Wednesday, April 22, 2015

Mnyika: Watuhumiwa Escrow wakamatwe, wafilisiwe.

Naibu Katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika (pichani), amesema baada ya Rais Jakaya Kikwete kukabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa uchotaji wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow, achukue hatua ya kuwakamata na kuwafilisi watuhumiwa hao.

Aidha, alisema watuhumiwa hao baada ya kukamatwa na kufilisiwa mali zao, wanatakiwa kufikishwa mahakamani pamoja na kuamriwa kurejesha fedha zote walizoiba.

Akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara, alisema iwapo hatua hizo hazitachukuliwa hadi Bunge lijalo la bajeti, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) watawasha moto upya ili kupata majibu ya kina kabla ya kuelekea uchaguzi mkuu.

Mnyika alisema baada ya Rais kupokea ripoti ya Baraza la Mawaziri, taasisi ya kuzuia rushwa (Takukuru) na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, ni wakati mwafaka ripoti hizo zikawekwa hadharani ili watuhumiwa wote wafikishwe mahakamani baada ya kufilisiwa mali zao.

“Katika kikao chetu na sasa mkutano wetu huu tunatoa azimio la pamoja na tunamtaka Rais Kikwete na tunataka watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani na mali zao kufilisiwa ili fedha za umma zirejeshwe,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema sakata la Tegeta Escrow mwaka huu, halitafunikwa kama walivyofunika mikataba ‘hewa’, hakuna majibu ya tofauti yatakayotolewa na kusukumiana mpira na viongozi wa sekta zingine bila kujali wao ndiyo wasimamizi wakuu.

Alisema kamwe Chadema hawawezi kuwa wasaliti wa Taifa hili kama bendera ya chama hicho yenye rangi ya kuonyesha upendo, hivyo lazima kitapamba hadi tone la mwisho kuona Watanzania wananufaika na rasilimali za nchi zao. Kuhusu elimu alisema serikali ya CCM licha ya kuiga sera iliyotangazwa na Chadema 2010 kwa ajili ya kutoa elimu bure, lakini inasikitisha serikali ya CCM kutangaza sasa kuanza kutoa elimu bure huku ikizidi kuwatoza wananchi michango katika sekta ya elimu msingi kuliko malipo ya ada.

No comments:

Post a Comment