Sunday, November 9, 2014

Mbowe: Vigogo CCM wamechota Sh1.2 mradi bomba la gesi

Nzega.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewatuhumu vigogo wa Serikali kwa ufisadi wa Dola 600 milioni za Marekani, sawa na Sh1.2 trilioni walizotumia katika mradi wa ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Bomba hilo lililoanza kujengwa mwaka jana, litasafirisha gesi asilia kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ili kuongeza vyanzo vya nishati ya umeme nchini.
Akihutubia wafuasi wa chama hicho jana kwenye ziara yake ya ‘Operesheni Delete CCM’ (ODC), Mbowe alidai kuwa fedha hizo walizojiongezea vigogo hao zimesababisha mradi huo sasa kugharimu Sh2.40 trilioni.
Alisema kuwa awali kampuni inayojenga bomba hilo, ilisema gharama halisi za mradi huo ilikuwa Sh1.20 trilioni, lakini wao wakaongeza mara mbili ya fedha hizo kwa manufaa yao binafsi.
Mbowe aliwaeleza wafuasi hao kuwa, vigogo wa ngazi za juu serikalini wamegawana kiasi hicho cha fedha kilichozidi.
“Huu ni ufisadi wa hali ya juu na nitathibitisha maelezo yangu popote nitakapotakiwa kufanya hivyo. Inaniuma sana, fedha hizi zitalipwa na Watanzania maskini, wakati nusu yake zimeingia kwenye mifuko ya vigogo,” alisema Mbowe.
Alisema kwamba kwa sasa vigogo wa CCM wanatafuta fedha za kugharimia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuwa ufisadi huo utasaidia kufanikisha malengo yao.
“Nawaomba wafuasi wa vyama vyote vya siasa tusibaguane kwa itikadi zetu za vyama, bali tushirikiane kupambana na ufisadi huu unaozidi kuwaletea umaskini wananchi,” alisema Mbowe ambaye anatembelea mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma, Morogoro na Dodoma.
Katika hatua nyingine, Mbowe alidai kuwa nusu ya wabunge wa CCM wamekaa bungeni huku wengine wakisinzia, lakini wananchi wanaowaongoza wana matatizo mengi yanayohitajika kutatuliwa kwa pamoja.
Mbowe alieleza kuwa yeye ameacha posho ya Sh300,000 na kufanya ziara kwa kutumia fedha zake binafsi kwa lengo la kuwaelimisha wananchi.
“Pale bungeni hamna jambo la maana linalofanyika zaidi ya kwenda kufuata posho. Ndiyo maana nimeamua kuondoka na kuachana na posho zao, ili nije niwape elimu,” alisema Mbowe.
Katika operesheni hiyo, Mbowe aliendelea kuvisisitizia vyama vya upinzani kushirikiana katika mambo wanayoyaamini kuwa ni ya msingi kama vile kuing’oa CCM.

No comments:

Post a Comment