
Shura ya Maimamu na wale wa Kikristo, nalo ni kuhusu ‘kutokuwezekana kufanyika kwa kura
ya maoni katika wakati huu kutokana na sababu za kuvunjwa na
ama kuwa na sheria ambayo haieleweki na haitekelezeki.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa randama ya Tume uk 14, nanukuu kipengele cha
2.6 kuhusu Changamoto , wamesema kuwa ‘Sheria ya kura ya maoni ina maeneo ambayo
hayawezi kutekelezeka na baadhi yake kuwa na tafsiri zaidi ya moja .Eneo ambalo
linaweza kuleta utata ni Uhesabuji wa Kura ya Maoni na Utangazaji wa Matokeo’
Mheshimiwa Spika,
Tume Imependekeza kuwa ili kura ya maoni iweze kufanyika
ni lazima sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 irekebishwe kwanza na Bunge ,
kifungu cha 2.7 cha randama, suluhisho la Changamoto uk 14 kinaeleza kuwa ili
kura hiyo iweze kufanyika ni lazima ‘Sheria ya Kura ya Maoni ifanyiwe
Marekebisho kwenye maeneo ambayo hayatekelezeki au kuwa na tafsiri zaidi ya
moja’
Mheshimiwa Spika,
Huu ni ukweli mchungu ambao Bunge hili linapaswa
kuuchukua kwani Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, tumekuwa tukilalamika juu ya utaratibu
wa Bunge na ambavyo tumekuwa tukitunga sheria zetu mbalimbali hapa Bungeni japo
mapendekezo yetu yamekuwa yakitupwa au kutokusikilizwa kutokana na mantiki yake
na madhara yake ni haya ya kutunga sheria ambazo hazitekelezeki , mbovu na ni
aibu kwenu ambao mara zote mmekuwa mkipiga kura
za Ndiyo bila kujali hoja yenyewe , hii ni aibu kubwa kwenu na
mmelisababishia taifa aibu kubwa!
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni , inakubaliana na ukweli huu kuwa kura ya maoni haiwezi kuwepo mwaka huu
wa fedha bila kwanza sheria kurekebishwa Bungeni na ndio maana hata kwenye
maombi ya fedha yaliyoletwa na Tume katika mwaka huu wa fedha 2015/2016 haikuomba kiasi chochote cha fedha kwa ajili
ya kura ya maoni
5.5 Msimamo wa Tume, hakuna kura ya
maoni ni wa Kikatiba na uheshimiwe !
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Katiba yetu ibara ya 74 (7) imeweka wazi
kuwa Tume ya Uchaguzi ni idara huru inayojitegemea ,itafanya maamuzi yake rasmi
kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa vikao vyake .
Kwa mujibu wa Katiba ibara ya 74(11)imeweka wazi kuwa “katika
kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa masharti ya katiba hii,Tume ya Uchaguzi
haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya serikali
, au maoni ya chama chochote cha siasa”
Hivyo basi ni imani ya Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa , kwa kuwa Tume ya Uchaguzi imeshakaa kwenye Vikao
vyake kwa mujibu wa Katiba na kuweka wazi vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha
2015/16 ambavyo vinapatikana kwenye randama yake uk 15 . Kura ya maoni siyo moja
ya vipaumbele vyake kwa mwaka huu wa fedha , Hivyo basi ni imani yetu kuwa viongozi
wa serikali na CCM wataheshimu maamuzi haya ya Tume na kamwe hawataiingilia
Tume katika kutekeleza vipaumbele vyake kwa mujibu wa Katiba kama ilivyojiwekea
katika mwaka huu wa fedha .
Hatutaki
kuamini kuwa Waziri Mkuu anaweza kuendelea kuwa sehemu ya kuvunja Katiba na
kulazimisha kura ya maoni ambayo hata hivyo kwa upande wa Zanzibar hata sheria
ya kura ya maoni haijawahi kujadiliwa na kupitishwa na Baraza la wawakilishi, na
hata kama ingepitishwa tunategemea kuwa wananchi wa Zanzibar wafanye kura ya
maoni ili kuruhusu kura hiyo kufanyika kwa upande wa Zanzibar kwa Mujibu wa
katiba yao kama ilivyorekebishwa mwaka 2010.
6. MAPITIO YA BAJETI YA SERIKALI
MWAKA 2014/15 NA UTEKELEZAJI WAKE.
6.1 FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO.
Mheshimiwa Spika,
Kwa
mujibu wa randama za wizara na idara mbalimbali za Serikali ni kuwa Fedha
zilizoidhinishwa na Bunge hili kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwa
mwaka wa fedha 2014/15 zimetolewa chini ya kiwango cha asilimia 40 na maeneo
mengine kukosa kabisa fedha kwa ajili ya miradi iliyokuwa imeidhinishiwa bajeti
na Bunge hili.
Eneo
linaloonekana kupokea fedha yote iliyopitishwa na Bunge kwa ajili ya Maendeleo
kwa asilimia 100 ni fungu 30 Ofisi ya Rais Ikulu eneo la ‘Ukarabati Ikulu’ ambapo zilidhinishwa jumla ya shilingi bilioni 10
na zote zilikuwa zimeshatolewa na Hazina na kutumika hadi mwezi Machi, 2015
Mheshimiwa Spika,
Maeneo
muhimu kama Vile fungu 40 Mahakama ya
Tanzania iliyokuwa imeidhinishiwa na Bunge hili jumla ya shilingi bilioni
40 walikuwa hawajapewa hata senti moja na Hazina kwa ajili ya maendeleo hadi
mwezi Aprili ,2015 .
Maeneo
mengine ambayo yaliidhinishiwa fedha na ambayo yalikuwa hayajapokea ni pamoja
na fungu 16 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliyoidhinishiwa bilioni 5,
fungu 41 wizara ya sheria na Katiba ,Fungu 37 Ofisi ya Waziri Mkuu ,Idara ya
Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali iliyoidhinishiwa Bilioni 1.
Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, inataka kupata majibu ya Kina ni kwanini maeneo
muhimu kama Mahakama hayakupatiwa fedha zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge
hili? Hivi kipaumbele chetu ni kukarabati Ikulu kwanza au ni kuziwezesha
Mahakama zetu kuwa bora na ili haki iweze kutendeka kwa wananchi wetu? Ni lini
serikali itaweka utamaduni wa kuheshimu muhimili huu muhimu wa Dola?
Kama
bajeti ya mwaka wa fedha ulioisha haikutekelezwa, hivi kuna maana gani kwa
Bunge hili kuendelea kukaa hapa kwa gharama za walipa kodi kupitisha Bajeti
ambayo mwisho wa siku haitatekelezwa na serikali hii ya CCM? Waziri Mkuu
unaisimamia serikali ambayo haiheshimu maamuzi ya Bunge ?
7. BAJETI YA SERIKALI 2015/16 NA
HALI YA UCHUMI WA TAIFA.
Mheshimiwa Spika,
Serikali
ya CCM ili kuweza kupata fedha ambazo imeweka kwenye bajeti yake imeamua kukopa
katika mabenki ya Ndani karibia shilingi Trilioni 6, maana ya hatua hii ya
serikali ni kuwa itapunguza mzunguko wa pesa ambazo mabenki ya kibiashara,
yangekopesha sekta binafsi kwa ajili ya uzalishaji na biashara ambayo ni muhimu
kwa ukuwaji wa uchumi na ajira.
Badala yake hizo pesa sasa zinapelekwa
serikalini zikatumilke kulipia matumizi ya kawaida yasiyo ya maendeleo. Kwa maneno mengine Serikali imeamua kuiua
Sekta binafsi kwa kuweka ushindani wa moja kwa moja kwenye kugombania mikopo
kutoka kwenye mabenki ya ndani.
Mheshimiwa Spika ,
Hali
hii inatokana na serikali kutumia zaidi
ya uwezo /kipato chake! NI hali ambayo itaenda kuongeza deni la ndani na hii
inatokana na serikali kushindwa kupata au kukopa fedha toka kwa mabenki na
wafadhili wa nje (Development partners) kutokana na mahusiano mabaya na hasa
yaliyosababishwa na kukithiri kwa vitendo vya kifisadi .
Mheshimiwa Spika,
Madhara
mengine ya hatua hii ya serikali ni Riba kupanda kwa wakopaji kutoka sekta binafsi
maana umepunguza fedha kwenye mabenki na hivyo kufuatia mahitaji, bei za mikopo
(riba) zinaweza kupanda japo hata sasa ziko juu sana, na kumekuwa na malalamiko
mengi toka sekta binafisi kwamba riba za mikopo kwa ajili ya uzalishaji na
uwekezaji ziko juu. Hii itapelekea mambo kuwa magumu zaidi na zaidi kwa
wakopaji wa ndani.
