Saturday, March 21, 2015

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI, MHE. GODBLESS LEMA (MB),

UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu, familia yangu na viongozi wangu wa chama na wananchi wa Jimbo langu. Nawashukuru pia maadui zangu kwa dhati kwani uadui wao, hila zao, na mbinu zao chafu dhidi yangu zimeendelea kuiimarisha imani yangu na tumaini langu siku hadi siku, katika vita hii muhimu tunayopigana ya kulikomboa taifa hili.

Mheshimiwa Spika,Muswada huu wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi unaletwa katika Bunge lako tukufu wakati ambapo nchi hii iko katika mtanziko mkubwa ambapo matukio ya ujambazi wa kutumia silaha yamekithiri; mauaji ya raia kwa kutumia silaha za moto yameongezeka; matukio yenye sura ya ugaidi ya utekaji na utesaji yameshuhudiwa hapa nchini, matukio ya uvamizi na uporaji wa silaha katika vituo vya polisi yanashamiri na uhamiaji haramu umekuwa ukiongezeka pia kwa kasi hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Ni ukweli usiopingika kwamba matukio yote haya yametokea huku kukiwa na sheria ya Usimamizi wa Silaha na Risasi ambayo itafutwa na muswada huu kama utapitishwa na Bunge. Hii ni dhahiri kwamba tatizo kubwa la nchi hii sio sheria na matumizi yake, bali ni uongozi uliokosa fikra chanya na utu katika kutawala.

Ndio maana leo, Serikali inafikiri kupambana na janga la Mauaji ya Albino ni kuwatenga Albino na jamii kutoka kwenye makazi yao ya kawaida wakati tatizo la msingi ni imani potofu iliyojengeka miongoni mwa jamii. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba; huwezi kuipinga imani kwa kutumia silaha isipokuwa kwa habari njema (imani inayojali utu) kuwafikia watu wote.

Endelea..........



Mheshimiwa Spika,Pamoja na nia njema ya Serikali ya kuleta Muswada huu, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kwamba, kama Serikali itajali utu, usawa, haki na demokrasia ya kweli pengine hakungekuwa na hofu ya matumizi mabaya ya silaha miongoni mwa wananchi na hivyo kusingekuwa na na haja ya kuleta sheria za kudhibiti silaha na kuweka masharti magumu kwa wananchi kumiliki silaha, hasa kipindi hiki ambacho kumekuwa na matukio mengi ya kigaidi, ya uvamizi, utekaji na utesaji ambapo kimsingi wananchi wanahitaji ulinzi wa Serikali na ulinzi binafsi zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Mheshimiwa Spika,Taifa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ifikapo Oktoba mwaka huu wa 2015. Matumizi bora ya sheria za kulinda amani nchini ni muhimu sana wakati huu. Lakini mambo muhimu na ya msingi yakipuuzwa amani inaweza kutoweka licha ya sheria ngumu za udhibiti ikiwemo ya udhibiti wa silaha kuwepo: Masuala hayo ni kama yafuatayo:

i. Kuchezea haki ya mwananchi kujiandikisha kuwa mpiga kura:

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasisitiza kwamba, mzaha katika jambo hili hautavumilika. Aidha, ijulikane kwamba wananchi watakapotambua kuwa hawawezi kuwapata viongozi wao wanaowataka kupitia sanduku la kura, basi wanaweza kutafuta haki yao kwa njia nyingine hali ambayo inaweza kuliingiza taifa katika machafuko kwani haki haiombwi ila inadaiwa.

Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura ili waweze kuamua nani atakuwa kiongozi wao kwenye uchaguzi Mkuu unaokuja. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamkumbusha kila mwananchi atambue kwamba “Kura yako ni Maisha yako, Nenda Kajiandikishe Sasa”

ii. Kufanya Mzaha na uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi:

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaionya Serikali kutofanya Mzaha na jambo hili kwani linaweza kuiingiza nchi katika machafuko makubwa. Mheshimiwa Spika, Viongozi wa nchi hii wamekuwa wakifanya mizaha kuhusu maisha ya wananchi kwa mambo mengi, yakiwemo ufisadi uliokithiri. Kwa mfano wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika, uliwahi kumwomba Mheshimiwa Andrew Chenge kutoa mwongozo wa kutengeneza maazimio ya Bunge kuhusu watuhumiwa wa wizi wa fedha za Escrow wakati yeye mwenyewe alikuwa ni mtuhumiwa.

Huu ni mzaha mkubwa ambao kwa tafsiri inaonyesha kwamba watawala wanawaona watanzania kuwa ni wajinga. Kambi Rasmi ya Upinzani inaonya kuwa mizaha kama hii ikiletwa kwenye suala la uwepo wa tume huru ya uchaguzi, taifa hili linaweza likasambaratika. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzaniinataka Tume Huru ya Uchaguzi, si kwa sababu inataka kushinda uchaguzi bali ni kwa sababu inataka kujenga na kulinda Imani ya Mpiga Kura ili kulinda amani ya nchi yetu”.

iii. Matumizi ya Kisiasa ya Jeshi la Polisi:

Mheshimiwa Spika, kwa vile imethibitika pasipo shaka yoyote kwamba Polisi mkatili na mkorofi dhidi ya Upinzani anapandishwa cheo, ni dhahiri kwamba kitendo hiki kimejenga msingi (precedence) wa polisi kuwaonea, kuwadhalilisha na kuwafedhehesha viongozi wa Upinzani kwa matarajio kwamba watapongezwa na kupandishwa vyeo na Serikali.

Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani imepigia kelele sana suala hili la matumizi mabaya ya Jeshi la Polisi ya kulinda maslahi ya kisiasa ya watawala kwa miaka yote. Viongozi, wanaharakati na wananchi wanaounga mkono mageuzi wamepita kwenye bonde la uvuli wa mauti kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, Hatukuonewa kwa sababu sisi ni wanyonge, ila ni kwa sababu tumeendelea kuwa wavumilivu. Nina mashaka kama uvumilivu huo utandelea kuwepo kama uonevu na ukandamizaji utaendelea.

Mheshimiwa Spika, Mwenyezi Mungu, pamoja na upole wake, ukarimu wake, upendo wake, rehema zake kwa watu wote lakini bado ametenga Jehanamu kwa watenda dhambi ambao amewaumba yeye mwenyewe. Tusisubiri wananchi wachoke kuvumilia, bali hekima ya Mungu ituongoze ili kuliepusha taifa letu na majanga ya uvunjifu wa amani pindi watu watakapokosa uvumilivu wa mateso.

iv. Ulinzi wa Raia na Mali zao:Mheshimiwa Spika,

Kukosekana kwa ulinzi na usalama wa raia na mali zao kunaweza kuliingiza taifa katika machafuko. Matukio ya kuuwawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi – Albino, mauaji ya vikongwe na wanawake kutokana na imani za kishirikina yamekithiri sana katika nchi yetu licha ya kuwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

Hali hii imefanya wananchi kukosa imani na Serikali kwa kuwa bado yanaendelea licha ya kampeni nyingi kutoka kwawanaharakati mbalimbali kupinga mauaji ya Albino. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitahadharisaha Serikali kutodharau kundi la Albino kuwa ni dogo na kutolipatia ulinzi wa kutosha.

Mheshimiwa Spika,Baada ya utangulizi huo, sasa naomba nijielekeze kwenye muswada wa Sheria uliopo mbele yetu unaohusu Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi.

Mheshimiwa Spika,Matukio yote niliyoyataja hivi punde, ni matukio ambayo kwa kiasi kikubwa yamedhoofisha hali ya usalama hapa nchini. Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kwamba muswada huu umekuja wakati muafaka kwa kuwa matukio niliyoyataja hapo juu ambayo yamekuwa yakiongezeka hapa nchini, ni matukio ambayo utekelezaji wake unahitaji silaha. Na kwa kuwa matukio hayo ni ya kihalifu, ni dhahiri kwamba hata silaha zinazotumika, hazina uhalali.

