Friday, January 23, 2015

CC Chadema kujadili kura ya maoni, daftari, uchaguzi 2015

Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inakutana kwa lengo la kujadili ajenda nne kuu, mojawapo ikihusu hali ya ushirikiano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) iliyojitokeza katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ili kujiandaa vema kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Ukawa, ambayo ilianzishwa wakati wa mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba Februari, mwaka jana, inaundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, ambavyo vimetiliana saini makubaliano ya kushirikiana katika chaguzi zote.

Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema jana kuwa ajenda hizo zitajadiliwa katika kikao maalumu kilichoitishwa na Kamati Kuu ya Chadema, jijini Dar es Salaam kwa dharura leo.

Alisema Kamati Kuu inatarajia kuibuka na maamuzi mazito katika kikao hicho.

Ajenda nyingine ni pamoja na uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa BVR, ambao ufanisi wake umegubikwa na utata mwingi.

Nyingine ni mchakato wa kura ya maoni ya wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa rasimu ya katiba inayopendekezwa kutokana na sheria yake kukiukwa na hivyo, kufanya uwezekano wa kutekelezwa kwa matakwa ya sheria Aprili, mwaka huu, kama ilivyotangazwa na serikali kuwa ndoto.

Alisema ajenda hizo zitajadiliwa na baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wataalamu, wakiwamo wanasheria pamoja na sekretarieti ya chama hicho kabla ya kuibuka na maamuzi mazito.

No comments:

Post a Comment