Mheshimiwa spika ,
Kwa miaka
ya siku za karibuni, nchi yetu imekuwa na utamaduni wa kukopa kutoka mfumo wa kibenki (Benki Kuu na Benki za
Biashara) kama njia ya uhakika ya kufidia nakisi ya bajeti yake . Ukopaji huu si tu unadidimiza ukuaji wa sekta
za uwekezaji na uzalishaji kama ilivyoelezwa hapo juu, bali pia unaipa Benki
Kuu wakati mgumu wa kusimamia ujazi wa fedha katika uchumi. Pia, kupanda kwa
riba kutokana na mabenki kuwa na fedha kidogo kunaweza kusababisha sekta zisizokuwa
na uwezo wa “ku-break even” kwa muda mfupi hasa sekta ya kilimo na viwanda kudidimia zaidi.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana
na ‘risk’ na gharama ya mabenki kukopesha sekta binafsi ni wazi kuwa mabenki
mengi yatapendelea kukopesha serikali kwa kuwa ‘risk’ ya kupoteza ni ndogo
sana. Na kwa kuwa tofauti kati ya riba zinazotolewa kwenye akiba ni kidogo
kuliko zinazotolewa na serikali kwenye uwekezaji wa hati fungani, mabenki mengi
kwa kuwa ‘risk averse’ zitawekeza kwenye hati fungani za serikali. Haya ni mabenki,
mbali na kuwa na riba za juu zimekuwa zikisita kukopesha sekta binafsi kwa kuhofia
usalama, hivyo hapa zitapata mteremko wenye gurantee ya usalama.
Mheshimiwa Spika ,
Kutokana
na Serikali kukopa kwenye mabenki binafsi katika riba ya soko (isiyo na unafuu)
ili kujalipa baadae, hiyo itapelekea deni la serikali kueindelea kuwa kubwa,
jambo ambalo halitakuwa tu msalaba kwa Taifa na Watanzania, bali deni hilo
litawaogopesha wawekezaji na wakopeshaji wa nje kama serikali ita-default
katika urejeshaji wa mikopo hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Ni kweli kuwa
kwa mujibu wa takwimu, Uchumi unakua na kwa sasa ni takribani asilimia 7,
lakini umasikini umebakia pale; inequality imeongezeka na ajira hasa kwa vijana
zimepungua sana. Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Wizara ya Fedha na
Benki ya Dunia inaonyesha umasikini bado uko juu kwani umepungua kidogo sana
toka asilimia 34 mwaka 2007 mpaka asilimia 28 mwaka 2012, na umebadilika kwani
masikini wengi wa vijijini wanahamia mijini. Hizi takwimu za serikali
zikifanyiwa uchambuzi huru hali ya umasikni na inequlity unaweza kuwa mbaya
zaidi. Kwa ufupi, matunda yanaliwa na wachache walioko kwenye sekta zinazokua
zaidi (utalii, biashara, madini, viwanda, etc.) wale walioko kwenye sekta ya
kilimo cha jembe la mkono (75%) inayokua taratibu ukilinganisha na ukuaji wa
jumla, wana njia ndefu ya kwenda, umaskini unakithiri!
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kupata majibu ya kina
serikali imejipanga vipi kuondokana na utaratibu huu wa kuwa na bajeti kubwa
kwenye makaratasi wakati kiuhalisia haina uwezo wa kuitekeleza bajeti hiyo?
Aidha, kuna
mkakati gani wa kuhakikisha kuwa inawanusuru wawekezaji wa ndani na riba kubwa
kutokana na serikali kuamua kukopa kwenye sekta za ndani za fedha ? Ofisi ya
Waziri Mkuu ina mikakati gani ya kukuza ajira na kuwezesha sekta binafsi kuweza
kuzalisha?
8. MAMLAKA YA USTAWISHAJI MAKAO
MAKUU-CDA
Mheshimiwa Spika,
CDA
ni mamlaka ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 1972 na hivi sasa ina umri wa miaka
43 katika utendaji kazi wake wa jukumu la kwanza lilikuwa ni kuhakikisha kuwa Mji
wa DODOMA ardhi yake yote imepimwa.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa
mujibu wa Randama Fungu 37 Uk. 126
inaonesha kuwa kwa mwaka wa fedha 2014/15 mamlaka kupitia Mradi wa
Uboreshaji Miji(TSCP) ilitengewa jumla ya Tshs.206,744,000/- kwa ajili ya
kujenga uwezo wa Taasisi. Kambi Rasmi ya Upinzani inajiuliza Taasisi yenye
miaka 43 na ambayo inakusanya kodi za nyumba na viwanja kwa muda wote huo
inapokeaje fedha za kujengewa uwezo?