Hivyo sheria bora itakayoweka udhibiti na usimamizi wa matumizi ya silaha hapa nchini inaweza kufanikiwa kupunguza matukio ya kihalifu ikiwa itatungwa kwa nia njema ya kulinda usalama wa raia wote na sio kwa lengo la kukandamiza kundi fulani la watu ili kukidhi matakwa ya kisisasa ya kundi la watu wachache.

MAONI NA MAPENDEKEZO YA JUMLA

Mheshimiwa Spika,Kabla sijaanza kuchambua vifungu vya muswada huu, naomba nitoe maoni ya jumla ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu utekelezaji bora wa muswada huu pindi utakapokuwa sheria kama ifuatavyo:

i. Serikali iimarishe ulinzi wa raia na viongozi sambamba na matumizi ya Sheria ya usimamizi na udhibiti wa silaha na risasi. Itakuwa haina maana sana kuweka sheria ya usimamizi na udhibiti wa silaha na risasi kama wananchi na viongozi watakuwa hawana ulinzi dhidi ya watu wanaotumia silaha kwa malengo ya kihalifu.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa ninapowasilisha maoni haya ya Kambi ya Upinzani kuhusu muswada huu, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawana ulinzi wa Serikali. Ni ajabu kwamba Mbunge ambaye kimsingi kazi zake zinamfanya awe na maadaui ambao ni wahalifu na mafisadi anakuwa hana ulinzi wowote wa serikali.

Kwa mfano maisha ya Mhe. David Kafulila aliyeibua sakata la wizi wa Escrow na kusababisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mawaziri kufukuzwa kazi yako hatarini kwa kuwa hana ulinzi wowote. Lakini wakuu wa Wilaya ambao kazi zao ni kupokea mwenge, kusoma taarifa za UKIMWI na njaa wilayani na kupokea wageni wa kitaifa wana ulinzi majumbani mwao.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka tukio la kuvamiwa na kuchomewa nyumba kwa wabunge wenzetu. Wabunge hawa wangekuwa wamepatiwa ulinzi wa polisi wenye silaha yamkini uvamizi ule ungeweza kuepukika.

Kwa mantiki hii Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuanzia sasa kutoa ulinzi kwenye nyumba za wabunge na viongozi wengine wanaostahili huduma hiyo kama ambavyo Serikali ya Kenya imefanya kwa wabunge na viongozi wake. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutofanya ubaguzi wa ki-ulinzi kwa viongozi katika mihimili mitatu ya Dola (yani Serikali, Bunge na Mahakama).

ii. Wabunge wote na viongozi wote wenye hadhi ya kidiplomasia (Diplomats) wawe na sifa za moja kwa moja (direct entitlement) za kumiliki silaha kwa ajili ya kujilinda mara tu wanapopata hadhi hiyo ya kidiplomasia.

Utaratibu wa kuwatambulisha kwa msajili wa Silaha ili kupatiwa leseni ya umiliki wa silaha ufanywe na taasisi wanazozitumikia. Lengo hapa ni kuepusha mlolongo mrefu wa kuwajadili viongozi walioaminiwa na wananchi walio wengi (kama Rais na wabubunge) au viongozi walioaminiwa kwa kiwango cha juu na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujadiliwa na ngazi za chini za uongozi katika vitongoji na mitaa kama ambavyo sheria ya sasa inavyoelekeza.

Kitendo cha kuruhusu viongozi wakuu walioaminika kujadiliwa na ngazi za chini kama wana sifa au hawana sifa za kumiliki silaha ni udhalilishaji wa itifaki (humiliation of protocol)

iii. Ulinzi na Usalama ni pamoja na kutambua hadhi na Itifaki.Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutambua hadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa ambao si wabunge lakini vyama vyao vina uwakilishi Bungeni na kuwapa hadhi ya kidiplomasia. Mheshimiwa Spika haiingii akilini kuona kiongozi wa Kitaifa kama Profesa Ibrahim Lipumba ambaye chama chake kina wabunge wengi bungeni na kinaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar anakuwa hana hadhi ya ki-diplomasia.

Kwa upande mwingine inashangaza kuona kiongozi wa kitaifa kama Dkt. Wilbroad Slaa ambaye chama anachokiongoza kinaunda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pia anakuwa hana hadhi ya kidipolmasia wakati wabunge walioko chini yake wana hadhi hiyo.Mheshimiwa Spika, viongozi wakuu wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi mkubwa bungeni ni viongozi wa Serikali watarajiwa.

Hivyo kupuuza itifaki na ulinzi wao ni kuiweka nchi katika mtanziko na mashaka. Hili si jambo ambalo mnaweza kuliunga mkono kwa sasa lakini ni jambo muhimu kwenu kuelewa.

MAONI NA MAPENDEKEZO YA VIFUNGU MAHSUSI

Mamlaka ya Msajili wa Silaha

Mheshimiwa Spika,Mamlaka na majukumu ya Msajili wa Silaha yametolewa chini ya kifungu cha 8(2) cha muswada huu wa sheria ya usimamizi na udhibiti wa silaha. Lakini kifungu hicho, hakijatoa mwongozo au mipaka ya utekelezaji wa majukumu ya Msajili wa Silaha. Matokeo yake ni kwamba katika maeneo mbalimbali ya sheria hii, Msajili amepewa mwanya mkubwa wa kuamua anavyotaka (discretion).

Kwa mfano kifungu cha 17 (1) na (2) kinampa Msajili wa Silaha mamlaka ya kutoa kibali cha kumiliki silaha kwa mtu yeyote kwa kipindi ambacho ataamua yeye mwenyewe na kuweka masharti ya kibali hicho yeye mwenyewe. Aidha, Msajili anaweza katika muda wowote kufuta kibali cha umiliki wa silaha.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtazamo kwamba, ni bora zaidi masharti ya utoaji kibali cha muda, masharti ya muda au kipindi ambacho kibali hicho kitakoma na masharti ya kufuta kibali yakawekwa na sheria na sio kutegemea utashi wa Msajili wa Silaha. Kwa kufanya hivyo, mianya ya rushwa au upendeleo au uonevu wa aina yoyote katika utekelezaji wa majukumu ya Msajili wa silaha inaweza kuzibwa na kuepukwa.

Watu wasio na Sifa ya Kumiliki Silaha

Mheshimiwa Spika,Katika kifungu cha 26(1) cha muswada huu ipo orodha ya mambo au tabia zinazoweza kumkosesha mtu sifa ya kumiliki silaha. Miongoni mwa tabia hizo ni pamoja na Ukorofi.Kwa kuwa tafsiri ya neno ukorofi ni subjective , na kwa kuwa kila mtu anaweza kutafsiri ukorofi kwa namna yake, hivyo msajili wa Silaha anaweza kuwa na tafsiri yake ya ukorofi kutokana na hisia zake na kumnyima mtu leseni ya kumiliki silaha kwa kisingizio kwamba mtu huyo ni mkorofi.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kwamba neno ukorofi litafsiriwe na sheria hii ili kuondoa mkanganyiko wa tafsiri pindi sheria hii itakapoanza kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, Kifungu 26(2) cha muswada huu kinaeleza kwamba endapo msajili wa silaha ataridhika kwamba kuna sababu za msingi za kuamini kwamba mtu hana sifa ya kumiliki silaha, atatoa notisi ya maandishi akimtaka mtu huyo kufika mbele yake katika muda na sehemu iliyotajwa katika notisi hiyo ili kuonyesha ni kwa sababu gani asitangazwe kuwa hana sifa ya kumiliki silaha. Aidha, ikiwa mtu aliyepewa notisi hiyo atashindwa kuhudhuria katika muda na sehemu iliyotajwa katika notisi, Msajili wa silaha atamtangaza mtu huyo kuwa hana sifa ya kumiliki silaha.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kwamba kifungi hiki kina mapungufu. Mapungufu hayo ni pamoja na muda wa kufika mbele ya msajili kutowekwa na sheria na badala yake kuachwa katika utashi (discretion) ya msajili wa silaha; na sharti la kufika mbele ya msajili wa silaha mwenyewe kujieleza kama mtu ana sifa ya kumiliki silaha iwapo kuna mashaka juu yake.

Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kwamba muda wa kufika mbele ya msajili uwekwe na sheria ili kuziba mwanya wa uonevu unaoweza kutumika kwa kuweka muda mfupi ili mtuhumiwa ashindwe kufika katika muda huo na kutangazwa kuwa hana sifa ya kumiliki silaha. Aidha, sharti la kufika mbele ya Msajili mwenyewe liondolewe na badala yake sheria iweke wasajili wasaidizi katika mikoa ili kupunguza adha na ghrama za kusafiri kumfuata msajili wa Silaha mmoja ambaye kwa vyovyote vile ofisi yake itakuwa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 26(3) kinasema kwamba cheti cha kuonyesha uwezo, leseni na kibali kilichotolewa kwa mtu aliyetangazwa kuwa hana sifa ya kumiliki silaha vitapoteza uhalali wake kuanzia tarehe ya kutangazwa huko. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji, ni kwa nini Serikali itoe cheti cha kuonyesha uwezo, leseni na kibali kwa mtu ambaye hana sifa?

Nasema hivi kwa sababu ikiwa Serikali itakuwa makini tangu mwanzo mtu anapoomba leseni au kibali cha kumiliki silaha basi uwezekano mtu huyo aliyekidhi vigezo tangu mwanzo vya kumiliki silaha kupoteza sifa na kutangazwa kuwa hana sifa utakuwa ni mdogo sana vinginevyo awe amekuwa kichaa ghafla.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 26(4) kinasema kwa pia kwamba mtu aliyetangazwa kuwa hana sifa ya kumiliki silaha, basi atasalimisha katika kituo cha Polisi haraka iwezekanavyo cheti cha kuonyesha uwezo, leseni na vibali vilivyotolewa kwake na silaha pamoja na risasi zilizo katika umiliki wake.

Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba huu unaweza kuwa ni uporaji wa hila wa silaha za wananchi kwa kutumia sheria, kwa kuwa muswada huu haujatamka ni hatua gani zitafuata baada ya mtu aliyetangazwa kuwa hana sifa za kumiliki silaha atakaposalimisha silaha yake na nyaraka za umiliki katika kituo cha polisi. Sheria hii ikiachwa kama ilivyo inaweza kutumika kwa kulipiza visasi au kutekeleza maelekezo yenye nia mbaya.

Utoaji wa silaha na risasi kutoka katika ghala la umma au kituo cha Polisi

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 29(1) cha muswada huu kinaeleza kwamba silaha au risasi zilizohifadhiwa katika ghala la umma, kituo cha polisi au sehemu nyingine yoyote iliyoelezewa na Msajili hazitatolewa humo isipokuwa kwa kibali kilichosainiwa na msajili. Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kuwe na ugatuzi wa madaraka ili kibali cha kuondoa silaha katika ghala la umma au sehemu nyingine yoyote kiweze kusainiwa na Wakuu wa Polisi wa Mikoa hasa pale kunapotokea dharura mfano ujambazi, uasi, wanyama hatari nk.

Masharti kwa Wauzaji wa Silaha

Mheshimiwa Spika,Kifungu cha 33 cha muswada huu kinampa Waziri mamlaka makubwa ya kutunga kanuni zitakazoweka masharti ya utoaji wa kibali cha muuzaji wa silaha, masharti kuhusiana na eneo la biashara la muuzaji, masharti ya kutolewa upya kwa kibali cha muuzaji na masharti ya kusitishwa, kufutwa kwa muda kwa kibali cha muuzaji wa silaha.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza masharti hayo yatajwe na sheria ili kuziba mwanya wa Waziri kutumia madaraka yake vibaya kwa kuweka masharti kandamizi au ya upendeleo kwa baadhi ya makundi ya wauzaji wa silaha.

Upekuzi na Ukamataji wa Silaha

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 54 cha muswada huu kinasema kwamba “Hakuna mashtaka au hatua zozote za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya Msajili au mtu mwingine yeyote aliyeidhinishwa anayetekeleza majukumu yoyote chini ya sheria hii kwa lolote atakalolitenda wa nia njema”

Mheshimiwa Spika, Hakuna utendaji bora usiokuwa na mipaka. Kifungu hiki kinaweza kutumika vibaya kwa kuwa kinatoa mwanya mkubwa kwa Msajili au afisa yeyote aliyeidhinishwa kupekua au kukamata silaha kufanya jambo lolote hata kama ni ovu kwa kisingizio cha “nia njema. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba sheria hii imtake msajili au afisa aliyeidhinishwa kuzingatia kanuni na taratibu za upekuzi na ukamataji, kwani kumiliki silaha kihalali sio kosa la jinai hivyo upekuzi na ukamataji uzingatie taratibu za kisheria hasa kwa wale wanaomiliki silaha kihalali.

Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya marekebisho ya baadhi ya vifungu yataletwa katika jedwali la marekebisho wakati wa Kamati ya Bunge zima.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, Imekuwa ni desturi kwa Serikali zilizoko madarakani kuleta miswada ya sheria kwa ajili ya kulinda maslahi yake yenyewe bila kujali maslahi mapana ya wananchi na taifa kwa jumla. Aidha, imekuwa ni desturi sheria nyingi kupitishwa haraka hara bila kupata maoni ya wadau wengi jambo ambalo husababisha sheria nyingi kupingwa kabla hata hazijaanza kutumika. Mfano halisi ni Muswada huu kutoshirikisha wadau ipasavyo. Wadau wengi walilalamika mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama kwamba hawakushirikishwa kabisa katika mchakato wa kuandaa muswada huu.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaihoji Serikali ni kwa nini inapuuza wadau katika sheria muhimu kama hii? Je, Serikali haioni kuna athari kubwa kiulinzi na kiusalama kwa kutowashirikisha wadau wakubwa wa silaha na risasi kama vile makampuni ya ulinzi binafsi, na wafanyabiashara wakubwa wa silaha hapa nchini?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasisitiza tena kwamba Amani na utulivu wa nchi hii hautategeme tu uwepo wa sheria ya udhibiti na usimamizi wa silaha na risasi bali uongozi unaozingatia misingi ya utawala bora, haki, usawa, ukweli na usitawi wa jamii nzima kwa jumla. Aidha, ugumu wa maisha unaosababishwa na umasikini uliokithiri kutokana na mfumuko wa bei, elimu duni, maradhi, ukosefu wa ajira, ukosefu wa maji safi na salama nk. ni viashiria vikubwa vya uvunjifu wa amani kuliko silaha na risasi ambazo Serikali inafanya bidii kubwa kutungia sheria.

Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni bado inaitaka Serikali kukumbuka na kuzingatia barabara masuwala manne muhimu iliyotahadharisha yasichezewe au kufanyiwa mzaha kwani yanaweza kuliingiza taifa katika machafuko.

Masuala hayo ni kuchezea haki ya mwananchi kujiandikisha kuwa mpiga kura, Kufanya Mzaha na uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi, Matumizi ya Kisiasa ya Jeshi la Polisi na Ulinzi wa Raia na Mali zao hususan ulinzi wa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).

Mheshimiwa Spika,Baada ya kusema hayo, kwaniaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, naomba kuwasilisha.

Godbless Jonathan Lema (Mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
NA WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI
19 Machi, 2015

No comments:

Post a Comment