Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, ameibua upya kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), baada ya kuhoji sababu za vigogo waliopewa mgawo wa Sh. bilioni 73 kutoka Benki ya Stanbic kutohojiwa wala kuchukuliwa hatua hadi sasa.
Alisema hayo jana bungeni wakati akichangia Muswada wa Sheria ya Mifumo ya Taifa wa Mwaka 2015.
Mnyika alisema kutungwa kwa sheria hiyo kunatia mashaka kama itaweza kufanya kazi vizuri kwa sababu mwaka 2006 zilitungwa sheria mbili muhimu, ambazo hata hivyo hazijasaidia kukomesha vitendo vya ufisadi.
Alizitaja sheria hizo zilizotungwa mwaka huo kuwa ni sheria ya mabenki na taasisi za fedha na sheria ya BoT ya mwaka 2006, ambazo kama zingeweza kufanya kazi vizuri zingesidia kutatua matatizo yanayojitokeza kwenye miamala.
“Kutungwa kwa sheria kunaweza kusiwe suluhisho la matatizo haya kwenye miamala, mfano ilikuwaje ikaruhusiwa kutolewa fedha katika Benki ya Stanbic dola za Marekani milioni 122 kwenda katika akaunti zisizoeleweka kwenda Austaria na Afrika Kusini,” alisema Mnyika.
Alisema pia Sh. bilioni 73 zilichotwa katika benki hiyo na kuingizwa kwenye akaunti za watu, ambao hawaeleweki na hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa na kumekuwa na usiri mkubwa wa suala hilo.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema uchunguzi wa kashfa ya Escrow bado unaendelea na kwamba, taarifa zitatolewa utakapokamilika.
No comments:
Post a Comment