Mheshimiwa Spika,
CDA
kama mamlaka ya kuendeleza makao makuu imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa wakazi
wa Mji wa DODOMA, kwa zaidi ya miaka 42 ya uwepo wake, Mamlaka haijakamilisha
jukumu lake la kwanza la kupima viwanja maeneo yote ya mji ili kufanya ujenzi
ufuate utaratibu utakao wekwa.
Mheshimiwa Spika,
Kabla
ya CDA kuanzishwa na baada ya kuanzishwa, wananchi wa Dodoma walikuwa wanaishi
katika maeneo yao na wanaendelea kujenga na kuishi kwa sababu hakuna mipaka ya
ardhi iliyowekwa na CDA. Lakini CDA wanapotaka kupima eneo Fulani ambalo tayari
lina makazi ya wananchi hutoa notice na kuwataka wakaazi wa eneo husika kubomoa
nyumba zao wenyewe bila ya fidia.
Mheshimiwa Spika,
Inapotokea
wananchi wanaposhindwa kubomoa nyumba hizo kutokana na kukosa mahali pa kwenda
,CDA hubomoa na kuwadai wananchi hao gharama za kubomoa nyumba zao. Maeneo
ambayo yamebomolewa nyumba zao na CDA ni pamoja na : Ndejengwa mwaka 2012
ambapo zilibomolewa nyumba 127, Eneo la Itega mwaka 2013, Msangalalee kata ya
Makaru mwaka 2014 nyumba 35 n.k.
Kambi rasmi ya
Upinzani Bungeni, inataka kujua ni lini uonevu huu
kwa wananchi wa Dodoma utasitishwa na serikali hii ya CCM? Maana wimbo wa Makao
makuu kuwa Dodoma unaonekana umekosa mchezaji na mamlaka hii haionekani ikiwa
tayari kufanya jukumu lake la msingi la kuanzishwa kwake .
9. IDARA YA MPIGA CHAPA MKUU WA
SERIKALI
Mheshimiwa Spika,
Idara
hii ni idara muhimu sana kama ingetumika vyema na kama Serikali ingekuwa na
nidhamu ya kutokuingilia utendaji wa Idara ambazo ziko chini yake. Kwani
gharama kubwa zinazoingiwa na taasisi na Idara za Serikali katika kuchapa
nyaraka mbalimbli ni kubwa mno.
Mheshimiwa
Spika, Ukiangalia Randama fungu 37 uk.3 kuhusu kupungua kwa maduhuli kuwa ni
kutokana uchakavu wa mitambo ya uchapaji ya Idara ya Mpigachapa Mkuu wa
Serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema hii ni aibu kubwa kwa Serikali kwani
ofisi ambayo ni tegemeo katika kuliingizia Taifa fedha inawezekanaje kushindwa
kununua vitendea kazi wakati inazalisha fedha
za kutosha?
Mheshimiwa Spika,
Kwa
mwaka wa fedha 2014/15 Idara ilitengewa fedha za ndani Tshs.1,000,000,000/- kwa
ajili ya Programu ya kuimarisha Idara hii, lakini kwa kuwa Serikali ya CCM
haioni umuhimu wa Idara hii hadi mwezi Machi, 2015 hakuna hata senti moja
ambayo Idara imepokea kwa ajili ya program tajwa.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka huu wa fedha Idara hii imepangiwa Jumla ya Tshs.500,000,000/-
tu. Hoja ni kama mwaka jana ilipangiwa kupatiwa shilingi bilioni moja na sasa
thamani ya shilingi imezidi kuporomoka imepangiwa kiasi pungufu ya nusu ya
mwaka jana. Mitambo inanunuliwa nje ya nchi, Je fedha hizo si zitakuwa ni kwa ajili
ya kufaulishwa kwenda kwenye mipango mingine ambayo si ya kuimarisha Idara
hiyo?
