Saturday, May 2, 2015

Chadema yashtukia zoezi la uandikishaji wapiga kura.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoani hapa kimesema uandikishaji wa majina ya wapiga kura kwenye daftari la kudumu la wapigakura unaotakiwa kuanza leo mkoani hapa, unafanywa kwa siri.

Mkurugenzi wa operesheni na mafunzo wa chama hicho ngazi ya taifa, Benson Kigaila, alieleza hayo kupitia mkutano wa hadhara, uliyofanyika kwenye uwanja wa barafu mjini hapa. Alisema Chadema kimeanza kufanya uhamasishaji katika viunga vyote vya mji huo kwa kuingia nyumba hadi nyumba na kuzungumza na mtu kwa mtu, kuhakikisha kila mwenye sifa ya kupiga kura, anajiandikisha.

Alisema zoezi hilo litafanyika bila kujali tofauti za itikadi za vyama vya kisiasa, kwa sababu Chadema inaamini lengo kuu ni kuikomboa Tanzania kutoka katika manyanyaso yanayofanywa na viongozi wa CCM ambao chama chao kimekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 50 huku nchi ikiendelea kudidimia kwenye umasikini. Mkutano huo ulitangaza wanachama wa Chadema wanaotarajia kuchuana katika uchaguzi wa ndani ili kupata watakaokiwakilisha katika kugombea ubunge, kwenye majimbo yote tisa ya mkoani Dodoma.

Jimbo la Chilonwa ambalo kwa sasa Mbunge wake ni Ezekiah Chibulunje, ambaye ametangaza kung’atuka baada ya kulitumikia kwa miaka 20, ilielezwa mkutanoni hapo kuwa wana Chadema wanaoliwania ni pamoja na Eva Mpagama, Manambaya Manyanya na John Kigongo.

Jimbo la Kongwa linalowakilishwa na Job Ndugai, ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, linawaniwa na Emmanuel Suday, Mashaka Madale na Mussa Muhaha. Majimbo mengine ambayo yalielezwa kuwindwa na chama hicho ni pamoja na Kibakwe, linalowakilishwa na Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.

1 comment: