Friday, April 17, 2015

Chadema: Hakuna kulala, hakuna kula

Dar es Salaam.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kilizindua mkakati wake wa ushindi “Hakuna kulala, hakuna kula mpaka kieleweke” katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba kwa kufungua mafunzo yatakayoendeshwa nchi nzima kwa viongozi wa vyama na Serikali za Mitaa.

Katika mkakati huo, chama hicho kimeigawa nchi katika kanda 10 za utekelezaji huku kikijipanga kuimarisha nguvu zaidi katika Jiji la Dar es Salaam lenye idadi kubwa ya wapigakura.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wakati wa uzinduzi wa mkakati huo kitaifa jijini hapa kuwa watafundisha viongozi wote wa chama hicho na watangaza nia, mbinu za uongozi bora na namna ya kushinda.

Mbowe alisema mpango huo wa mafunzo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya chama kwa kuwa hawawezi kushika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa bila kuwa na viongozi bora na weledi.

Alisema Chadema kitakwenda katika kanda zote, majimbo ya kichama 242, kata 4,852, matawi 22, 749, misingi 64,803 na kuwafikia viongozi 224,287 na timu zote za mafunzo zimeshatawanyika nchi nzima.

“Tunawafundisha viongozi wetu walio tayari ndani ya chama au Serikali za Mitaa namna ya kutekeleza wajibu wao. Lakini tunawaimarisha wanaokusudia kugombea nafasi mbalimbali kuwa wagombea wazuri zaidi, kuandaa ajenda za chama na namna ya kukamata madaraka kwa kuwa safari ya kushika Dola 2015 haina kizuizi,” alisema Mbowe huku akishangiliwa.

Kuahirisha uchaguzi
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya viongozi na watia nia wa Kanda ya Pwani ya chama hicho, Mbowe aliitaka Serikali kutojaribu kabisa kuahirisha Uchaguzi Mkuu kwa sababu ya kusuasua kwa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) akitishia kuwa ‘moto utawaka’.

Alisema Ukawa hawakusema chochote wakati wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipoahirisha Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa ilikuwa batili na ilianzishwa kwa masilahi ya Serikali na aliahirishwa na wao wenyewe.

Aliitaka Serikali kuharakisha uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kuwa imesalia miezi mitatu na nusu kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu hapo Agosti.

Alisema tarehe ya kupiga kura ambayo ni Jumapili ya Oktoba ilifahamika tangu awali kwa kuwa ni ya kikatiba lakini mpaka sasa uandikishaji unasuasua katika Mkoa wa Njombe wenye wapiga kura 340,000 ambao alisema hawafiki hata nusu ya waliopo Jimbo la Ubungo.

“Wanasubiri kama walivyofanya kwenye kuahirisha Kura ya Maoni na ili waseme ‘ndugu Watanzania kwa kuwa tumechelewa kuandikisha wapigakura tunaomba Bunge lako tukufu liongezee muda kwa Serikali ya awamu ya nne’... mtakubali?” aliwahoji wafuasi hao na kujibiwa “Hapanaaaa”.

“Serikali ikijaribu tu kuahirisha uchaguzi, nchi itawaka moto. Ikifika tarehe 25 Oktoba, Rais Jakaya Kikwete nenda Msoga (Bagamoyo) ukapumzike utuachie Ukawa na nchi yetu.”

Kuimarisha ngome Dar
Katika kile ilichoita kuimarisha ngome yenye kura nyingi, Chadema imetoa maazimio matatu kwa viongozi na wafuasi wake wa Dar es Salaam kuhakikisha inashika nafasi zote za uongozi hapo Oktoba.

Alisema jiji hili siyo tu makao makuu ya Serikali, balozi za nchi mbalimbali, au kitovu cha mapato, bali lina majimbo saba ya kwanza kwa idadi kubwa ya wapigakura kuliko mkoa wowote nchini, hivyo kusiwe na utani katika kutekeleza mikakati ya ushindi.

Mbowe, aliyesubiriwa kwa hamu tangu saa tatu asubuhi na kufika saa 6.05, alisema Jimbo la Ubungo ni la kwanza na lina wapigakura wengi kuliko hata mikoa ya Njombe na Katavi.

Akishirikiana na viongozi hao, Mbowe aliweka maazimio kuwa, Ukawa wanatakiwa kushinda majimbo yote, nafasi zote za umeya na madiwani ili kudhibiti mapato na kuleta maendeleo.

“Dhamana kubwa ya Taifa hili inawategemea wana Dar es Salaam, kazi tutakazozifanya kuanzia leo hadi siku ya uchaguzi zitasaidia nchi hii kubadilika au kuendelea kuwa na Serikali ya mabavu ya CCM,” alisema.

Alia kuzuia mpasuko
Kuhusu ugawanaji madaraka ndani ya Ukawa, Mbowe aliwataka makada hao kuvumiliana na kuzishinda changamoto zinazowakabili na kuwa Chadema na viongozi wa umoja huo wanaendelea vizuri na mipango ya ushindi.

Aliwaeleza wafuasi hao kuwa licha ya watu kuwaombea mabaya, wao hawatagombana zaidi ya kuungana kuing’oa CCM.