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani inaona kuwa kama kweli ofisi hii ikiimarishwa ni dhahiri
kusingekuwa na ulazima wowote kwa Serikali kuingia kwenye Kandarasi za uchapaji
wa nyaraka mbalimbali za uchaguzi na nyingine nyingi. Kwani tunaamini katika
ushindani wa Zabuni hizo Idara ingeshinda kwa kuwa kuna ruzuku ya Serikali
katika uendeshwaji wake. Hili lingewezekana pale tu dhana nzima ya Utawala Bora
itakapotekelezwa kwa vitendo na wananchi kuona kwamba utawala bora upo katika
utendaji wa Serikali. Mabilioni ya fedha za Walipa kodi yangeokolewa na pia
kusingekuwepo na ucheleweshaji wa kazi kwaajili ya watendaji waandamizi wa
Serikali kudai kwanza 10% kabla ya kazi kutolewa, jambo linaloturudisha nyuma.
10.
MAPENDEKEZO YETU YA NYUMA NA AHADI ZA
SERIKALI
10.1 RERA (Real Estate Regulatory Authority)
Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba yangu ya mwaka wa fedha 2011/2012 niliitaka
serikali kuanzisha chombo kitakachoweka uratibu na usimamizi wa sekta ya
majengo makubwa ya biashara inayokuwa kwa kasi kubwa.
Mamlaka hii siyo tu itasimamia haki za wapangaji, bali
hata mapato ya Serikali na ubora wa majengo haya na huduma zake. Nilipendekeza
mamlaka hii ya udhibiti iitwe ”Real Estate Regulatory Authority.” Tunarudia
tena kusisitiza ushauri wetu huu kwani Serikali inapoteza mapato bila sababu ya
msingi kwa jeuri na kiburi cha kutokubali ushauri uliotoka upinzani.
10.2 Uundwaji wa Tume Huru za Kimahakama
Mheshimiwa Spika,
Kumbukumbu za taarifa rasmi za Bunge zinaonyesha kwamba
katika hotuba yangu ya mwaka 2011/2012
tuliishauri Serikali kuhusu kuunda tume ya kijaji ya uchunguzi wa vifo
vya raia. Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
walikubali na wakaahidi kutekeleza hilo, lakini toka mwaka huo hadi sasa hakuna
chochote kilichotekelezwa na Serikali hii ya CCM.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba Serikali haina
dhamira yeyote ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu suala hili ambalo wananchi
wamekuwa wakililalamikia kuhusu jamaa zao kuuawa na vyombo vya dola. Ni ukweli
uliowazi kwamba tangu kipindi hicho vimeripotiwa vifo kadhaa, majina ya watu
waliouawa yanapatikana katika taarifa ya haki za binadamu ya mwaka 2013, uk.
22.
10.3 UNUNUZI WA SAMANI
ZILIZOTENGENEZWA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na msisitizo
kuhusu ofisi na taasisi za serikali kununua samani zinazotengenezwa nchini. Ni
dhahiri kuwa nchi zilizoendelea hazikufanikiwa kupiga hatua bila kushirikiana
na wafanyabiashara wa ndani hivyo samani za ndani zikinunuliwa kwa wingi pato
la taifa litaongezeka kwani lita – stimulate sekta nyingine za uchumi ikiwemo
ajira. Serikali lazima sasa ieleze ni
wizara, taasisi na ofisi zake ngapi zimeanza kutekeleza tamko la
Serikali la kuanza kutumia samani zilizozalishwa na viwanda vya ndani ya nchi ,
pamoja na ahadi za Waziri Mkuu hapa Bungeni?
10.4 Gharama kubwa za uendeshaji wa Serikali
Mheshimiwa Spika,
Kama Serikali ingekuwa inajali
gharama basi ingekuwa inafanyia kazi mapendekezo ya Kambi ya Upinzani tangu
mwaka 2011 ambapo tuliishauri kupunguza matumizi ya kawaida na kuongeza fedha
katika miradi ya Maendeleo.
Aidha, Serikali ingeacha kuendelea
kugawa mikoa na Wilaya kwani kwa kufanya hivyo ni kuongeza gharama za uendeshaji
wa Serikali. Ni jambo la ajabu kabisa kwamba kwa jinsi Serikali hii isivyojali
gharama za uendeshaji wa Serikali, hata Kata ya Mbagala sasa inapendekezwa kuwa
Wilaya Mpya!!!
Ofisi ya Waziri Mkuu imeshindwa
kumshauri Rais juu ya ugawaji wa Mikoa na Wilaya, matokeo yake kila kukicha
tunajenga Makao Makuu ya Wilaya na Mikoa wakati fedha hizo tungeweza
kuzielekeza kwenye miradi ya Maendeleo na huduma za jamii kama vile shule,
hospital , hata Tume ya Uchaguzi imelalamikia jambo hili kuwa linawavuruga sana
katika kuweza kupanga mipango yake kama kuweka mipaka ya majimbo na Kata kwa
mujibu wa sheria .
10.5 Sherehe za Kitaifa
Mheshimiwa Spika, maadhimisho hayo yote hufanyika kuanzia ngazi ya
Taifa hadi ngazi ya Wilaya kwa kufanya sherehe mbalimbali zinazohusisha viongozi
wa kiserikali, na hivyo ni dhahiri matumizi ya kodi za wananchi hutumika. Kambi
ya Upinzani inasema kuwa matukio hayo ya kihistoria ni muhimu yaeleweke kwa
vizazi vyetu vya sasa na vijavyo.
Mheshimiwa Spika, katika kufikia azma hiyo si
lazima tutumie fedha nyingi za walipa kodi wakati Serikali inashindwa
kutimiza wajibu wake muhimu zaidi wa kutoa huduma za msingi kwa wananchi wake,
kama vile huduma ya maji safi na salama, elimu bora kuanzia ngazi ya msingi
hadi elimu ya juu, kupeleka nishati kwenye maeneo ya uzalishaji na kwa
Watanzania waishio vijijini n.k.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali badala ya
kufanya maadhimisho ya Sherehe hizo zote tuchague ni sherehe zipi zinatoa tija
kwa Watanzania na zipi hazileti tija na maadhimisho yake yaweke kwenye
kumbukumbu za kihistoria.
Hoja
yetu hiyo imeungwa mkono katika taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu pamoja na
Bajeti ya Matumizi ya kawaida na Mpango
wa maendeleo ya Mwaka 2013/14, 2014/15
na Makadirio ya mwaka 2015/16 ya Mkoa wa RUKWA fungu 89 uk. 15
Nanukuu
“Kuongezeka
kwa vikao, mikutano na makongamano yanayoitishwa na ngazi za Kitaifa kwa
maagizo ya kugharamiwa na Mikoa na Halmashauri, ambayo hayapo katika bajeti za
mikoa na Halmashauri, katika mazingira ambapo Mikoa na Halmashauri haina fedha
za kutolea hata huduma za msingi kwa wananchi” Hiki ni kikwazo kikubwa
kwa maendeleo ya Taifa .
10.6 Pension kwa Wazee
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani wakati tunawasilisha hotuba yetu mwaka 2011/2012
tulisema yafuatayo, nanukuu: “Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa dhana ya hifadhi ya
jamii ni pana sana, Kambi ya upinzani tunaitaka serikali kuzingatia pendekezo
letu kuweka mfumo utakaowafanya wazee wote kupata pensheni (Universal pension)
kila mwezi ili kuwapunguzia wazee wetu hasa waishio vijijini gharama kubwa za
maisha“. Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani
inasisitiza kuwa pensheni hii ni muhimu kwa kuwa itasaidia kuongeza kipato kwa
wanaoishi vijijini ambako umasikini wa kipato umejikita na kupunguza umasikini
kwa kiwango cha takriban asilimia 57.9 kwa wazee walio na umri zaidi ya miaka
65.
11.0 SERIKALI KUPUUZA NA KULIDANGANYA BUNGE
Mheshimiwa Spika,
Taifa
hili limekuwa mhanga wa mara kwa mara wa uzembe au kudanganywa na hata kupuuzwa
kwa maazimio ya Bunge, ambalo kikatiba, ndilo lenye wajibu wa kuisimamia
Serikali. Kupuuzwa huku kwa Bunge, kunadhalilisha uwepo wa taasisi hii nyeti ya
Taifa, kunaondoa uwajibikaji wa Viongozi na watumishi wa Serikali na hatimaye
kunalisababishia Taifa hasara kubwa siyo tu kiuchumi katika maeneo yanayohusu
musuala ya kiuchumi, bali pia katika upatikanaji haki katika Taifa.
