Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, ameondoka nchini kuelekea Marekani kwa ziara ya kikazi.
Mkuu wa Mambo ya Nje Chadema, Deogratias Munishi, alisema jana kuwa Dk. Slaa ambaye aliambatana na mkewe, Josephine Mushumbusi, waliondoka juzi na watakuwa Marekani kwa ziara ya siku tisa.
Alisema ziara hiyo inafuatia mwaliko wa Gavana wa Jimbo la Indiana, Mike Pence, pamoja na taasisi mbalimbali za nchini humo vikiwamo vyuo vikuu kutokana na kutambua mchango wa kisiasa na kijamii wa Dk. Slaa na chama chake katika maendeleo ya Bara la Afrika.
Munishi alisema ziara hiyo itamwezesha Dk. Slaa kushiriki mijadala mbalimbali inayohusu uwekezaji, elimu na uongozi iliyoandaliwa kwa ajili yake ambayo lengo lake kuu ni kuitangaza Tanzania.
Alisema akiwa Marekani, Dk. Slaa atafanya mihadhara kwenye vyuo vikuu vya Purdue, Indiana na Marion.
Aliongeza kuwa Dk. Slaa pia atakua na vikao vya mashauriano na baadhi ya wahadhiri wa vyuo vikuu mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya kisiasa na maendeleo na kijamii na ushiriki wa Chadema katika siasa za kimataifa.
Alisema ziara hiyo itamkutanisha Dk. Slaa na viongozi na watendaji wakuu wa kiserikali wa Jimbo la Indiana, kampuni na taasisi kubwa za uwekezaji kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika masuala ya uchumi na uwekezeji barani Afrika.
No comments:
Post a Comment