Wednesday, March 18, 2015

Chadema yaigaragaza CCM marudio uchaguzi serikali mitaa.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibuka na ushindi dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa marudio wa Serikali za Mitaa katika mtaa wa King'azi B, Kata ya Kwembe, jijini Dar es Salaam.

Uchaguzi huo uliofanyika juzi katika mazingira ya amani na utulivu, ulishirikisha wagombea wa nafasi ya mwenyekiti, wajumbe wa serikali ya mtaa na wa viti maalum kutoka vyama vya Chadema na CCM.

Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi huo, George Lupia, alisema kuwa Chadema kimeshinda nafasi zote hizo dhidi ya wapinzani wake CCM na hivyo kuwa viongozi wa mtaa huo.

Msimamizi huyo alisema kuwa mgombea wa Chadema, Donath Mtemekele, alishinda kwa kupata kura 585 huku wa CCM, Daud Ngaliba, akipata kura 376 na kwamba kura 18 ziliharibika.

Lupia alisema wananchi ambao walikuwa wamejiandikisha katika daftari wa wapigakura walikuwa ni 1352, lakini waliojitokeza kupiga kura ni 979.

Mtaa wa huo ulirudia uchaguzi baada ya uchaguzi wa Desemba 14, mwaka jana kuvurugika na kuahirishwa mara mbili kutokana na sababu mbalimbali.

Uchaguzi huo ulivurugika kutokana na vurugu ambazo zinadaiwa kufanywa na wafuasi wa vyama hivyo ambavyo vilikuwa vinachuana kuongoza mtaa huo.

Katika uchaguzi huo wa mwaka jana, ilidaiwa kuwa mgombea wa nafasi wa mwenyekiti kupitia Chadema alikuwa ameshinda kwa kura 312 huku wa CCM akipata kura 207.

Kufuatia ushindi huo, Chadema kimesema kitawatumikia ipasavyo wananchi wa eneo hilo ili kuwaletea maendeleo.

KAULI YA DK. SLAA
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema chama chao kimeupokea wa furaha ushindi huo akissema ukombozi umeanza kuonekana kutokana na wananchi kufanya uamuzi shahihi.

“Tumeupokea ushindi kwa furaha kwa mataokeo haya ni jinsi gani ukombozi umeanza kuonekana, wananchi wamemchagua kiongozi sahihi wananyemtaka kwa ridhaa yao,” alisema Dk. Slaa.

Dk. Slaa alisema kuwa kilicho mbele yao ni kuwatumikia wananchi kwa moyo mmoja na kuwaondelea kero zinazowakabili.

KATIBU KATA AZUNGUMZA
Naye Katibu wa Chadema wa Kata ya Kwembe, Raphael Gwelino, alisema siri ya kupata ushindi katika mtaa huo ni maanadalizi mazuri waliyoyafanya na kupambana na hujuma zote walizotaka kufanyiwa.

“Tunashukuru tumeshinda kwa kishindo, tulijiandaa vizuri pamoja na hujuma zote tulizotaka kufanyiwa, wananchi wamefurahi sana wametengeneza jeneza lina bendera ya Chama cha Mapinduzi, wanalipitisha mtaani,” alisema Gwelino.

Aidha, alisema watakuwa makini kusimamia miradi iliyopo katika mtaa huo ukiwamo mradi wa maji unaofadhiliwa na Saint Marry.

No comments:

Post a Comment