Mheshimiwa Spika,
Wakati
Dunia inajua vilivyo kwamba Bunge lilifanya kazi yake katika kuisimamia
serikali, juu ya kashfa ya Operesheni Tokomeza na mwishowe kuishia kwa mawaziri
wanne kuachia madaraka kwa kuwajibika kisiasa, leo serikali inarudi kwa mlango
wa nyuma na kudai eti hakukuwa na tatizo.
Aidha,
Serikali imeendelea kufanya mkakati wa makusudi wa kuficha uovu na uzembe kwa
kusafisha viongozi katika masuala yote
yanayohusu umma hususan pale viongozi wa serikali na familia zao wanapokuwa ni
wahusika wakuu katika kashfa husika. Kwa mfano, Serikali imeshindwa hadi leo
kuweka hadharani ripoti ya Tume iliyoundwa na Rais ya majaji watatu; Jaji
Hamisi Msumi (Balozi) akiwa mwenyekiti; Jaji Stephen Ernest na Jaji Vincent
Kitubio ikiwa imekabidhi ripoti yake serikalini na badala yake kutangazwa na
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Kwa
mfano, Balozi Sefue anasema mawaziri wote wanne waliojiuzulu mwaka 2013 kwa
sakata la Operesheni Tokomeza hawana hatia. Yaani serikali inataka hata kusema
kwamba hata kule viongozi hao kuchukua wajibu wa kisiasa kuwajibika ni kinyume
cha utawala bora.
Wakati
ikisema hivyo, serikali hii ya CCM inakubali kwamba kuna watu waliuawa kwa
makosa, idadi ya ilikuwa inaonyesha ni watu 15 ingawa Tume inathibitisha vifo
tisa; Tume inakiri kwamba kuna watu walidhalilishwa; kuna watu waliharibiwa
nyuma na mali zao kama mifugo kupigwa risasi na kila aina ya uonevu. Serikali
imekubali kulipa fidia kwa wote waliokumbwa na madhila haya. Katika mazingira
haya uwajibikaji wa kisiasa unakuwaje kosa? Serikali inasafisha vipi
waliowajibika kisiasa?
Mheshimiwa Spika,
Kwa
nini hatujifunzi kwa Mzee wetu, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alipowajibika
miaka ya sabini kwa sababu ya madhila waliotendewa wananchi na askari ingawa
yeye mwenyewe hakushiriki. Serikali hii kwa nini inaogopa na kukwepa
uwajibikaji? Kama serikali hii inaamini katika uwajibikaji na uwazi iweke
hadharani ripoiti ya Majaji watatu kuhusu kashfa ya Operesheni Tokomeza ili
wananchi waisome na kujiridhisha vinginevyo serikali hii inaendeleza tabia ile
ile ya kukwepa kuwajibishwa na Bunge kama ilivyokuwa kwenye maazimio ya
Operesheni Tokomeza.
Mheshimiwa Spika,
Juhudi
za serikali za kutaka kusafisha na kufunika kashfa zake pia kumethibitika wiki
iliyopita tu baada ya Katibu Mkuu Kiongozi tena kujaribu kuwasafisha wahusika
wa sakata la Tegeta Escrow. Watanzania wanajua na dunia inajua kwamba kama kuna
wizi wa mchana kweupe umefanyiwa nchi hii ni kashfa ya Tegeta Escrow, watumishi
wa umma wamehongwa mamilioni ya fedha, majina yametajwa; aliyekuwa Katibu Mkuu
Nishati na Madini, Eliackim Maswi na Waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo,
walionyesha ni kwa jinsi gani walishindwa kuisaidia serikali na nchi isiibiwe kwenye
kashfa hii, lakini pamoja na maazimio ya Bunge kuwataja kwa ushahidi jinsi
walivyoshindwa kutekeleza majukumu yao, serikali imekuwa hailali eti ikitafuta
njia ya kuwasafisha.
Hii
ni serikali pekee duniani inayokasirika Bunge likifanya kazi yake sawa sawa ya
kuisimamia ndiyo maana mara nyingi imegeuka na kutafuta njia ya kufunika madudu
ambayo siyo tu yameiaibisha sana, bali yamegharimu kodi nyingi za wananchi.
Serikali
inajua kwamba utekelezaji wa bajeti ya serikali inayomalizika ya mwaka 2014/15
umekwamishwa sana na kashfa ya Tegeta Escrow baada ya nchi wafadhili kuzuia
kutoa fedha za kuchangia fungu la maendeleo kutokana na tabia ya serikali
kufunika kombe mwanaharamu apite kwenye kashfa hii. Tunataka serikali iseme
kwamba inapolinda na kubeba wahusika wa kashfa hizi wanataka kuwasaidia
wananchi au viongozi wameamua kujiunga dhidi ya wananchi wao?
Serikali
inajua kuwa kashfa ya Escrow ina mizizi katika kashfa ya IPTL iliyoanza mwaka
1994 ndani ya Wizara ya Nishati na Madini Rais Jakaya Kikwete akiwa waziri,
ikaidhinishwa mwaka 1995 Rais Jakaya Kikwete akiwa Waziri wa Fedha na sasa
inafumuka katika sakata hili la Escrow na kuiparaganyisha serikali Rais Kikwete
akiwa madarakani. Ni kwa nini mambo haya yanatokea na serikali inaendelea
kuyabeba na kusafisha uoza huu? Ni kwa faida ya nani?
Mheshimiwa Spika,
Kamato
Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mhe. Christopher Ole Sendeka ilitoa mapendekezo
muhimu na mazuri wa namna ya kukabiliana na kutatua migogoro yo muda mrefu ya
Wakulima na Wafugaji. Hadi sasa Serikali haijaeleza kinagaubaga imejipanga vipi
kutekeleza maazimio haya ya Bunge, lakini tunashuhudia wakulima na wafugaji
wakiendelea kupambana na kuharibiana mali na hata kuuana,
Mheshimiwa Spika,
Katika
mlolongo huu wa kushindwa kusimamia nchi, kuendekeza makundi na vita vya kisiasa
ndani ya CCM na serikali yake kwa gharama ya Taifa, taifa hili sasa linadaiwa
Sh. bilioni 120 baada ya kushindwa kwenye kesi ya Dowans/Richmond katika
Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) huko Paris. Serikali haijataka
kuliweka jambo hili wazi na ni dhahiri kuna siri kubwa inayosababisha jambo
hili kuwa la usiri mkubwa. Huko mbele ya safari jambo hili litaligharimu Taifa
mabilioni haya ya fedha ambayo yangeweza kuepukika kama ukweli, uwazi na haki
vingetawala mchakato mzima wa kashfa ya Richmond. Serikali isimame sasa na
ilieleze Taifa ni nani anasema kweli, ni nani alilidanganya Bunge na ni nani
analindwa na serikali katika kashfa hii?
Mheshimiwa Spika,
Mapambano
ya mitandao ndani ya serikali ya CCM na minyukano ya kupigania maslahi na ulaji
ndani ya mikataba mbalimbali ya miradi ya umma ikiongozwa na walio karibu na
Watawala na familia zao imeota mizizi katika serikali hii.
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni ingependa kujua kwamba serikali hii ya CCM ambayo
imefikia mwisho wake ni kwa nini inawaachia Watanzania madeni makubwa hivi? Je,
kashfa hizo zote za serikali kushindwa kuwajibika, kutafuta visingizio vya
kufunika madhambi yake, ndiyo maisha bora kwa kila Mtanzania ambayo wananchi
waliahidiwa miaka 10 iliyopita? Nini kauli ya serikali juu ya tabia hii ya
kuwabebesha wananchi mizigo ya madeni huku serikali hiyo hiyo ikijitahidi kwa
nguvu zake zote kuwasafisha viongozi walioitumbukiza nchi kwenye madhila haya?
Ni
jambo la kumshukuru Mungu kuwa sasa hatimaye utawala wa CCM unakaribia ukingoni
na ni rai yangu kwa Watanzania wote waonyeshe hasira yao ya kuibiwa,
kudhalilishwa na hata kufanywa mafukara kwa kikinyima chama hiki cha zamani
kilichogawana rasilimali za Taifa hili kwa misingi ya kifisadi kwa muda mrefu.
TUKUBALIANE KWA PAMOJA KUWA NI
KWA MASLAHI YA TAIFA LETU NA VIZAZI VIJAVYO KUIONDOA CCM MADARAKANI SASA KWANI
KASI YA UKWAPUAJI INAZIDI KUSHIKA KASI.
Mheshimiwa
Spika,
Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni naomba kuwasilisha.
……………………………………
Freeman Aikaeli
Mbowe (MB)
KIONGOZI
WA UPINZANI BUNGENI (KUB)
12
Mei, 2015
No comments:
Post a Comment