Sunday, March 22, 2015

CHADEMA YAZIDI KUSAMBARATISHA NGOME ZA CCM


NA MWANDISHI WETU, SENGEREMA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetaja ngome saba za Mawaziri wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zilizosambaratishwa na kuchukuliwa na Chadema katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Ngome hizo ni pamoja na Jimbo la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Jimbo la Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Jimbo la Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Jimbo la Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, Jimbo la Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Stephen Wassira.

Mengine ni Jimbo la Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka pamoja na Jimbo analotoka Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, Januari Makamba na mengine mengi, na kwamba Mawaziri hao hawana sifa wala uwezo tena wa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Hayo yalibainishwa juzi na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalim, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Sengerema mjini hapa mkoani Mwanza.

Katika mkutano huo, Salum aliyeongozana na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho Taifa, Patrobas Katambi, alieleza kuwa Chadema na washirika wake wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), imezima ndoto za vigogo hao wa CCM kugombea urais 2015.

“Naomba leo niwatobolee siri hii. Ndani ya CCM mtu aliyekuwa wa kwanza kuwa na kiherehere cha kutaka kugombea urais alikuwa ni Dk. Harrison Mwakyembe, huyu mtu na Mawaziri wenzake niliowatajia mitaa yao wanayoishi ilichukuliwa na Chadema katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Yaani ni hivi, wakitaka kugombea urais lazima wathibitishe uraia wao kwa barua itakayoandikwa na Mwenyekiti wa Chadema katika maeneo yao wanayoishi. Kwa maana hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu njia ya Chadema na UKAWA kwenda Ikulu ni nyeupeee,” alisema Mwalim na kushangiliwa.

Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema (Zanzibar), aliwaambia wananchi kwamba UKAWA imejipanga vema kuchukuwa dola Oktoba mwaka huu, na Serikali yake itazingatia nyayo na misingi iliyoachwa na Mwalimu Julius kambarage Nyerere.

Mwalim aliitaja misingi hiyo kuwa ni uzalendo, uadilifu, uaminifu, utu na haki za binadamu, na kusema kwamba: “Utawala wa Nyerere ulikuwa imara kiuchumi kutokana na kuwepo kwa viwanda vingi nchini ambavyo kwa sasa vimeuzwa na kubinafsishwa na Serikali ya CCM,”.

Aliwaomba Watanzania kutokwenda kuipigia kura Katiba Mpya Inayopendekezwa kwa madai kwamba CCM na Serikali yake imetupa maoni ya wananchi yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Jaji Joseph Warioba, hivyo ni vema CCM ikaangushwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Pamoja na mambo mengine, Mwalim aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili wawe na shahada za kupigia kura Oktoba 2015 zitakazowawezesha kuiingiza madarakani Serikali ya UKAWA itakayokuwa na neema kwa Watanzania wote.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment