Tuesday, May 19, 2015

Bawacha: Wanawake msikubali wagombea wa CCM kuwatumia.

Katibu wa Baraza la Wanawake CHADEMA Taifa (BAWACHA) Grace Tendega

Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Taifa (Bawacha), Grace Tendega, amewataka wanawake nchini kukataa kutumiwa kama daraja la kuwapitisha wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu na badala yake wakipigie Chadema ili kishike dola.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano wa baraza hilo Mkoa wa Arusha na kuhudhuriwa na mamia ya wanawake wa mkoani humu.

Alisema CCM wamekuwa wakiwatumia wanawake vibaya kwa kuwapa khanga, fulana na vijisenti ili wawapigie kura na baada ya kuwapa kura huwasahau na kubaki katika maisha magumu yasiyoelezeka.

“Nawaomba sana akina mama na ili kuwaondoa hawa watu, lazima kila mmoja kwenye mitaa yenu mvute wenzenu kujiandikisha ili tuwe na uhakika wa ushindi wa kishindo,” alisema.

Aidha, aliwataka wanawake kushikamana katika wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu na kuacha majungu yasiyo na tija kwa chama.

Aliwataka kutumia vizuri simu zao za kiganjani kueneza mabadiliko na waepuke kuzitumia kwa masuala yasiyo na tija kwa chama kama kuchambuana na kutoleana lugha za matusi.

“Lakini tujitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na pindi mtu atakapokosa asichukie, kwani hatuwezi wote kupata nafasi hiyo, ila juhudi na elimu yako vitakubeba zaidi,” alisema.

Tendega aliwaomba wanawake hao kuheshimu viongozi wao kwa kujali itifaki ili chama kisonge mbele na siyo kuendekeza majungu.

Naye Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (pichani), alisema hana wasiwasi wa ushindi Arusha, kwani ana jeshi kubwa la wanawake kwa kulinganisha na miaka ya nyuma alikotoka.

Lema aliwataka wanawake hao kupokea fedha zilizomwagwa kwenye majimbo yote ya Chadema na kutafuna lakini kura zao wazipeleke Chadema.

Aliwaomba wanawake hao kusikiliza maelezo ya viongozi wao na hasa pale uchaguzi utakaposogezwa mbele.
"Mkisikia kuna maandamano, jitokezeni kwa wingi kudai haki ya uchaguzi," alisema.

“CCM mwaka huu wamekwisha na ndiyo sababu wanaogopa uchaguzi na wanaanza kupanga njama za kuusogeza mbele, hivyo sisi hatukubali, waache tuingie uchaguzi na tushike dola, japo watatuachia nchi ikiwa na changamoto nyingi,” alisema.

Aliwaomba wanawake hao kupuuza propaganda zinazoenezwa katika mitandao na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu viongozi wao kwa maelezo kwamba wapo baadhi ya watu wamenunuliwa kufanya kazi hiyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Walemavu Wasioona, Graceelly Macha, aliomba wanawake kuwabeba wanawake walemavu kwa kuwashawishi kuingia katika siasa.


“Tuwasaidie hawa walemavu kuingia katika siasa kwani kuwa mlemavu siyo sababu ya kutoshiriki siasa, wajitokeze kuandikisha katika daftari la mpiga kura ila ni lazima wahamasishwe,” alisema.

No comments:

Post a Comment