Saturday, April 18, 2015

CHADEMA kazini, maandalizi ya kushika dola; Prof. Safari hapa, Mnyika kule, Mwalimu Salum huko

Baada ya Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe kufanya uzinduzi wa kitaifa wa mafunzo kwa ajili ya timu za kampeni nchi nzima, viongozi wa chama nchi nzima na mafunzo kwa ajili ya viongozi wa Serikali wanaotokana na CHADEMA walioenea nchi nzima, utekelezaji umeanza mara moja kuanzia leo.

Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya kukiandaa chama na viongozi wake kwenda kushika dola na kusimamia serikali ya UKAWA, kwa niaba ya Watanzania kupitia uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Naibu Katibu Mkuu Bara John Mnyika ambaye kwa sasa ni Kaimu Katibu Mkuu (wakati Dk. Slaa akiendelea na ziara ya kikazi nje ya nchi baada ya kufanya kazi ya kukijenga chama mijini na vijijini nchi nzima), leo atazindua mafunzo hayo kwa Kanda ya Victoria (Mwanza, Geita na Kagera), katika Hoteli ya Mash, ambapo wakufunzi hao watashuka chini kwenye ngazi ya mikoa, wilaya, majimbo, kata, matawi na misingi, hivyo yatawafikia viongozi wote wa chama nchi nzima hadi ngazi ya vitongoji kwenye nyumba kumi kumi.

Baada ya uzinduzi wa mafunzo hayo, Kaimu Katibu Mkuu Mnyika atafanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Furahisha kuanzia majira ya saa 9 jioni ya leo, ambapo wananchi wote wamealikwa kuhudhuria kwa wingi kama ilivyo ada ya watu wa Jiji la Mwanza na vitongoji vyake linapokuja suala la harakati za ukombozi wa kuiong'oa CCM madarakani.

Siku ya kesho, Jumapili Aprili 19, kazi zitakuwa zinaendelea kushika kasi.

Makamu Mwenyekiti Bara, gwiji wa sheria na Kiswahili, Prof. Abdallah Safari atazindua mafunzo hayo kwa Kanda ya Pwani pale mjini Kibaha.

Semina ya mafunzo hayo inatarajiwa kuanza saa 3.00 asubuhi hadi saa 7.00 mchana, kisha yatafuatiwa na mkutano mkubwa wa hadhara utakaofanyika Kibaha Mjini kuanzia saa 9.00 alasiri.

Makamu Mwenyekiti Prof. Safari ataambatana na Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani (Temeke, Kinondoni, Ilala na Pwani), Wakili Mabere Marando, ambao wote kwa pamoja wanatarajiwa kuendelea kutia chachu ya kuiondoa CCM katika kanda hiyo.

Siku hiyo hiyo ya kesho Kaimu Katibu Mkuu Mnyika atakuwa ameingia mkoani Mara kwa ajili ya kuzindua mafunzo hayo kwa Kanda ya Serengeti (Simiyu, Mara na Shinyanga) na kufanya mkutano wa hadhara Musoma, wakati huo huo 'pacha' wake, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu atakuwa ameingia mkoani Mbeya ambapo kesho pia atazindua mafunzo kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Iringa na Njombe) kisha atafanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Dk. Slaa jijini Mbeya.

Tutawapatia ratiba hii ya 'hakuna kulala...' kwa ajili ya kujipanga kushika dola, kuendesha na kusimamia serikali, itakavyokuwa nchi nzima kadri muda unavyokwenda.

Ni dhamira ya wazi ya CHADEMA kwa kushirikiana na vyama washirika wenza katika UKAWA, kuiondoa CCM madarakani kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Makene...

No comments:

Post a Comment