Alisema wanaotangaza nia wapo wengi kuliko nafasi zilizopo na atapatikana mmoja katika kila nafasi na watakaozipata, itakuwa kwa misingi ya haki na siyo dhuluma.

“Wale wote watakaokosa nafasi za kugombea ubunge na udiwani watambue kuwa vita tunavyopigana Chadema na Ukawa siyo ya kugombea madaraka. Bado wana nafasi kubwa ya kulitumikia Taifa hili kupitia Serikali yetu ya ushirika,” alisema.

Huku akishangiliwa na kuonyesha kujiamini, Mbowe aliongeza: “Tunahitaji watendaji wa Serikali, ndiyo nyinyi… msifikiri fursa ni ubunge pekee, zipo nyingi lakini zipatikane kwenye misingi ya haki, uwazi na kuheshimiana.”

Mbowe alibainisha kuwa CCM hawatakiwi kugombana huku wakitegea kusubiri mgombea wa Ukawa atangazwe ili wamtangaze wa kwao, wakifanya hivyo watasubiri sana na kwamba mgombea wa ushirika wao atatoka muda ukifika.

Ziara ya Dk Slaa
Akimkaribisha Mbowe, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema Tanzania inahitaji viongozi makini watakaoweza kukiondoa CCM madarakani.

Huku akishangiliwa, Mnyika alisema lengo kuu la chama hicho ni kushika dola Oktoba mwaka huu, ndiyo maana Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa yuko Marekani kwa ajili ya kuzungumza na Watanzania waishio huko na kuimarisha uhusiano na mataifa rafiki kwa kuwa Chadema kitashika dola.

Akizungumzia ziara hiyo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando alisema Dk Slaa yuko ughaibuni kuyafuta yaliyofanywa na Serikali ya Rais Kikwete ili Ukawa iweze kuwa na uhusiano mzuri na nchi za kigeni.

Ongezeko la madiwani
Mnyika alisema kuongezeka kwa madiwani wa upinzani katika mabaraza ya madiwani na wabunge Dar es Salaam, kumeonyesha ufanisi katika kusimamia fedha za umma tofauti na hali iliyokuwa kabla ya 2010.

“Baada ya kuongezeka kwa wabunge wa upinzani katika Manispaa ya Kinondoni, mapato ya ndani ya manispaa yaliongezeka kutoka Sh7 bilioni mwaka 2010 mpaka Sh35 bilioni hivi sasa,” alisema Mnyika ambaye anakaimu nafasi ya Katibu Mkuu.

Mbunge huyo alisema ufanisi unajitokeza kwa sababu viongozi wa Chadema wanafanya kazi kubwa ya kusimamia rasilimali za Taifa na kuhakikisha haziibwi.

Alisema mabadiliko yameanza kuonekana baada ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka jana ambao Chadema ilishinda mitaa 93 iliyopo Dar es Salaam kutoka mitatu kiliyoshinda mwaka 2009.

“Lengo letu si kuongeza idadi ya madiwani kwa ajili ya kuwa wapinzani, bali kuwa na madiwani wengi katika manispaa ya Kinondoni ili meya atoke Ukawa kuiongoza halmashauri,” alisema Mnyika huku wanachama wakimshangilia.

Uimara wa Ukawa
Marando ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, alisema Ukawa ni muungano ambao CCM haina ubavu wa kupambana nao na kwamba umedhamiria kukiondoa madarakani ili kurudisha rasilimali za nchi kwa wananchi.

Alisema wananchi wamechoshwa na dhuluma za Serikali ya CCM na kusisitiza kuwa Chadema kina viongozi wengi makini na wazalendo ambao watarejesha uhuru na haki kama alivyopigania Mwalimu Julius Nyerere.

“Wananchi wamechoshwa na miaka 50 ya CCM madarakani na mwisho wao ni Oktoba. Wanachotaka wananchi ni watu wenye nyota ya uongozi, ndiyo maana tumeanzisha mpango huu wa mafunzo,” alisema Marando.

Mwalimu na ziara ya ushindi
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema - Zanzibar, Salum Mwalimu alisema hiyo ni awamu ya pili ya kutoa mafunzo ambayo yatafanyika katika kanda za Victoria na Nyanda za Juu Kusini na Pwani na kubadilishana katika kanda zilizosalia.


Alisema wameunda vikosi vitatu vitakavyozunguka katika maeneo hayo. Kikosi cha kwanza kitakwenda Kanda ya Serengeti inayojumuisha mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu. Kikosi hicho kitakachokuwa chini ya Mnyika kitaendelea na mafunzo katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita.

Kikosi cha pili kitakuwa chini Mwalimu mwenyewe na kitakwenda Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Rukwa, Njombe, Iringa, Morogoro na kuhitimishwa Dar es Salaam.

Mwalimu alisema kikosi cha tatu kitaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema – Tanzania Bara, Profesa Abdallah Safari na kitatoa mafunzo katika mikoa ya Pwani na Tanga.

“Kuanzia Jumamosi itakuwa ni hakuna kulala, hakuna kula, mpaka kieleweke. Ziara hii ya mafunzo itakuwa ni moto nchi nzima,” alisema Mwalimu huku wanachama wakipiga makofi.

No comments:

Post a Comment