Sunday, April 19, 2015

YANAOENDELEA KATIKA MIKUTANO YA UZINDUZI WA KANDA

Mkutano wa Uzinduzi Kanda ya Victoria uliofanyika leo;
Leo Kaimu Katibu Mkuu John Mnyika amezindua mafunzo hayo kwa Kanda ya Victoria (Mwanza, Kagera na Geita), ambapo amezungumzia masuala 2.
1.     Suala la ajali ambalo linaendelea kumwaga damu na kukatisha damu za Watanzania wenzetu kila kukicha bila kuwepo kwa mkakati wowote wa kushughulikia wala uwajibikaji.
i.                    Baada ya kikao hicho cha mafunzo kusimama kwa dakika moja kuwakumbuka marehemu waliokufa jana kwenye matukio mawili tofauti, akitoa hotuba ya ufunguzi, Mnyika amemtaka Rais Kikwete kutoendelea kutoa pole kwa wafiwa bila kutoa kauli ya mkakati wowote ambao serikali inao katika kushughulikia suala la ajali ambalo alisema linapaswa kutangazwa kuwa ni janga la taifa.
ii.                  Ameendelea kumtaka Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta kuweka hadharani ripoti ya Kamati iliyoundwa na mtangulizi wake, Harrison Mwakyembe, mwaka jana kuchunguza vyanzo vya kukithiri kwa matukio ya ajali zinazosababisha kupotea kwa maisha ya watu wengi, wengine kuwa walemavu, wajane, yatima n.k huku pia nguvu kazi ya taifa ikipotea.
iii.                Amehoji ukimwa wa Rais Kikwete na Sitta wakati watu wanaendelea kupoteza maisha huku hadi sasa kukiw ahakuna uwajibikaji wowote ule kutokana na janga hilo.

2.     Amezungumzia suala la BVR na hatima ya uchaguzi mkuu.

i.                    Amesema kuwa majibu ya Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lubuva kwa kauli ya Mwenyekiti wa CHADEMA kuhusu mchakato wa uandikishaji wapiga kura kwa mfumo wa BVR na suala la kusogeza muda wa uchaguzi na hivyo kuongeza muda wa serikali iliyoko madarakani, hayajakidhi haja, vigezo wala kuondoa shaka iliyopo sasa inayoibua kizungumkuti kikubwa kwa taifa kuhusu hatma ya uchaguzi.
ii.                  Amemtaka Jaji Lubuva ili kumaliza shaka na kizungumkuti hicho cha kusogezwa kwa uchaguzi, NEC itoe ratiba kamili yote ya uandikishaji wa wapiga kura kwa BVR, itakayoonesha tarehe za zoezi zima litakavyofanyika, kata moja hadi nyingine, nchi nzima.
iii.                Ameitaka NEC kusema tarehe ambayo vifaa vyote 8,000 vya uandikishaji (BVR kits) vitakuwa vimewasili nchini kwa ajili ya kumaliza mchakato wa uandikishaji ndani ya muda ambao Jaji Lubuva amesema zoezi litakuwa limekamilika.
iv.               Kwa sababu kwa kuzingatia uozefu unaoendelea Mkoa wa Njombe, huku NEC ikitarajiwa kuandikisha wapiga kura mil. 23.9 (kwa mujibu wa tume) nchi nzima, au mil. 24 (kwa mujibu wa NBS), kiuhalisia mahesabu ya kawaida yanadhihirisha kabisa kuwa zoezi la uandikishaji halitaweza kukamilika ifikapo mwezi Julai kama ambavyo Jaji Lubuva amekaririwa akisema.  
v.                 BVR NA BOMU LA UFISADI; kwa kuwa baada ya mwongozo ulioombwa na Mnyika bungeni kuhusu hatma ya BVR, kura ya maoni na hatma ya uchaguzi mkuu mwaka huu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema kuwa tayari serikali imeshatoa 75% ya malipo ya BVR, lakini hadi sasa NEC haijaweza kufanya kutimiza wajibu wake sawasawa ikiwemo kupatikana kwa vifaa (kulingana na malipo ya 75% aliyosema PM), basi kuna haja ya Bunge kupitia Kamati ya Hesabu za Serikali kuingilia kati na kukagua matumizi ya fedha hizo za walipa kodi wa Tanzania.
vi.               Amesema hivyo kwa sababu katika masuala ya zabuni na mikataba lazima kila upande uwajibike kulingana na utekelezaji wa mkataba wa shughuli husika.
vii.             Hivyo amesema mbali na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ambayo inapaswa kukutana na NEC kama ilivyoagizwa bungeni, lakini pia PAC inapaswa sasa kuingilia kati kuangalia mahesabu na matumizi ya fedha hizo kwenye mchakato wa BVR, maana kuna harufu ya uvundo wa ufisadi.
NB; Mnyika atakuwa na mkutano wa hadhara jioni la leo, Uwanja wa Furahisha, Mjini Mwanza.
RATIBA YA KESHO JUMAPILI, APRILI 19
KANDA YA PWANI- KIBAHA
Unaweza kuingiza kwenye diary ya dawati lako; kesho Makamu Mwenyekiti Prof. Safari atazindua mafunzo hayo Kanda ya Pwani (Temeke, Kinondoni, Ilala na Pwani), asubuhi, Ukumbi wa Country Side, Kibaha Mjini.
Baada ya kuzindua mafunzo, Prof. Safari akiambatana na Mwenyekiti wa Kanda Mabere Marando, watahutubia mkutano wa hadhara Uwanja wa  Mpira- Bwawani, Stendi ya Kibaha Maili moja. Kuanzia saa 8 mchana.
 KANDA YA SERENGETI (Mara, Simiyu na Shinyanga)
Kaimu Katibu Mkuu Mnyika atakuwa Musoma, ambapo atazindua mafunzo hayo mjini Musoma kwenye Ukumbi wa MCC kisha yatafuatiwa na mkutano wa hadhara Uwanja wa Mkendo.
KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI
Kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Ruvuma, Mbeya, Njombe, Iringa na Rukwa) Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu atazindua mafunzo hayo mjini Mbeya katika Ukumbi wa Mkenda, Soweto, kisha yatafuatiwa na mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Dk. Slaa (zamani Rwandanzovwe).


No comments:

Post a Comment